(Hubiri nililolitoa sabato ya tarehe 6 Aprili, 2013, kanisa la SDA Magomeni-Tanga)
0. Utangulizi
“Unalionaje
Kanisa lako?” Swali hili moja lakini laweza kuamsha majibu mengi. Watu wana
mitazamo tofauti tofauti juu ya kanisa. Kwa macho ya mwingine kanisa ni kama
“kimbilio la wanyonge,” huku kwa mwingine ni kama “nyumba iliyohamwa siku
nyingi.” Kwa mwingine kanisa ni kama “mgodi wenye utajiri wa milele,” huku kwa
mwingine ni kama “shimo la mapokeo ya
zamani.” Kwa huyu KKKT ndilo kanisa, na
kwa yule SDA ndilo kanisa. Kanisa linaweza kuonekana vizuri kwa macho ya mmoja na
kwa mwingine likaoneka vibaya. Uzuri wa kitu upo katika macho ya mwonaji.
Lakini
uzuri wa macho wa kitu sio lazima ufanane na ubora wake katika uhalisia wake. Ndio
maana mwanamke niliyemwona mrembo jana leo ninamwona wa kawaida tu. Na kanisa
nililoliona limejaa ngano jana, leo naliona limesheheni magugu. Macho yetu
yanacheza-cheza, na hisia zetu huhamisha hamisha mitazamo yetu kama mawingu ya
angani yanavyosukumwa sukumwa na upepo. Kama mtu anakuuliza unalitazamaje
kanisa bora umwambie ukweli. Mwambie siwezi kukupatia kielelezo kinachofanana
na kanisa uso kwa uso, isipokuwa picha yake niliyoichora mimi akilini mwangu.
Tena
mwambie asipoteze muda wake na muda wako na swali lake. Mwambie, yupo wa kumuuliza, yaani Mungu. Mungu
ndiye mwenye kanisa na analitazama ndani na nje, juu na chini. Mungu pekee
analitazama kanisa katika uzuri wake na ubaya wake—hakuna kinachoweza kutoroka
macho ya Mungu; maana, macho yake yanawaka kama tochi. Ni Mungu pekee ndiye anayelitambua
kanisa katika uhalisia wake.
Na
hapo natamani kujua: hivi Mungu analitazamaje kanisa? Japo swali hili nauliza
leo, lakini jibu lake lilitolewa zamani kama injili ya Mathayo ilivyoandikwa
zamani. Katika injili ya Mathayo 16 Yesu anauliza mitazamo ya watu kwanza kumhusu
Yeye. “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa nani?” (fungu 13). Hivi watu
wananionaje? Kwa kuuliza swali hili, Yesu hakuwa anatafuta utambulisho wake,
kana kwamba hajifahamu. Hapa Yesu alitaka kujua maono yao juu yake, ili
awapatie maoni yake juu yao.
Na
Yesu akapewa majibu. Majibu yao yalikuwa tofauti-tofauti kulingana na maoni yao
yalivyokuwa yametofautiana. Kulikuwa na hao waliosema Yesu ni Yohana Mbatizaji;
wengine walisema Yesu ni Eliya; Yesu ni Yeremia; Yesu ni mmojawapo wa manabii.
Bila shaka Yesu alihuzunishwa na majibu yao. Kwa sababu Yesu alikuwa zaidi ya
Yohana Mbatizaji, Eliya, Yeremia, au nabii. Yesu aliona jinsi watu
walivyochagua kumchora mawazoni mwao kama walivyopenda na si kumtazama kama
alivyojitambulisha kwao.
Ndipo
Yesu akawageukia wanafunzi wake na kutaka kujua wanamtambuaje. Tusubiri tuone. Je,
wanafunzi watafumbia macho uungu wa Yesu na kuyakazia tu kwa ubinadamu wake?
Je, wanafunzi waliokuwa na nafasi ya kumtambua Yesu kwa miaka mitatu hivi
watamwona tu kama mmoja wa wacha Mungu wa zamani? Yesu alikuwa ana hamu kujua
wanafunzi wake wamechagua kumtambuaje.
Bahati
nzuri Petro akatoa jibu lililotuliza moyo wa Yesu. Petro akamwambia Yesu: “Wewe
ndiwe Kristo (Masihi-Mkombozi aliyetumwa na Mungu) na Mwana wa Mungu aliye
hai?” (Haleluya!). Na Yesu akampongeza haraka akimwambia, una bahati, huo sio
mtazamo wa kibinadamu. Ninajua macho ya watu yanavyotazama; kwa vyoyote, “mwili
na damu havikufunulia hili, bali baba yangu aliye mbinguni”(fungu la 18).
Katika
mazungumzo yaliyofuata; Yesu ni kama anasema, “kwa kuwa pamoja na ubinadamu
wangu umekubali kuniona kama Masihi na Mwana wa Mungu, nami sasa nitakueleza
ninavyokutazama wewe na wote wanaonikiri kama wewe. Niacheni sasa niwaambie
ninyi ni nani.” Na hebu tuone Yesu anawatambuaje waumini wake?
1. Kanisa ni Kama Jengo lililosimama Mwambani
Kwanza
kabisa ninamsikia Yesu anawatambua waumini wake kama Jengo lililosimama Mwambani (angalia nami fungu
la 18a): “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga
kanisa langu”. Ni mara mbili tu
katika shuhuda za Injili zote nne[1]
Yesu amekaririwa akitambua wafuasi wake kama kanisa (na kanisa likiwa na maana
rahisi ya jamii ya watu wa Mungu). Na hii ni mara yake ya kwanza kufanya hivyo.
Na
ili tulielewe vizuri kanisa kama linavyoonekana mbele ya Yesu ni vizuri
tutafute kuelewa ana maana gani anaposema, Wewe
ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu”? Yesu
analilinganishaje kanisa kama Jengo juu ya mwamba? Na Petro anahusikaje hapo?
Kuna uhusiano gani kati ya jamii ya waumini na
Petro na jengo na mwamba? Kwani Petro na jengo na mwamba vinawakilishaje
kanisa?
Tuanze
na Petro. Hebu turudie kumsikia Yesu akimpongeza Petro kwa kumkiri ilivyo sahihi.
Yesu anapompongeza anamwita kwa jina gani? Nasikia Yesu anamwita Petro kwa jina
lake la zamani (jina alilopewa na wazazi wake)-Simoni Baryona. Na Yesu
anapotaka kumhusisha na kanisa anatumia jina alilompatia kama mfuasi wake-Petro
(Yoh 1:42). Simoni Baryona, kama yeye, hana uhusiano wowote na hicho ambacho
Yesu anakwenda kukizingumzia kulihusu kanisa lake. Yesu anapomwita kwa jina
Simoni mwana wa Yona, anaharakisha kumkumbusha kuwa yeye ni Petro. Petro ni
jina la kiyunani (lunga ya waandishi wa Agano Jipya) lenye kumaanisha “mwamba/ jiwe kubwa”. Lakini
Petro na Yesu walizoelea kuzungumza lugha yao ya asili ya kiaramaki. Na jina la
Petro kwa kiaramaki ni Kefa, likiwa na maana ile ile ya “mwamba”. Bila shaka kauli
ya Yesu kwa Petro katika kiaramaki ilisikika hivi: “Wewe ndiwe Kefa (mwamba) na
juu ya kefa (mwamba) hili nitalijenga kanisa langu”.
Kwa
kauli hii, ni wazi kwamba Simon Baryona
ni mwamba na juu yake Kanisa litajengwa. Lakini kauli hii inanifanya
nisugue kichwa na kuuliza hivi, Simon
Baryona kweli ni mwamba? Mbona muda mchache baadaye Yesu alimwita Simon
Baryona “shetani”(Mathayo 16:23)? Inawezekanaje kanisa lisimame juu ya mwamba
wa namna hii? Simon Baryona ni mwamba?
Mbona wakati huo Yesu alimwambia Simon Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta
kama vile ngano, lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike [isipungue]?”
(Luka 22:31,32). Inawezekanaje Simon kama kweli ni mwamba ahofiwe
kurushwa-rushwa kama kijiwe kwenge ungo? Simoni
Baryona ni mwamba? Mbona baadaye mwamba ulisogea dhoruba ya mateso
ulipoipiga huko Gethsemani na katika nyua za Kuhani Mkuu? Ni mwamba gani
unaoweza kusogea? Simon Baryona ni
mwamba? Kanisa linawezaje kuwa imara kama litajengwa juu ya “kefa” hili na
mwamba huu? Bwana unamwona sawa sawa Simon Baryona? Simon mwana wa Yona ana
umwamba gani hata aweze kutoa usalama kwa kanisa litakalojengwa juu yake?
“Tulia”
namsikia Yesu akiniambia. Ni kweli Simon mwana wa Yona ni kama wana wengine
waliozaliwa na wanadamu. Lakini hapa ninamwona kama nilivyompatia jina Mwamba
alipochagua kuwa mfuasi wangu. Sasa hivi na hapa hapa Petro ameishi sawa sawa
na jina lake. Ninyi ni mashahidi: wengi wamechagua kuyumbishwa na upepo wa
maoni ya watu kunihusu mimi. Wengi wameniona kama Yohana Mbatizaji, Eliya,
Yeremia, na kama nabii tuu. Lakini Petro amekataa kuyumbishwa na maoni ya
wengi. Hapa Petro ameonesha ukefa au upetro au umbwamba. Petro ni muumini wa
kwanza kunikiri mimi kama Mwana wa Mungu. Imani ya Petro kwangu kwangu ni
msingi imara na salama ambao juu yake nitalijenga kanisa langu. Umwamba wa
Mwamba (Petro) ni imani yake kwa mwana wa Adamu kama Mkombozi na Mwana wa
Mungu.
Na
hebu tuulize historia, Je Yesu alijenga kanisa lake juu ya mwamba wa imani ya
Petro? Ni kweli:
- Katika mathayo 16:16 tunamkuta Petro kama mwanafunzi wa kwanza kumkiri Yesu mbele ya wanafunzi wenzake kama Mkombozi aliyetumwa na Mwana wa Mungu kabla wanafunzi wengine hawajafanya hivyo.
- Katika Matendo sura ya 2, tunamkuta tena Petro kama mhubiri wa kwanza kumkiri Yesu mbele ya wayahudi wenzake kama Masihi na Mwana wa Mungu kabla wahubiri wengine hawajafanya hivyo.
- Na katika Matendo sura ya 10 tunamkuta Petro kama mhubri wa kwanza kumkiri Yesu mbele ya wamataifa kama Masihi na Mwana wa Mungu kabla wahubiri wengine hawajafanya hivyo.
Kwa
kifupi historia takatifu inashuhudia kuwa kanisa limesimama juu ya imani
aliyokiri Petro. Na imani hiyo ni imani kama historia ya Ukristo
inavyodhihirisha. Miaka 2000 imekuja na kuondoka, mataifa yamekuja na kuondoka,
lakini kanisa limeendelea kuwepo likikiri kwamba Yesu ni Mkombozi na Bwana. Na
mpaka leo wakristo wapo na wataendelea kuwapo wanapoendelea kushiriki ungamo la
Petro: Yesu ni Mkombozi wa Ulimwengu na Mwana wa Mungu.
Haikuwa
rahisi mara zote kwa Petro kumkiri Yesu kama alivyo mbele ya watu waliokataa
kumtambua Yesu. Petro alipigwa viboko, tupwa gerezani, na mwishoni kusulubiwa
kama Bwana wake. Haijawa rahisi kwa waumini wa Kristo kushikilia imani yao huku
wakikabiliwa na vitisho na upanga na
njaa na dhiki na adha na dhihaka. Lakini ni imani yao ndiyo iliyowafanya
waendele kuwepo. Ni imani yao imara kama ilivyo ya Ki-Petro ndio iliyowafanya
wasalie kama jengo lililojengwa mwambani.
Na
hakuna msingi imara mwingine tuliopewa kusimamia isipokuwa imani yetu kwa Yesu.
Hatuwezi kubakia kama wafuasi wa Yesu kama tutasita kumtangaza Yesu kama Kristo
na Mwana wa Mungu. Inawezekana kwa kumtangaza hivyo tutaonekana hatuvumilii
dini za wengine au tunavuruga amani na utengamano katika jamii. Inawezekana kwa
kumkiri Yesu tukaonekana wajinga wasiokwenda na wakati; kwa kuwa, wasomi na
watu maarufu hawamwoni mwana wa Mariam kama Mwana wa Mungu, hawamwoni mwalimu
wa Galilaya kama Mkombozi wa dunia yote. Inawezekana wengi wakataka
kumwona Yesu kama wanavyotaka kumwona;
yaani, nabii tu, mwalimu tu, mponyaji tu, mshauri tu. Lakini sisi hatuwezi
kukubaliana na mitazamo yao isiyotulia kama mchanga wa baharini na tukabakia
wakristo shupavu. Inahitajika imani kali kumtangaza Yesu kama Mwokozi na Bwana ukiwapo
nyumbani na kazini na mjini; na hiyo ndiyo imani imara kama jengo mwambani. Bila kujali kisomo
chao, makabila yao, au madhehebu yao, hakika waumini wasio na haya kumtangaza
Yesu alivyo, ndio Kanisa litakalosalia kuwepo mpaka mwisho wa wakati.
Kanisa
la Mungu ni Jengo linalosimama juu ya mwamba wa imani. Ndivyo linavyosimama
mbele ya macho ya Yesu.
2. Kanisa ni kama Jeshi lililoko uwanja wa vita
Yesu
aliposema atalijenga kanisa lake mwambani hakutaka tufikiri litakuwa salama
mbali na hatari na ushindani. Maana, Yesu analitambua pia kanisa lake kama
Jeshi lililo katika uwanja wa vita (angalia
Math 16:18b). Yesu anasema, “milango
ya kuzimu haitalishinda [kanisa langu].” Kanisa ni kama Jeshi lililoko
vitani likipambana.
Lakini
linashindana na nani? Yesu ameweka wazi, Kanisa linashindana na “milango ya
kuzimu”. Na kuzimu haiwakilishi kitu kingine isipokuwa mauti na kifo (uf 1:18).
Mahali pengine tunasoma kwamba dhambi huzaa mauti (Yakobo 1:15). Na kama dhambi
huzaa mauti, basi kanisa linapambana na dhambi kama mzazi na mauti kama mtoto.
Adui wa kanisa sio wewe sio mimi na wala si wao; adui wa kanisa sio wapagani,
adui wa kanisa sio viongozi wake wala washiriki wake; isipokuwa tu kama ni
vibaraka wa dhambi na mauti.
Kanisa
liko vitani, na Yesu anataka tulitazame hivyo. Kanisa halijatulia na haliwezi
kutulia. Mpaka limeondolewa uwanjani mwa vita, mbali na dhambi na kifo, kanisa
haliwezi kutulia. Wale wanaolilia utulivu na amani watusubiri malangoni mwa
Yerusalemu. Huko ndiko hakuna maombolezo wala kilio wala maumivu (ufu 21:4).
Wale wanaolalamikia magugu yamezidi kanisani, au uovu umezidi kulinukisha
kanisa, au siasa zimezidi kulichafua kanisa waliacha kanisa la Mungu. Wanyamaze
wakisubiri siku ya hukumu ifike; siku ambayo wema na wabaya watatenganishwa
milele na vita dhidi ya wema na uovu itamalizwa milele. Kabla ya hapo kila
mmoja sharti aelewe Kanisa ni Jeshi lililoko vitani na hivyo ndivyo Yesu
anavyoliona.
Wewe
na mimi tuko vitani. Inawezekana tumemkimbia Yesu, tumemkana hadharani au
sirini, hilo lisitukatishe tamaa. Tukumbuke tuko vitani. Tunaweza kutetereka na kujeruhiwa,
si neno, kwa hatutaitupilia mbali imani
yetu. Mapambano yanaweza kuwa makali na majeraha yakatuliza usiku na mchana,
lakini hatutaachilia imani yetu kwa Yesu. Vidole vya wanaotushtumu na
kutushtaki vinaweza kutusonda na kutukumbusha tulivyomkana Yesu, lakini
hatutakata tamaa kutumaini wema wake kutusamehe na uweza wake kutusimamisha
tena. Kama tutabakia uwanjani mwa vita na silaha ya imani yetu kwake ikisalia
mikononi, hakika tutasonga mbele kwa ushindi hadi ushindi.
Yesu
amekwisha sema, “milango ya kuzimu” haitatushinda. Haleluya! Ijumaa adui
anaweza kudhuru miili yetu, Ijumaa adui anaweza kukimbiza marafiki zetu mbali
nasi, Ijumaa adui anaweza kutupiga mapigo, akanyanganya nguo zetu na heshima
yetu. Lakini, bado ijumaa tunaweza kukabidhi roho zetu kwake Yeye awezaye
kuzitunza. Kama jiwe la adui lilishindwa kumzuilia Yesu kaburini jumapili ile
ya ufufuo, kadhalika hata sisi “milango ya kuzimu haitatushinda.”
Kanisa
ni imara kama Jengo mwambani na hodari kama Askari vitani. Na ninafurahi kuwa
ndivyo Yesu anavyowatazama waumini wake.
3. Kanisa kama mlinzi wa malango ya Ufalme
Mwishoni,
katika aya yetu Yesu anamalizia kulitambulisha kanisa kama Mlinzi wa malango ya
ufalme (angalia nami fungu la 19): “Nami
nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni”. Kefa nitakupa wewe funguo [ni wewe ukisimama pamoja na
waumini wote watakao nikiri mimi}. Wewe ni mshika funguo, mlinzi katika malango
ya ufalme. Unaweza kufunga na kufungua, kuruhusu na kuzuia, wewe ni mlinzi.
Lakini
Petro na wote wenye imani kama yeye ni walinzi wa namna gani mlangoni pa ufalme?
Petro anaweza kufungulia au kuzuilia nini mlangoni mwa ufalme? Kabla
hatujalielewa hilo: unakumbuka maneno ya Yesu kwa walimu wa dini katika Luka
11:52? Yesu alisema, “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa
maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.” Mahali
pengine Yesu anawalaumu Mafarisayo (washika dini) kwa kosa hilo hilo (Math
23:13). Mara zote hizo funguo zinasimama badala ya maarifa na ujuzi waliopewa.
Wana-sheria na Mafarisayo walikuwa na ujuzi wa maandiko ambao ungeweza
kuwanufaisha wao na wengine. Lakini hawakutumia maarifa hayo ipasavyo.
Na kwa
Petro na waumini wote, ujuzi na maarifa ya ufalme umetolewa.
Petro
na waumini tumefunuliwa na Baba wa mbinguni kumwona Yesu kama Masihi na Mwana
wa Mungu. Ufunuo huo ni ufunguo langoni mwa ufalme. Injili ya Yesu yaweza
kuwafungulia malango ya ufalme wote wanaoipokea na kuwafungia malango hayo hayo
wanapoikataa. Petro na sisi tumepewa funguo nyeti.
Na
hivi Petro alizitumiaje funguo zake? Petro alizitumia funguo hizo mara nyingi:
- Mara ya kwanza ni siku ya Pentekoste alipowaonesha wayahudi kuwa Yesu ni Masihi na Mwana wa Mungu aliye hai. Akawaambia, “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi” (Mdo 2:38). Na siku ile maelfu walifunguliwa malango ya ufalme.
- Mara nyingine Petro alimfungulia malango ya ufalme, Kornelio na nyumba yake na wote wakaingia (Mdo 10).
- Mara nyingine Petro akiwa na Yohana alimfungulia kiwete malango ya ufalme naye akanyanyuka akiingia hekaluni akirukaruka kwa furaha.
- Mara nyingine Petro na Yohana wakawafungulia wasamaria nao wakapokea Roho Mtakatifu.
- Lakini mara nyingine Petro alimfungia Anania na Safira na hawakuingia katika ufalme.
Funguo
alizopewa Petro ndizo tulizopewa. Tumepewa kuwafungulia watu wamjue Yesu kama
Mkombozi nao wafunguliwe. Na kama kila mmoja wetu aliyepewa funguo hizi
atazitumia wangapi wangepokea msamaha wa dhambi, wangapi wangefunguliwa na
utumwa wa dhambi, wangapi wangepokea uponyaji. Wengi wamesimama langoni mwa
ufalme wakisubiria mtu awafungulie. Watu hao wapo magerezani na hospitalini na
kazini na manyumbani na kwenye facebook na kwenye youtube na kwenye simu.
Wafungulie, waingie. Zitumie funguo zako za ufalme.
0. Mwisho
Sihitaji
kuuliza tena unalionaje kanisa. Kristo mwenye kanisa amekwisha kulitambulisha
kanisa lake. Yesu ametuambia kuwa kanisa lake ni kama Jengo mwambani, askari
vitani, na mlinzi mlangoni. Yesu anakwambia unabakia salama unaponiamini, unapata
ushindi unaponiamini, na uwasaidie wengine waniamini.
Na
Mungu akubariki unapomtambua Yesu kama alivyo, akubariki unapojitambua kama anavyokutambua,
na akubari unaposaidia wengine wamtambue. Mtambue, jitambue, watambue.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni