30/05/2013

Mwanamume Huyu ni Nani? (Yoh 9)

Kabla ya Yote

Kati ya watu wote walioingia na kutoka katika jukwaa la historia, nani aliyegawa walimwengu kama mwanamume huyu? Alipotua tu juu ya uso wa sayari dunia, ripoti zinaonesha namna watu walitofautiana namna kumpokea. Mwandishi mmoja anasema wageni walisafiri umbali mrefu ili kumsujudia mtoto huyu wa kiume, huku wenyeji wakifanya mikutano mirefu ili kumuua. Mwingine anaandika kuwa alipokuwa angali mvulana mdogo, walimu wa dini waliinamisha masikio yao kumsikiliza, huku wazazi wake wakimnyoshe vidole kumgombeza. Na tena mwingine akaongeza kuwa alipotoa hotuba yake ya kwanza katika hadhara ya watu waliomfahamu tangu utoto wake, wasikilizaji walimsikia kwa furaha lakini muda mfupi baadaye waliziba masikio yao na kutaka kumfungia kufuli mdomo wake. Lakini ripoti inaendelea kuonesha mwanamume huyu aliendelea kuhutubia mikusanyiko midogo na mikubwa. Siku moja katika hotuba yake mwanamume alidai kuwa Yeye ni mkate ulioshuka toka mbinguni na wasikilizaji wake wanapaswa kumpokea nafsini kama chanzo pekee cha uhai.  Wachache waliweza kuyakubali madai hayo, lakini wafuasi wake wengi hawakuweza kumwelewa na walimwacha (Yoh 6:66). Viongozi wa dini na jamii waliposikia madai ya mwanaume huyu wakajaribu kutumia nyadhifa na nyenzo walizokuwa nazo kumdhibit mhubiri huyu asije akaligawa zaidi taifa. Viongozi wakatuma vyombo vya usalama kumkamata, laikini askari waliotumwa wakarudi na pingu tupu wakisema hatujawahi kusikia mwanamume anayenena kama mwanamume huyu  (7:32). Katika historia iliyoandikwa sijui mwanamume mwingine aliyewahi kuamsha hisia mchanganyiko kiasi hiki kama mwanamume huyu? Mtu huyo huyo akubaliwe na akataliwe, aheshimiwe na adharauliwe, apendwe na achukiwe?

Mwanamume huyo si mwingine ila Yesu wa Nazareti. Natamani kujua undani wa Yesu ili kubaini kwa nini watu watofautiane kumpokea kwa hisia zilizopishana kiasi hiki. Nitajaribu kurudi kwenye kurasa za historia na kufuatana naye anapopita katika barabara za vumbi za Palestina. Nitafuatana naye ili nisikie anasema nini na nimtazame anafanya nini huku nikifuatilia miitikio ya waliomshuhudia. Na ninaanza kukutana na Yesu kwenye injili ya Yohana sura ya tisa. Katika sura hii Yesu anafanya mambo ambayo hayajawahi kuonekana na anasema mambo ambayo hakuna mtu aliyewahi yasema.Mwanamume huyu nin nani?

Tukio A: “Nani katenda dhambi?”

Yesu anapita, anamwona kipofu. Wapo vipofu wengi hapa mjini Yerusalemu. Wengi wao ni upofu wanaupata ukubwani kwa sababu za uchafu, maji yenyewe hayawekwi dawa. Hapa kuna kipofu aliyezaliwa hivyo. Yesu anamwona kwa macho ya huruma. Lakini wanafunzi wanamwona kipofu huyu kwa macho ya udadisi. Wanafunzi wakimtazama kipofu huyu wakaona huo ndio wakati mwafaka wa kukata rufaa kwa Yesu kwa malumbano yaliyokuwa yakiendelea miongoni mwa wayahudi kuhusiana na uhusiano wa dhambi na ugonjwa. Wapo walioamini mtu anaweza kuumwa kwa sababu ametenda dhambi (wayahudi kwa ujumla wao waliamini afya ni baraka toka kwa Mungu na ugonjwa ni laana). Lakini kulikuwa na nadharia nyingine. Walimu wengine wa kiyahudi walifundisha hata kama mtu hajatenda dhambi maishani kabla ya kuumwa inawezekana alitenda kabla hajazaliwa (japo ilikuwa ngumu kuthibitisha hilo). Wapo wayahudi wengine walioamni mtu anaweza kuumwa kwa sababu wazazi wake walitenda dhambi (wakielewa yale maneno ya Torati kwamba Mungu huwapatiliza adhabu kwa maovu ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne cha wamchukiao).  Sasa kichwani mwa wanafunzi , swali halikuwa, je dhambi inaleta magonjwa, isipokuwa je, mdhambi yupi kaleta upofu huu? Sikiliza swali lao kwa maneno yao, “Rabi ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu”?(fungu, 2).

Yesu anajibuje swali la wanafunzi? Kwanza, Yesu anakanusha nadharia zote zilizotolewa kwamba mgojwa mwenyewe au wazazi wake walitenda dhambi ndio maana akazaliwa kipofu. Magonjwa mengine hayasababishwi na dhambi tuliyotenda bali ni maumbili dhaifu tuliyorithi. Kuna wagonjwa wa ukimwi waliozaliwa nao au kuambukizwa na wenzi wao wa ndoa. Kuna magonjwa ya kurithi au kuletewa. Usimtazame kipofu wa kuzaliwa au ukoo wake kama wadhambi. Hilo Yesu aliliweka wazi kabisa.
Lakini utata unajitokeza katika maelezo ya Yesu yanayofuata ufafanuzi huo. Ni kama Yesu anasema,  amekuwa kipofu ili Mungu ajidhihirishe! Sawa Yesu, kweli Mungu ni Mwenye enzi yote na anastahili kujidhirisha kwa wote wenye mwili, wenye afya na wasio na afya. Lakini Bwana wa dunia yote hapaswi kuwa Mungu wa haki? Je, Mwenyezi Mungu ana haki ya kumfanya mtu kipofu ili aoneshe uwezo wake wa kuponya? Bwana hivi hapa hautuchanganyi? Kama Mungu ana haki kuharibu ili atengeneze, mbona sauti ya haki ndani yangu inabisha na mimi nimeumbwa kwa mfano wake? Lakini hivi Yesu aliwaambia wanafunzi Mungu amemfanya mtu huyo kipofu iliajioneshe? Au kwa kusema hivyo tunamuwekea Yesu maneno mdomoni? 

Inawezekana shida haipo kwa kauli ya Yesu yenyewe ila kwa kauli ya Yesu kama ilivyotafsiriwa. Tukisoma kauli ya Yesu kama Yohana alivyoandika katika kiyunani tunaona kauli ya Yesu inaweza kufasiriwa tofauti na ilivyo sasa na kutusababishia tumfikirie Mungu vibaya. Tuanze na mstari wa tatu wa sura hii ya tisa. Yesu asema, “Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake” (weka nukta[.] hapa badala ya semi koloni[;]). Sehemu ya pili ya fungu la tatu inapaswa ianze na maneno, “Ili kwamba (neno la kigiriki hina ambalo linaweza kufasiriwa pia bali kama ilivyo kwenye tafsiri ya Union Version) kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake, imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi” (fungu 4). Hapa Yesu hakutoa tungo tata.

Kwa hiyo ni kama namsikia Yesu anawaambia wanafunzi wake; swala hapa sio nani katenda dhambi. Mimi ninapomtazama mgonjwa huyu ninaona fursa ya kazi. Nikitazama majeraha ya mtu simtazami kama polisi kutaka kujua ni nani aliyemsababishia nimtie nguvu. Mimi nikitazama udhaifu wako ninaona nimepata fursa ya kukuganga! Nimetumwa kama “Nuru ya Ulimwengu” (9: 5) Na ninakwenda kumtia nuru kipofu huyu. Ninajua kazi yangu itanitambulisha mimi ni nani japo utambulisho wangu unagawa watu. Ninajua sina muda, kama jua nimepewa masaa 12 tu kuangazia vipofu wapate kuona tena. Imenipasa kufanya kazi hii bila kujali matokeo. Ni lazima wajue mimi ni "Nuru ya Ulimwengu" (8:12).

Tukio B: Yesu akutana na kipofu mara ya kwanza

Alipokwisha kusema hayo Yesu akaendelea mbele na kazi yake. Kwa ujasiri mwingi na huruma tele akatema mate chini kutengeneza tope, akampaka kipofu mate usoni. Neno aliyekuwepo mwanzo wa uumbaji (Yoh 1:1-3) aliyetengeneza tope na kumuuba mtu wa kwanza (mwanzo 2:7), siye huyu amefanyika mwili na sasa anaumba tena? Wanafunzi wanaona hilo?  Yesu kwa kutema mate na kutengeneza tope ni kama anamkumbusha kila mtu kisa cha uumbaji na kuwaashiria kuwa yeye ni muumbaji na anaumba upya macho haya. Nani atamuona Yesu hivyo? Yesu akaendelea mbele kumtuma kipofu aende kunawa katika bwawa la Siloamu (maana yake, Aliyetumwa). Kipofu akakubali kufanya alichotumwa kukifanya, japo haikuwa rahisi kufanya hivyo. Kwanza mpaka hapo kipofu hajaahiwa kusikia vipofu wakinawa Siloamu wanapona. Pili vipi aibu ya kutembea na tope usoni? Tatu, kwa nini aende umbali huo mpak kisimani wakati angeyapata maji njiani kabla ya kufika huko? Mwanamume huyu anaagiza watu wafanye mambo ambayo hayaingii akilini. Lakini kipofu aliamini Yesu anaweza kuwa anania nzuri kwa kumpatia maagizo aina hiyo. Aliyaamini, aliyatii kwa kuende kunawa Siloamu. Na aliponawa, kipofu akarudi nyumbani anaona! Mara nyingi, maana ya maagizo ya Mwanamume huyu haionekani haraka akilini, lakini matokeo yake ni ya wazi machoni.

Tukio C: Majirani na Kipofu anayeona

Kipofu anayeona akarudi nyumbani na kuzua mshangao katika mitaa ya Yerusalemu—mitaa iliyojaa nyumba zilizobanana na majirani wanaofahamiana. Kundi la watu mtaani waliokuwa wakimfahamu kipofu kama omba-omba na kumsaidia njiani, walishtushwa kumuona  na kushindwa kukubaliana na ukweli uliokutana na macho yao. Wengine wakasema, “ndiye”; wengine, “siye ila anafananaye tu”! Kipofu mwenyewe akiingilia kati na kuzima malumbano kwa kusema, “ni mimi, ni mimi.” Watazamaji wakataka kujua alipataje kuona. Bila kumungunya maneno kipofu akajibu jinsi alivyoponywa: aliniwekea tope la mate machoni, akaniamuru niende kisimani kunawa, nikanawa na kurudi ninaona. Tangia hapo, hawakua na shaka kuwa ni yeye na aliponaje, lakini kilichowatatiza ni nani aliyeweza kufanya kitu hiki. Ni nani huyu aliyeweza kumponya kipofu tangu kuzaliwa? Ana mamlaka gani ya kuponya mlemavu wa aina hii, na amepata kibali cha nani kuponya siku ya Sabato, siku ya mapumziko, ambapo kazi yoyote ile hata ya uponyaji imepigwa marufu na viongozi wa dini?

Maswali hayo yalikuwa magumu mno kutatuliwa na wenyeji waliomfahamu kipofu huyu. Hivyo wakakata rufaa kuomba msaada kwa viongozi wa dini. Ninatamani kufuatilia viongozi wataamuaje kesi hii. Je, mtu aliyefanya uponyaji huu atakubalika kwa kazi nzuri aliyoifanya au atapingwa bila kujali kazi nzuri aliyoifanya?

Tukio D: Mafarisayo na Kipofu anayeona

Viongozi wa dini waliopelekewa kesi walijulikana kama mafarisayo, viongozi walioheshimika mbele ya jamii kwa uadilifu wao kwa katiba na sheria ya Israeli. Mafarisayo walimchukua aliyekuwa kipofu kwa mahujiano maalumu, kwanza wanataka kuhakiki kama ni kweli alitendewa muujiza:

Mafarisayo: Ulipataje kupona?
Aliyekuwa kipofu: Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona.
Mpaka hapo mafarisayo wakaona shida katika maelezo ya kipofu aliyepokea uponyaji. Hawakuguswa kwamba kipofu omba-omba sasa ni mzima, ila walitatizwa na mamlaka ya mtu aliyefanya kitendo hiki. Wengine wakasema Yesu hakufanya uponyaji kwa ridhaa ya Mungu, maana haishiki Sabato. Wakadai Yesu si chochote isipokuwa mvunja-sheria. Lakini wengine wakakataa na kusema mtu hawezi kuwa mvunja-sheria na hapo hapo Mungu amwezeshe kufanya muujiza huu. Basi baraza likagawanyika pasipo maamuzi kuchukuliwa: Yesu ni nani? Ndipo mafarisayo wakamgeukia kipofu kutaka kujua maoni yake.
Mafarisayo: Unamaoni gani juu ya mtu huyo. Wewe unahusika zaidi kujibu swali hili, maana ni macho yako aliyoyafungua.
Kipofu: Ni nabii. Kichwani Kipofu haoni tofauti ya Yesu na nabii Elisha eliyefanya miujiza mingi kwa idhini ya Mungu?, Jibu lake: Yesu ni nabii

Mpaka hapo mafarisayo hawakuridhika. Hawakudhani kuwa Yesu anaweza kuwa kama manabii wa kale waliofanya miujiza ya kweli; maana kulikuwepo na wazushi enzi hizo, watenda miujiza bandia.

Tukio E: Mafarisayo na Wazazi wa Kipofu anayeona

Basi wakataka ushahidi wa kutoka kwa chanzo sahii cha habari—wazazi wa kipofu. Wazazi watasemaje? Sikia mahojiano yao:

Mafarisayo: Mnamtambua mtu huyu, ni mtoto wenu? Mnakubali alizaliwa kipofu? Kama ndio, alipataje kuona?
Wazazi wa Kipofu: Tunajua ni mwana wetu, kweli alizaliwa kipofu, lakini kwa habari ya alipataje kupona hatujui. Muulizeni mwenyewe, atajisemea mwenyewe maana ni mtu mzima.

Wazazi walijua hatari ya kutoa ushahidi utakaothibitisha mamlaka ya Yesu juu ya magonjwa na mapokeo yao ya utunzaji Sabato. Waliambiwa yeyote atakayemkiri Yesu kama masihi atatupwa nje ya jamii ya Wayahudi. Nani anapenda kufutwa ushirika?

Tukio F: Mafarisayo na Kipofu anayeona

Mafarisayo wakamgeukia kipofu, na kutaka kumbana amkiri akili mamlaka ya Yesu ili wapate kumuadhibu.

Mafarisayo: mpe Mung utukufu. Tunajua huyo si nabii kama ulivyosema, ila mwenye dhambi
Kipofu: ni mwenye dhambi mimi sijui. Najua neno moja tu, nalikuwa kipofu na sasa naona
Mafarisayo: Alikutendea nini mpaka ukapata kuona?
Kipofu: Niliwaambia hamkunisikia na sasa mnaniuliza tena? Mnataka kuwa wanafunzi wake?
(Kauli hii toka kwa aliyekuwa kipofu, asiye msomi ilikuwa ni kama matusi kwa mafarisayo wasomi. Wakakasirika)
Mafarisayo: Labda wewe ndiwe mwanafunzi wake, sisi ni wanafunzi wa Musa mtoa Sheria. Huyu jamaa yako hata hatujui alikotoka (wenzetu enzi hizo umashuhuru wa mtu unauhusiano na alikotoka)
Kipofu: Hii ni ajabu mtu mashuhuri aliyeweza kunifungua macho hamjui alikotoka? Tunajua Mungu hutumia watu wema kufanya mema. Haijawahi kusika mtu amemfumbua macho kipofu wa tangu kuzaliwa.  Kama huyu mtu asingelitoka kwa Mungu mwema, asingeweza kufanya wema huo?
Mafarisayo: Ama wewe mtoto wa laana! Ulizaliwa katika dhambi tupu na unajaribu kutufundisha sisi?
(Wakamtupa nje)

Tukio G: Yesu na Kipofu aliyeponywa

Yesu kusikia wamemtoa nje akamfuata na kuanza kuhojiana naye.

Yesu: Unamwamini mwana wa mwanadamu, mjumbe wa Mungu?
Aliyekuwa Kipofu:Ni nani nipate kumwamini?
Yesu: Umekwisha muona, na ndiye anayesema nawe sasa
Aliyekuwa Kipofu: Naamini Bwana. Akaanguka chini kumsujudia
Yesu: Nimekuja ulimwenguni kuhukumu; na hukumu yangu ndio hii: wasioona waone, wanaoona wasione.
Mafarsayo: Unamaana umetuhukumu sisi kuwa wasioona?
Yesu: Kama mngekuwa hamuoni nisingewahukumu mnaona, lakini sasa mnasema mnaona huku hamuoni hamuna hudhuru na hukumu yenu ipo pale pale.

Mwanamume Huyu ni Nani? Majibu Mbalimbali

Katika injili ya Yohana miujiza ya Yesu inajulikana kama ishara. Na muujiza wa kuponywa kipofu ulikusudiwa kuamuashiria Yesu ni nani? Lakini makundi mbalimbali yaliyokutana na Yesu katika yaliitikia utambulisho wake tofauti tofaut kulingana na sababu zao mbalimbali.

Majirani wa Kipofu: Hawana Hamu Kujua Yesu ni Nani

Kundi la kwanza la watu walioshuhudia kazi ya Yesu ya kuwatia nuru watu ni majirani na waliomfahamu kipofu hapo mtaani. Hawa walishuhudia mtu waliyekuwa wakimuona mtaani kwao na kila mara wakimsaidia kama omba-omba eti sasa anaona! Walishangaa sana wakiulizana ni kweli? Walipojua kuwa ni kweli, wakakimbia kuwapasha habari viongozi wao. Hawa wapenda-umbeya hawana kazi nyingine isiipokuwa kusimulia kipya walichokiona. Hawana muda wa kutafakari walichokiona. Wanawashwa kusikia muujiza mpya, hotuba mpya, muziki mpya, lakini hawana muda wa kutafakari walichosikia kinamfunuaje Yesu kwao. Watu wa namna hii kwa kwa kukosa hamu kumjua Yesu, wanabakia katika upofu wao. Hapana sisi si watu wa aina hiyo. Sisi huwa tunaimba huku tukiomba, “nataka nimjue Yesu na nizidi kumfahamu, nijue Pendo lake kuu wokovu wake kamili. Zaidi, zaidi zaidi...."

Mafarisayo na Viongozi wa Dini: Hawataki Kujua Yesu ni Nani

Kundi la pili la watu waliokutana na ushahidi wa Yesu kama Nuru ya ulimwengu ni mafarisayo na viongozi wa dini. Hawa hawakutaka kujua Yesu ni nani. Na wanasababu zao.

Kwanza kama viongozi, hawataki kujua wasije wakaonekana hawajui. Walijiona kama viongozi wasomi, wakijiita wanafunzi wa Musa. Na kama wasomi walidhani wanajua sana kiasi cha kutotegemea kufundishwa na mtu yeyote. Waliamini viongozi waliosoma vitabu  kama wao hawezi kufundishwa na mtu ambaye hakwenda shule. Eti usomi ni kutojifunza tena! Na hata kipofu alipowaambia mtu  aliyenifungua macho si mwingine isipokuwa nabii, mtu aliyetoka kwa Mungu, walimtusi yeye na wazazi wake kwa kebei na dharau! Hivyo walimu wa hawa wa dini wakakataa kufundishwa na mwanafunzi wao na wakabakia katika upumbavu wao, bila ya wao kutambua Yesu ni nani hasa.

Wafuasi wa Yesu sio kama mafarisayo na hawapaswi kuwa kama wao. Tofauti na mafarisayo wakristo tunajua Yesu ni nuru ya ulimwengu. Ulimwengu wote unaangazwa na jua hili moja. Tofauti na mafarisayo walioamini Musa ni wa Waisraeli, na hasa wao walioisoma sheria yake, sisi wakristo tunafahamu Yesu wetu ni nuru inayomtia nuru kila mtu, wanaoona na wasioona, viongozi kwa wafuasi, wasomi kwa wasio wasomi. Tofauti na mafarisayo, sisi tunaamini kila mtu ameumbwa katika sura ya Mungu na kila mtu anaangaziwa na utukufu wa Kristo.

Na siku inakuja, nayo imefika ambapo wakristo hawatatafuta kuwa walimu zaidi kuliko wanafunzi na waumini hawatakuwa wepesi kusema kuliko kusikia. Siku hiyo wanaoona watafunguliwa macho na wasioona, wasomi wataelimishwa na wasio na elimu, viongozi watawasikiliza wafuasi wao. Na siku hiyo wakristo kwa waislamu, wakaloliki kwa waprotestanti, watunza jumapili kwa watunza jumamosi watafurahia kuutazama utukufu wa Mungu unaoonekana katika kipaji cha uso cha mwenzake, kila mtu atafaidika na uzoefu wa imani ya mtu mwingine. Na siku hiyo Kristo atajulikana kweli kama nuru ya kila mtu.
Ninajua siku hiyo inakuja maana sisi sio mafarisayo ambao walikataa kumtambua Yesu ni nani wakidhani wanajua kila kitu na hakuna wa kuwaambia kitu.

Lakini kuna sababu nyingine iliyowafanya mafarisayo kutotaka kumtambua Yesu. Madai ya Yesu kama mkombozi aliyesubiriwa yalitofautiana kabisa na elimu yao. Walijua mkombozi ajaye atakuwa mtu mashuhuri, na watu mashuhuri walijulikana kwa sehemu mashuhuri walikotoka. Sasa Yesu hawezi kuwa mashuhuri kama mkombozi maana hata hajulikani ametokea wapi. Wakahitimisha, Yesu hawezi kuwa masihi. Kadhalika wayahudi walijua mkombozi ajaye atakuwa kama Musa wa pili, iweje huyu Yesu aponye mtu katika siku ya mapumziko na hivyo kufanya kazi tofauti na Torati ya Musa tunavyoifundisha? Yesu-mvunja sheria hawezi kuwa Musa wa pili wala mkombozi wa Israeli. Mpaka hapo utaona Mafarisayo hawakuwa tayari habari yoyote mpya inayotofautiana mtizamo wao wa kidini.

Wazazi wa Kipofu: Hawana ujasiri kueleza Yesu ni Nani

Kundi la tatu lililoshuhudia jinsi uponyaji wa kipofu ulivyomtangaza Yesu ni wazazi wenyewe wa kipofu. Wao walijua lakini hawakuwa na ujasiri wa kueleza walichojua. Walijua mtoto wao aliyezaliwa kipofu ndiye anayesimama mbele yao anaona. Walijua aliyeweza kufanya hivyo ni mkombozi kutoka kwa Mungu. Miujiza ya namna hii ndio walisikia manabii wa kale wakiifanya, na manabii walitabiri masihi ajaye angefungua macho ya vipofu. Walijua Yesu aliyefanya hivi si mwingine ila masihi. Lakini walipoulizwa kushuhudia kwa maneno imani yao kwa aliyemponya mtoto wao, walikwepa kwa hofu ya kutengwa na kunyanyaswa na vyombo vya dola.

Mpaka injili ya Yohana inafungwa, hatujasikia wazazi wa kipofu wakiwa wanafunzi wa Yesu. Huwezi kumtambua Yesu ni nani bila kumtangaza na bado ukawa mfuasi wa Yesu. Imani isiyokugharimu haina thamani, ikikugharimu utaithamini. Kama unajua Yesu ni nani usiogope kumtangaza kwa gharama yoyote na utaufurahia uhusiano wako naye.

Kipofu Anayeona: Hana woga kukiri Yesu ni Nani

Kati ya makundi yote yaliyoshuhudia uponyaji alioufanya Yesu ni kipofu pekee aliyefunguliwa macho ndiye aliyepata kumtambua Yesu ni nani. Maneno ya Yesu yalidhirika ukweli wake: “mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao wasioona waone, na wanaoona wawe vipofu” (39). Nuru ya Yesu iliyomfungua kipofu haikumuangukia kwa ghafla na kwa wingi usoni hata kumpofusha asiuone utukufu wa Yesu. Yesu alijifunua kwake taratibu taratibu na kipofu hakusita kuifuata nuru iliyokuwa ikimuangazia hatu kwa hatua. Mwanzoni alipoulizwa majirani zake nani aliyekuponya, alijibu, “mtu yule aitwaye Yesu” (11), baada alipoulizwa na mafarisayo anamwonaje Yesu, alijibu bila woga, “nabii” (17) na baadaye kidogo akaongeza kusema Yesu ni mtenda miujiza aliyetoka kwa Mungu (30-33). Baadaye Yesu alipojitambulisha kwake hekaluni, akaanguka chini kumsujudia akimuita, “Bwana.”

Kipofu anayeoona ni mfano wa kuigwa wa namna sahii ya kumuitikia Yesu kama Nuru ya ulimwengu. Nuru inapokuangazia usiipuuze kuifuatilia kama majirani walivyoipuuza wakabakia gizani, usiiogope kuikuikubali hadharani kama wazazi wa kipofu walivyokwepa kuikiri wakabakia gizani, na wala usipingane nayo kwa nguvu kama mafarisayo ukabakia gizani. Kubali hivi leo kutembea nuruni

Yesu ni Nuru ya Ulimwengu

Siulizi tena kwa nini mwanamume huyu agawe watu. Kwa kauli na matendo Yesu alijitambulisha kama Nuru ya Ulimwengu na hasa katika sura ya tisa ya Yohana. Hakumungunya maneno aliponena na hakuficha matendo alipoyatenda. Alikuwa wazi kama nuru. Lakini kama ilivyo asili ya nuru Yesu huangaza na kutia giza. Kwa wanaomkubali Yeye ni taa iongozayo wanaomkata ni giza la kujikwaa. Nuru ni ile ile, lakini humtia nuru macho huyu na humtia giza mwinginge. Wasioona wanaona na wanaoona wasione. Uamuzi ni wa mpokeaji. Amua leo pamoja nami kumkubali mwanamume huyu ili upokee nuru na uzima na furaha!




Hakuna maoni: