Utangulizi
1 Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya
Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu.
2 Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao
Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha,
ambalo lilikuwa nabaraza tano zenye matao.
3 Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi
wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza.*fa*
4 missing 4maana mara kwa mara malaika
alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza
kuingia majini baada yamaji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.
5 Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa
mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane.
6 Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo,
akatambua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, "Je,
wataka kupona?"
7 Naye akajibu, "Mheshimiwa, mimi sina
mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu
mwingine hunitangulia."
8 Yesu akamwambia, "Inuka, chukua mkeka
wako utembee."
9 Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake,
akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.
10 Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia
huyo mtu aliyeponywa, "Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako."
11 Lakini yeye akawaambia, "Yule mtu
aliyeniponya ndiye aliyeniambia: `Chukua mkeka wako, tembea."`
12 Nao wakamwuliza, "Huyo mtu aliyekwambia:
`Chukua mkeka wako, tembea,` ni nani?"
13 Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya,
maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa
wa watu.
14 Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo
aliyeponywa Hekaluni, akamwambia, "Sasa umepona; usitende dhambi tena,
usije ukapatwa na jambo bayazaidi."
Bethzatha

Swali “Je, Wataka Kupona? Limeulizwa katika kisa hiki. Kabla
hatujaelewa swali hili, nakualika tutembelee eneo la tukio, na kufuatilia kwa
karibu yaliyotokea katika hadithi hii. Kisa chenyewe kimetokea kandokando ya
bwawa lililoitwa Bethzatha. Bethzatha ni jina lilitoholewa na Yohana kutoka
kiebrania kwenda kwa kigiriki na limebakia hivyo hivyo katika biblia zetu za
kiswahili—Bethzatha. Yohana kama
mwanahistoria makini hakumuacha msomaji wake akisie mwonekano wa bwawa lenyewe.
Anatuambia kuwa bwawa lilikuwa limezungukwa na matao (mabaraza) matano. Kwa
muda mrefu wasomi wasioamini walidhani hadithi hii ni ya kutunga, wakisema eti
hakuna mahali kihistoria palipojulikana kama Bethzatha. Mpaka mwaka 1940
wafukuaji wa mambo ya kale (wajulikanao kama wana akiolojia) walipofanikiwa kupata jiwe la kale lenye jina
Bethzatha. Hivyo, hii si hadithi tu yenye fundisho. Hadithi ni ya hakika kama
Bethzatha yenyewe ilivyo mahali halisia.
Yohana akitusimulia kisa kwa nia ya kutuminisha zaidi
uhakika wa kihistoria wa hadithi yake anaendelea kutuambia Yesu alipitia lango gani
akiingia Yerusalemu. Anasema Yesu aliingia Bethzatha kupitia lango
lililojulikana kama “Lango la Kondoo” (leo watalii wanaozuru mji wa Yerusalemu
ya zamani wanaambiwa panaitwa “Lango la mtakatifu Stefano.”). Hili ni lango lililotumika kupitishia kondoo
ndani ya mji wa Yerusalemu tayari kwa mauzo kwa mahujaji. Yesu kama hujaji aliingia
mjini kwa kupitia lango hili, kaskazini-mashariki mwa mji. Karibu na soko hili
Yesu akakutana na Bethzatha yenyewe. Ukubwa wa Bethzatha ni futi 150 kwa 300;
kubwa la kutosha kupokea watu kwa mamia. Wenyeji wa Yerusalemu wanapaita mahali
hapa Bethzatha, huenda wakimaanisha "Nyumba ya Neema." Nyumba hii ni
bwawa la maji yanayoaminiwa kuponya maradhi. Na utaonai eneo limefurika
wagonjwa waliotafuta neema ya kufunguliwa (kumbuka watu walivyojaza kwa babu).
Anapokuja hapa Yesu anakutana na hospitali isiyo na kuta, kliniki ya iliyojaa
vipofu, na viwete, na walioopoza wakiwa wamejazana! (Fikiria harufu ya kondoo
upande huu na ya wagojwa upande huu, jiulize kwa nini Yesu aingie Yerusalemu
kupitia lango hili!)
Inaonekana hakuna anayefahamu mpaka sasa nani aliyeingia
hapa katika “Nyumba ya Neema.” Wagonjwa wa Bethzatha hawajui kuwa mahujaji
aliyetokea Galilaya ni Bingwa wa magojwa! Yesu anawatazama kwa huruma. Apande juu ya dari na atangaze kuwa saa ya
neema imefika? Apaze sauti yake kuwaambia amefika awasaidie? Kwamba sasa
anakwenda kuifunga hospitali hii na kuwarudisha wote nyumbani? Hapana. Huo sio
mpango-kazi wa Yesu. Huwa Yesu hatangazi kazi zake, ila kazi zake zinamtangaza.
Yesu akiwatazama wagonjwa, macho yake yakawa yakikimbia-kimbia kumpata mgonjwa
aliyechoka kupita wote.
Katika wagonjwa wote, Yesu akaamua kumkaribia mgonjwa mmoja
tu. Mgonjwa hajamwita Yesu na wala hamfahamu, lakini huyu ndiye anayetaka
kumponya. Mgonjwa hajawahi kuita ama kuimba “usinipite
Mwokozi, unapodhulu
wengine” lakini huyu ndiye Yesu anataka kumfikia. Kweli Bwana humrehemu
amurehemuye na kumbariki ambarikiye, bila kujali imani ya mpokeaji. Mgonjwa
huyu hana imani atapona tena. Mwanzoni aliamini atapona, lakini si sasa.
Mwanzoni ndugu na jamaa zake waliamini, hata wakasaidia kumleta yalipo maji ya
uzima. Lakini sasa hawaamini tena atapona, ndio maana wamemwacha mwenyewe. Kwa
miaka 38 ameteseka na sasa yupo hapa mwenyewe pembezoni mwa maji ya uponyaji
akisubiria uponyaji. Hana shamba, hana nyumba. Mali yake ni mkeka wake
anaoulalia. Mikono yake imekakamaa kwa kutembea chini akijibuluta kama
omba-omba. Ugonjwa wa kupooza miguu umewasababishia baadhi ya wagonjwa
kujikojolea bila wao kuwa na habari. Inawezekana Yesu anapomkaribia mgonjwa ana
harufu ya mkojo, mgonjwa amechoka!
Yesu anapomfikia, anainama kuanza kuongea naye. Hapo nyuma
ni Nikodemu kiongozi wa Kiyahudi na afisa mwingine wa kirumi ndio walioanza
kumsemesha Yesu. Lakini alipoongea na mwanamke msamaria aliyetengwa na sasa
mgonjwa mchovu ni Yesu ndiye anayeanza kuongea. Yesu anajali masikini zaidi ya
watu wote! Yes akamuuliza mgonjwa,"Je, Wataka Kupona?" Utadhani mgeni
huyu anayesimama mbele ya mgonjwa haoneshi kumjali mgonjwa; atamuulizaje
mgonjwa, "Je, Wataka Kupona?" Kwani yeye hajui mgonjwa yupo
Bethzatha?
Je, Wataka Kupona?
Je, Uko Tayari Kukaribiana na Changamoto za Mtu Mwenye Afya?
Kwa haraka haraka utadhani kumuuliza mgonjwa kama anataka kupona ni kufanyia mzaha zahama yake, lakini ukilitazama swali lenyewe kwa ukaribu haionekani hivyo. Mara nyingine wagonjwa hawataki kupona. Mgonjwa anapopona anakuwa amemaliza
seti moja ya matatizo lakini na kuibua mengine. Kuna changamoto za maisha
zinazowafikia walio na afya tu! Kwa upande wa mgonjwa huyu, kwa miaka 38
hajawahi kugombana na viongozi wa dini, lakini leo atakapotoka miguuni pa Yesu
atakabiliana na changamoto ya kutofautiana na viongozi wake wa dini. Atakapoponywa na
kuamuliwa kujitwika mkeka wake na aende atakuwa anakwenda kinyume na walimu
wake wa dini walivyomfundisha. Kumbuka kuwa kati ya mambo 39 wayahudi
waliyokatazwa kutoyafanya siku ya sabato kwa kuwa kwa kuyafanya ni kutenda kazi
mojawapo ni kubeba kitanda siku ya sabato. Mgonjwa yupo tayari kukutana na
changamoto ya kutofautiana na viongozi wake? Atakuwa tayari kuwajibika kwa
matendo yake kama mtu mzima, au ataishia kusema, “msinilaumu mimi, si kosa
langu. Muulizeni aliyeniponya”?
Cha ajabu ndicho mzee huyu alichokifanya (fungu
10). Alipotakiwa kuwajibika kwa matendo yake inawezekana akafika mahali akasema
moyoni mwake, kuliko vita hii maisha yalikuwa bora pale kwenye mkeka wangu.
Yesu akatafuta kumwokoa mgonjwa huyu na majuto ya kuingia kwenye maisha ya
kujitegemea. Kwa lugha nyingine alikuwa anamuuliza, uko tayari kulipa gharama
ya kuwa mtu mzima? Unahiari kukabiliana na changamoto za Mtu mwenye afya?
Je, Uko Tayari Kupoteza Fursa za Kubakia “Kwenye Mkeka”?
Lakini Yesu ana nia nyingine anapouliza mgonjwa wa Bethzatha
swali hili. Kabla hajamponya, Yesu anamtaka ajihoji kama yupo tayari kupoteza
fursa alizokuwa akizifaidi kama mgonjwa. Kumbuka wagonjwa kama huyu katika
Yerusalemu ya karne ya kwanza walikuwa omba-omba. Omba-omba walijikimu maisha
kwa fadhila za mahujaji waliokuja kuabudu Yerusalemu. Na mahujaji waliamini
watapata thawabu kubwa
kwa kuwasaidia masikini wanapotembelea mji mtakatifu.
Mgonjwa alifaidi fursa zote hizi akiwa kwenye mkeka wake. Rafiki, Kuna fursa za
kubakia kwenye mkeka, na kabla ya kuponywa unahitajika kuhihari kupoteza faida
hizo:
- Ukiwa kitandani, shida ya kuamuka asubuhi kwenda shule haipo tena, Tuition huendi tena, homework hutakiwi kufanya tena; isipokuwa, unaletewa juisi, chips zinakaangwa, kuku wanapoteza maisha kwa ajili yako, unakaa ukiangalia TV muda wote. Lakini ukipona fursa zote hizi umezikosa. Je, wataka kupona?
- Ukiwa mlevi, unajisikia kuchangamka, aibu hupotea, huna mawazo ya kukusumbua: hufikirii Mungu amenikataza nini, hukifikirii nitailisha nini familia yangu. Lakini ukipona fursa zote hizi umezikosa. Je, wataka kupona?
- Ukiwa tapeli na fisadi, unajisikia mwerevu, unakula bila jasho, una muda wa kutosha kwa starehe zako. Lakini ukipona fursa zote hizi umezikosa. Je, wataka kupona?
- Ukiwa kwenye ndoa haramu, bado kuna heshima unayopata (nimeoa, nimeolewa) na matunzo unayofaidi. Lakini ukipona, fursa zote hizi umezikosa. Je, wataka kupona?
- Ukiwa mwenye hasira, umezoea kumkasirikia mwenzi wako wa zamani, wazazi wako au Mungu wako, kuna utamu fulani unausikia unapokasirika. Lakini ukipona utamu umeukosa. Je, wataka kupona?
- Yesu anapouliza, Je, unataka kupona? Kweli anahitaji kujua kama uko tayari kupoteza fursa zote unazozifaidi sasa uwapo kwenye mkeka wako.
Yesu amesimama pale pale na swali lile lile. Je unataka
kupona? Utamjibuje? Utajibu: “labda baadaye?”, “Ndiyo”, au “Hapana”?
"Ninataka kupona"
Bahati nzuri mgonjwa wa Bethzatha alitaka kupona. Japo
hakutoa jibu la moja kwa moja lakini alionesha anataka kupona. Akaanza
kumsimulia Yesu jinsi alivyohangaika kupata uponyaji bila mafanikio. Aliamini
kama kila mmoja mitaani alivyoamini kwamba maji katika bwawa hili yakitibuliwa
wa kwanza kuingia anapona. Imani yake ndiyo iliyomleta hapo, japo imani hiyo
bado haijazaa matunda. Anamweleza kuwa amekosa mtu wa kumudumbukiza haraka maji
yatibuliwapo. Utadhani anajaribu kumshawishi Yesu amsaidie kumtumbukiza siku
maji yakivurugwa eti na malaika.Shida yake alikosa njia sahii ya uponyaji. Yesu
akamsikiliza akimuhurumia. Bila kutafuta kumsahihisha kuwa imani yake kwa maji
haya ni potovu na yeye hana muda na hadithi za mitaani, Yesu akaamua sasa
kumponya.
"Simama, jitwike mkeka wako, uende"
Yesu akitambua mgonjwa hamtambui yeye ni nani, akaamua
kutoa amri ya kimamlaka: “Simama, jitwike mkeka wako, uende.”
“Simama, jitwike mkeka wako”
Ukinukuu maneno haya moja kwa moja toka kigiriki, lugha
aliyoitumia Yohana utaona maana iliyokusudiwa: Simama (kitendo cha mara
moja[aorist imperative]), jitwike mkeka wako (kitendo cha mara moja[aorist
imperative]). Yesu anatamka kwa kishindo na anataka kitendo cha mara moja. Mara moja aamuke
na aachane na mazingira ya ugonjwa wake. Hilo ni tendo la mara moja na upesi.
Yesu hamwachii mgonjwa asema, “asante sasa nimeweza kusimama, ila kkilago
changu nitakiacha hapa, ikitokea shida tena niikute nafasi yangu pembezoni mwa
maji ya uponyaji.” Hapana, Yesu anamtaka mgonjwa aachane na maisha yake ya
kale,. Aachane na aliyokuwa anayafanya. Anamtaka asimame na kujitwika godolo
lake.
Kama mgonjwa wa Bethzatha ukitaka kupona, “simama, jitwike godolo lako uende”:
- Ukitaka kuachana na ugonjwa uliokulaza miaka yote, nyanyuka tupa shuka na blanketi ondoka kitandani, simama jitwike godolo lako
- Ukitaka kupona kutoka uvivu na kutojituma, simama jitwike mkeka wako
- Ukitaka kupona kutoka kulazimika kufanya kazi na Sabato, achana na kazi hiyo, simama jitwike mkeka wako na uende.
- Ukitaka kupona unywaji, kamwage chupa iliyosalia kabatini, achana na wanywaji wenzako, usizubaye katika mazingira ya unywaji, simama jitwike godolo lako
- Ukitaka kupona na hasira dhidi ya mpenzi wako, achana na mawazo yanayoamsha hasira yako, acha kujihurumia, acha kivitazama vidonda au makovu uliyosababishiwa, simama jitwike mkeka wako.
- Ukitaka kupona kutoka mapenzi haramu, futa namba yake ya simu, usimpigie, usimtembelee, usiongee naye, simama jitwike mkeka wako.
Rafiki usisite kusimama na kujitwika gogoro lako. Kama kwa
kusimama na kujitwika mkeka wako unaogopa utapoteza fursa ya kuwa pembezoni mwa
bwawa la maji uliyoyaamini, tupilia mbali hofu yako, maana maji uliyoyaamini na
kuyasubiria hayaja kukusaidia na ukiendelea kubakia hapo utakufa tu.
Mpendwa, najua mazoea yanatabu. Tunajisikia salama tukibakia
kwenye mtindo wa maisha tuliyoyazoea. Lakini ndugu kama mazoea hayo hayatupi
usalama, ni bora kuchukua uamuzi mgumu: achana na mazoea hatarishi. Tumeona
Yesu akikutana baadaye na mgonjwa aliyepona na kumtahadharisha asirudie mtindo
wake wa maisha ya dhambi yasije yakampata makubwa zaidi ya yaliyompata! Kama
jicho lako, au mkono wako au miguu yako inakukosesha achanana viungo vyako,
vingo’oe na vitupilie mbali, ni bora uingie uzimani ukiwa mpungufu kuliko
kuingia Jehanamu ukiwa na viungo na mazoea yako hatarishi
“...uende”
Tumesema ukiyasoma maneno aliyotumia Yesu katika lugha ya
mwandishi utaona maana iliyokusudiwa ikibaki wazi: Simama na Jitwike
[aorist imperative] ilikuwa ni amri ya mara kwa kitendo cha mara moja. Lakini
sasa tunaposoma agizo la mwisho katika lungha hiyo hiyo ya awali (kiyunani)
tunakuta Yesu anamtaka mgonjwa afanye kitendo cha mara kwa mara. Yesu
anapomuagiza mgonjwa Uende, Yesu anamwambia mgonjwa adumu kutembea. Mgonjwa
asiache kutembea, aendelee kutembea.
Mgonjwa wa kupooza aliyeponywa baada ya kusimama na mkeka
kichwani angeweza kusema, “ndio nimesimama na godolo nimebeba, lakini miguu
bado inauma, sikuzoea kutembea, hebu nisimame kidogo.” Hilo Yesu hakulitaka
mgonjwa alifanye ndio maana akamwabia, “dumu kutembea”. Ushauri ambao Yesu
anampatia ni ushauri ambao daktari yeyote wa mifupa angempatia mgonjwa wa
Bethzatha. Mgonjwa wa mifupa ni lazima atembee mara kwa mara! Mgonjwa wa
Bethzatha ni lazima adumu kutembea. Haitoshi asimame na kilago chake kichwani.
Haitoshi apige hatua moja au mbili na kutegemea atabakia mzima. Ndio maana Yesu
anamwambia dumu kutembea. Na
alichomwambia mgonjwa yule ndicho anatuambia sote: dumuni kutembea katika
maisha mapya!
- Haitoshi kuacha kulaghai na kutapeli kwa mwaka mzima, lakini ukibanwa sana unaongeza uongo kidogo ili ujikwamue, dumu kutembea katika mazoea mapya
- Haitoshi kuacha kuvuta au kunywa kilabuni, lakini nyumbani unatumia chupa moja au mbili, dumu kutembea katika mazoea mapya.
- Haitoshi kuacha kumsalimia mpenzi wako haramu kwa wiki moja, lakini wiki ya pili unasema hebu nimsalimie kidogo, dumu kutembea katika mazoea mapya
- Haitoshi kuacha kukasirika ukiwa ndani katika nyumba ya sala, lakini tukitoka ibaadani huwezi kumsalimia, tembea sasa katika mazoea mapya.
- Haitoshi kuanza kwenda katika nyumba ya ibaada kwa wiki mara moja au mbili lakini wiki zingine huuendi, dumu kutembea katika mazoea mapya
Rafiki huo ndio ukweli. Tukidumu kutembea katika uzima mpya
tuliopokea, tutabakia uzimani, na hakuna hatari kwamba tutarudi kifoni.
Mwisho
Kwa hiyo swali ambalo Yesu alilomuuliza mgonjwa wa Bethzatha
ndilo analomuuliza mtu yeyote anayetaka mabadiliko. Je, wataka kupona? Hili ni swali
linalostahili kujibiwa sasa kama wahitaji kupona sasa. Swali hilo linalenga
nini katika maisha yako? Unahitaji kupona kutoka shida gani? Kama Yesu hakuwa
na haja ya kukusaidia, unadhani angeuliza, unataka kupona?
Ombi pamoja nami ombi hili:
Bwana Yesu, hapa unasimama karibu yetu. Unajua mahali
ulipotukuta. Tupo penye mkeka wetu, wapweke katikati ya watu. Unajua kushindwa
kwetu maishani. Kama ni kushindwa kusamehe, kushindwa kupenda, au kushindwa
kuachana na mazoea yanayotuharibu, Bwana wewe watujua. Sasa Bwana, umetuuliza
leo kama tunataka kupona. Tusaidie tutake kusaidiwa. Tusaidie tuseme “Ndiyo,
Bwana, Ndiyo, Bwana”. Hapa hapa Bwana kuna mtu anaomba, “nataka nipone, niko
tayari kuponywa”. Bwana sikia maombi yetu. Sema nasi kwa sauti yenye nguvu na
ya uponyaji, gusa akili zetu na mioyo yetu, mpaka tusikie maneno yako, “inuka,
chukua mkeka wako uende” Tuachanishe Bwana na maisha yetu yaliyopita, na tembea
nasi katika upya wa maisha. Ameni
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni