10/09/2013

Mwana Mpotevu: Yesu Rafiki ya Wote (Luk 15:11-32)

Kabla ya Yote

Mafisadi. Matapeli. Majangili. Wapenda pesa. Waponda mali. Nani angependa kuwakaribia? Watu ambao majina yao yananuka kwa jamii, ni mwadilifu yupi anaweza kuwa rafiki? Lakini katika meza ya Luka 15 hao ndio wanaomzunguka Yesu. Watoza ushuru na wenye dhambi hawajakuja mezani kwa ajili ya chakula tu (kama pesa ya chakula wanayo). Wamekuja chakulani ili kumsikiliza Yesu. Kutoka midomoni mwake wanadaka maneno matamu kuliko hata chakula mezani. Katika Yesu wamekutana na rafiki anayewakubali bila kujali maovu yao—angalia anavyokula nao.


Lakini jambo la Yesu kula sahani moja na wahuni halijaonekana na halijazoeleka. Hatujaona kiongozi wa dini anayejichanganya na watu wote namna hii--hata watu wasioheshimu dini kwa matendo yao ya wazi, watu wanaojulikana na kila mtu kuwa ni “wenye dhambi”! Iweje mwalimu Yesu ajichanganye kiasi hiki na watoza ushuru? Hawa mawakala wa warumi, vibaraka wa wakoloni, wanaoshirikiana na warumi-wageni kukandamiza wayahudi wazawa ni wasaliti wakubwa na si watu kabisa.  Inakuwaje Yesu awachukulie kama watu wa maana? Mafarisayo, watetezi wa dini wanapomkuta Yesu mezani akiwa pamoja na watoza ushuru wanaanza kunungunika: "Haifai bwana! Yesu asijitafutie umaarufu hapa. Hakuna rabi yeyote aliyefanya hili. Hata kama anataka kuwahubiria hawezi kuwakaribia “wenye dhambi” kiasi hiki mezani?"

Yesu si mtu wa kujibu kila shtuma anayozushiwa, lakini kwa hii hawezi kunyamaza. Hivyo utamsikia akiinua sauti yake kujitetea. Na Yesu anapojitetea anataka wanyeji wake--"wenye dhambi"- waliopo pamoja naye mezani wamsikie; na ataka mafarisayo-wanung'unikaji wamuelewe. Hata wewe utafahamu kwa nini Yesu anapendelea kuwepo walipo “wenye dhambi”. Tulia sasa umsikie Yesu akisimulia kisa kinachojibu kashfa ya Yesu kula na watoza ushuru na wenye dhambi. Kisa kinapatikana katika sura ya 15 ya Injili kama ilivyoandikwa na Luka mtakatifu.

Baba, Kijana Mkubwa, na Kijana Mdogo (fungu 11)

Yesu anaanza na kusema, "kulikuwa na mtu mmoja mwenye wana wawili.” Japo kwa kauli hii hatuambiwi mengi kuhusiana na mtu huyu, zaidi ya kuwa ana wana wawili, mtu huyu kwa vyovyote ana wasifa zaidi ya huo. Baadaye utaona mtu huyu si masikini. Mtu awezaye kugharimia pati bila ya michango michango si maskini. Tena utaambiwa ana watu chini yake wa kumtumikia. Ana mavazi ya gharama kuvalisha wanae. Kwa hiyo, huenda mtu huyu ni mfanya biashara mkubwa au mkulima wa kufanikiwa.

Lakini katika nchi hii aishiyo mtu huyu  watu hawathamini mali tu bali pia watoto. Mali bila mtoto atakayeirithi, eti kwao ni kama kujirisha upepo, kazi bure. Bahati nzuri mtu huyu ana watoto wawili: mkubwa na mdogo. Kwa kawaida wakati wa kugawa urithi mzaliwa wa kwanza hupata mara mbili ya wadogo zake. Katika familia ya baba huyu tunategemea “siku ya arobaini”, wakati wa kumaliza msiba, mkubwa atapata theluthi mbili na mdogo ataambulia theluthi moja ya mali yote.

Kijana Mdogo anadai urithi wake (fungu 12)

Yesu anaendelea kusimulia katika fungu la kumi la mbili akisema yule mdogo, akamwambia baba yake: `Baba, nipe urithi wangu.` Naye baba akawagawia mali yake. 

Hatujawahi kusikia ombi la namna hii. Kijana hawezi kusubiri kupokea sehemu yake ya urithi babaye atakapofariki dunia. Baba bado yu hai na mali ndio inayomweka aendelee kuwepo, lakini kijana hatambui hilo. Anachojua hata kama baba anaishi hastahili kuishi. Kijana ndiye anayestahili kuishi. Eti baba alivyokula vimemtosha! Baba apotelee mbali, ila yeye apewe chake ili aendeshe maisha yake. Kwa lugha nyingine kijana mdogo anasema,  “Baba, nataka maisha yangu na wewe unasimama njiani mwangu. Sitasubiria mpaka uondoke. Nipishe, niondoke”

Kwa kuomba hivyo kijana ameumbuka, nia yake imefichuka. Kumbe anataka mali ya baba sio urithi wa baba. Angetaka urithi angefuata desturi za kupokea urithi. Kwanza kwa kawaida urithi hupokelewa bila kudaiwa. Na urithi ukipokelewa mrithi anatazamiwa kumuenzi Mrithishaji kwa kuutumia ipasavyo. Baraka na wajibu, urithi na majukumu  husindikizana siku zote. Hata siku za mzee Isaaka, urithi ulitolewa baada ya Yakobo mwanaye kutimiza wajibu wake. Ndio maana tunasema, kijana anataka mali ya baba na sio urithi wa baba. Na hilo ni hatari, kijana amevuka mstali mwekundu. Mali pasipo maadili ni laana. Kwa kudai mali na mali pekee kijana mdogo anataka balaa.

Nani kati yetu anayeweza kutimiza ombi la kijana huyu? Nani aweza mpa wembe  mwanaye anayelilia wembe akijua wembe unaenda kumkata? Nani aliye na shamba au biashara ya kifamilia inayofanikiwa anayeweza kusikiliza ombi la kijana huyu? Ampe mwanaye mali yake huku akijua inakwenda kupotea na kumpoteza kijana mwenyewe. Mzazi yupi aweza kufanya hivyo? Lakini Baba wa kijana ndicho anachokifanya. Baba akamsikiliza mwanaye na anawagawia wanae wote wawili  mali yake. 

Kijana Mdogo Aondoka Nyumbani (fungu 13)

Kabla kijana hajaondoka: Mahojiano 

Bila aibu Bwana mdogo anapokea sehemu ya tatu ya mali zote. Siku chache zinapita. Kijana anafanikiwa kuugeuza urithi wake kuwa fedha taslimu. Na sasa anataka akazitumie “nchi ya mbali”. Kijana anataka aondoke lakini baba ana moyo mzito, kama mama aliyemkubalia bintie aolewe lakini siku ya “send-off party” analia asitake aende.
Kabla kijana hajaondoka nyumbani Baba na kijana mdogo wana maongezi ya kuagana. Sikia wanavyoongea:

Kijana: “Baba nataka kuwa huru. Ni lazima unipe uhuru wangu. Siwezi kuendelea kuishi na sheria zote hizi zimenifunga. Nimekua sasa. Mimi ni mtu mzima kuyatambua mema na kujichagulia na kung’amua mabaya na kuyakimbia. Acha kunifuga nyumbani kama kuku wa kisasa. Kunifunga kama mtumwa anayekwenda kuuzwa Bagamoyo sitaki. Nataka nifunguliwe.  Nipe nafasi nipumue”

Baba: “Mwanangu, unafikiri hauko huru? Mbona wewe ni mtoto wa nyumbani. Kama mtoto una uhuru wa kunieleza haja za moyo wako nikakusikia. Mpaka sasa una uhuru wa kufaidi yote niliyonayo. Unaishi nyumbani, ufalme wangu upo mikononi mwako. Ninakuwekea mezani chakula asubuhi, mchana na jioni. Ninakuvisha mavazi ya hadhi yako. Hata siku moja hujalala nje. Vijana wa barabarani wangetamani kufaidi bahati hizi. Mwanangu mbona uko huru. Hata unapokosea nakusahiisha, unaposikitikia makosa kwa furaha na kusamehe. Mwanangu hujafungwa kwa yeyote. Unapokuwa nyumbani mwanangu hauko chini ya yeyote isipokuwa mimi. Na ninapokuwa juu yako, sikufanyii lolote lile isipokuwa kulinda uhuru wako; na bado unasema hauko huru?”

Kijana: “Baba nimechoka na jitihada zako za kulinda uhuru wangu. Huku kusahiishwa-sahiishwa, kufuatwa-fuatwa sipendi. Sitaki tena kusikia: kwa nini umechelewa kurudi nyumbani. Au kwa nini hukushiriki leo chakula cha mchana mezani. Mbona usiku huu umechelewa kurudi nyumbani. Nimechoka na nyumbani na niache niende ‘nchi ya mbali’.

Ninajua mbali na nyumbani sitasikia kelele za Mchungaji akinichunga: eti pita hapa lakini usipite pale, kula toka mti huu lakini usile matunda ya miti mingine, kunywa maji ya kisima cha nyumbani tu usinywe maji ya barabarani. Mbali na nyumbani sitasikia nikiitwa, “  uko wapi?” Baba ni lazima niachane na wewe. Ninajua katika nchi mbali na nyumbani nitakuwa huru kufanya ninachojisikia kufanya bila ya kubugudhiwa na kelele za eti “walinzi wa uhuru.”

Baba: “Mwanangu nenda pole. Uhuru wa kweli una mipaka ya kulindwa. Kufanya unachojisikia kufanya sio uhuru. Uhuru sio utumishi wa hisia; uhuru sio utumwa wa tamaa, wala ufungwa wa shauku. Na ninakwambia kweli tupu. Unapoitimizia hamu yako kupata pesa na mali na utajiri badala ya kukuachia, itaendelea kukushikiria usiponyoke mpaka imefirisi utu wako kama mwana. Unaposhikiriwa na tamaa ya kufurahisha nafsi na kukubalika na watu wewe si mwana huru bali mtumwa wa kuburutwa. Kijana wangu fikiria mara mbili uamuzi wako kabla kuondoka nyumbani.

Mazungumzo kati ya Baba na kijana hayakuendelea tena. Bado kijana amebakia na pamba masikioni; hakuna ushauri unaoweza kupenya. 

Kijana aondoka: Baba unamwacha aende?

Hivyo anaamua kuondoka nyumbani—nyumbani kuliko na upendo wa Baba, nyumbani kuliko na desturi zilizomkuza, nyumbani kuliko na maisha ya uhakika.

Baba anamtazama kijana mdogo akiondoka. Baba ana watumishi walio tayari kutii amri yake. Je, awaagize sasa wamzuie kijana mkaidi asivuke lango kuu la mji wake? Awaagize wamue kijana asiyesikia wazazi kama amri ya Musa inavyoagiza na hivyo kuepuka aibu na adha ya kuwa na mtoto mwenye kiburi? Baba ana haki ya kumlaani mtoto asiye sikia, lakini anamwancha kijana aende bila kumuingilia uamzi wake kumuacha.

Umewahi kuona mzazi kama Baba huyu? Baba anayempatia mwanae uhuru wa kutompenda na kutomtii. Machoni pa mzazi huyu uhuru wa uchaguzi ni wa thamani kama utii. Ni bora Baba akaye mwenyewe kuliko kumshikiria nyumbani mtoto ambaye moyo wake hauko naye. Upendo wa kweli haufurahii upendo wa kuigizwa au utii wa kujilazimisha.

Na kijana anachagua kumgeuzia mgongo babaye, anaondoka kweupe, jua likiwaka, na kila jicho linamuona. Anabamiza mlango usoni mwa Babaye na huyo anaondoka. Na anakwenda “nchi ya mbali” asikokujua Babaye isipokuwa  yeye mwenyewe. Hataki mtumishi aje nyuma yake kufuatilia nyayo za miguu yake.

Kweli kijana ameondoka, lakini ameacha pengo kubwa. Nafasi yake nyumbani haiwezi kuzibwa na yeyote. Hata kama Baba atapata mtoto mwingine, hawezi kuchukua nafasi ya kijana mdogo aliyeondoka. Ameondoka lakini hatasahaulika. Tazama Baba amemchora kijana kama tatoo katika viganja vya mikono yake na uso wake hautafutika katika kumbukumbu zake (Isa 49:16).

Kijana mdogo aingia Nchi ya mbali: Mashauri

Lakini kijana anapoingia katika “nchi ya mbali” anamsahau Babaye. Sauti za wenyeji wa nchi hii zinamhangaisha hata kumfanya hamsahau babaye kabisa. Kila mmoja anajaribu kumpatia kijana ramani ya nchi hii. Washauri ni mengi:
Wengine wanamwambia bwana mdogo: hapa ni mjini una uhuru wa kufanya chochote roho yako inachopenda. Usifuatilie mambo ya watu na hakuna atakaye hangaika na yako. Ukiona mtu amekabwa njiani, usisimame kumsahidia, ukipiga kelele utageuziwa kibao wewe na utapigwa. Usijifanye mlinzi wa ndugu yako. Mjini hapa tunasema “mind your own business”, jali mambo yako.

Wengine wanamshauri kijana: ukiwa nazo zitumie, ukizikosa zijutie. Wanamwambia katika nchi hii sherehe na pati zipo kila wikendi. Na bado kila jioni katikati ya juma ipo migahawa na vilabu unakoweza kujiachia. Kufa kuliumbwa. Ponda mali kufa kwaja. 

Wengine wamwambia thamani ya mtu iko katika uwingi wa marafiki alionao. Marafiki zaidi, mvuto zaidi. Utu wa mtu unaonekana katika kuchangia gharama za arusi na kusafirisha maiti. Nunua marafiki kwa kuwalipia vinywaji vya moto.. Usiridhike na mpenzi mmoja, panua wigo wa unyumba, ujiongezee watoto. Na ukifanya hivyo utakubalika na watu.

Wengine wanasema: Usikubali kuonekana dhaifu kwa yeyote. Kwa gharama yoyote jenga nyumba nzuri kupita zote mtaani. Nunua gari la kisasa zaidi ukiingia maofisini utashangaa unavyotetemekewa. Tunza ngozi yako ipendeze nao watakuja wenyewe. Vaa nguo za gharama hata watu wakikuona waseme anazo. Tafuta kuwa kichwa sio mkia, utadharauliwa. Hata ukipelekwa mahakamani kwa kesi ya kuku, kauze kiwanja, weka mwana sheria, na wataogopa kushindana na wewe.

Wengine wanamsisitizia: usilale. Kazana kujihangaikia hakuna atakaye kuangaikia. Kazi ndiye baba yako. Kazi yoyote inapokelewa kwa shukrani. Hakuna kazi haramu hapa mjini. Ili mradi inalipa fanya kazi. Ukiridhika umezipata ndio unaweza kwenda kanisani. Hapa hakuna kulala.

Kijana mdogo akiwa nchi ya mbali (fungu 14-16)

Apoteza Mali


Kijana amepewa ramani ya mji. Sasa anajua wenyeji wa Roma wanaishije Roma. Japokuwa yeye ni myahudi inabidi sasa aende na mazingira na aishi kama mrumi. Kwa kuwa amepata pesa ya mkupuo, pesa ya bingo, hawezi kutulia. Kijana amekuwa kiruka njia akitafuta kuonekana kwa watu kuwa anazo. Na ndani ya muda mfupi kijana amejulikana. Wenyeji wa mji hawamfahamu kwa jina lingine isipokuwa mwana mpotevu. Kijana ni mtumiaji wa pesa. Mara kanunua simu ya gharama. Mara kanywa bia ya gharama. Mara katembea na mpenzi mwingine. Kama nyuki wafuatavyo ua lililochanua, Bwana mdogo kokote anakokwenda anafuatwa na mashabiki na wadandiaji. Na ukimwona kijana anavutia--kijana amechanua kwa uzuri wa sura, ananukia pesa, damu inachemka; hajazeeka bwana, hajachoka eti. Kijana bado ana nguvu za kuhangaika kupoteza mali.

Lakini kwa nini tuseme kijana anapoteza mali? Hatumwonea kijana? Mali sio zake? Hakupewa na Babaye? Hana uhuru wa kuzitumia? Iweje tuseme anapoteza mali anapozitumia? Ni mali gani isiyotumika? Kusema ukweli, ikiwa mali ni za kijana hatuna haki kusema kijana anapoteza mali. Matumizi ya pesa ni manunuzi ya huduma. Lakini si hivyo kwa kesi ya kijana huyu. Mali aliyopewa bado ni ya Babaye. Wote tunatambua urithi siku zote unasindikizana na desturi. Na desturi ya urithi inatambua sauti ya Mrithishaji kwa mali inayorithishwa. Kijana hawezi kutumia mali kumsahau Mtoaji. Hayo si matumizi sahii. Huo ni upotevu wa mali.

Kijana hukupewa mali ili umsahau mtoaji. Umepewa mali na nguvu na mvuto na maisha kama urithi. Tumia urithi kumkumbuka Mpaji nawe utakuwa unatumia mali kwa usahii. Nunua chakula kwa utukufu wa Mungu, agiza vinywaji kwa utukufu wa Mungu, hudhuria sherehe kwa utukufu wa Mungu, kazike kwa utukufu wa Mungu, jenga nyumba kwa utukufu wa Mungu, jipatie mpenzi kwa utukufu wa Mungu, pata elimu kwa utukufu wa Mungu; kwa kifupi, fanya jambo lolote na rasilimali ulizopewa huku ukizingatia mapenzi ya Baba-Mtoaji. Na ukifanya hivyo hupotezi mali—na yeyote ile hana haki kukuita mwana mpotevu.

Apata Fedheha 

Lakini kijana wa mzee huyu ni mpotevu kweli kweli. Amepote mali zote kwa kuzitumia  pasipo kumkumbuka Babaye. Na mali aliyoitumia bwana mdogo haina baraka ya Baba, imepotelea katika mifuko ya kutoboka-toboka  asiione tena.

Tumeambiwa njaa kali imeanguka katika nchi hii. Na kijana hajapona. Mtazame  anaanza kuhangaika. Anahangaika na hakuna wa kumsaidia. Ua lililochanua na kuvutia sasa limenyauka na kukimbiwa. Anahangaika na hakuna anayemwonea huruma. Hapa ni mjini, bwana mdogo atajiju, hapa kila mmoja analia machozi yake.

Bwana mdogo inabidi ahangaikia tumbo lake, hivyo anaomba kibarua kwa mwenyeji mmoja wa nchi hii naye anampeleka shambani mwake kulisha nguruwe.  Tunavyo fahamu sisi  myahudi hafugi mnyama haramu kama nguruwe. Kwa matumizi gani? Myahudi hali nguruwe na wala hagusi mzoga wake. Kwa vyovyote mfugaji huyu si myahudi bali mmataifa. Na hili ni tatizo.

Ina maana kijana ameshindwa kuvumilia njaa hata kwenda kumtumikia kafiri? Tujuavyo sisi, myahudi wa karne ya kwanza hawezi kuingia katika nyumba ya asiye myahudi, kafiri-najisi, hata kula naye (Matendo 10), mbali ya kumlishia wanyama wake najisi-nguruwe. Iweje kijana mdogo anafanya hivyo? Kwa kufanya hivyo  kijana anatofauti gani na watoza ushuru wa siku hizi za Yesu wanaowatumikia Warumi makafiri tena kuwakusanyia kodi haramu kama nguruwe? Kodi dhalimu inaondeleza unyonyaji wa wakoloni-wawekezaji kwa wayahudi waliovamiwa katika nchi yao ya ahadi. Sawa na mtoza ushuru, kweli kijana amekosa kazi nyingine itakayomuwezesha kupeleka mkono kinywani? Ni haki atangulize masilahi ya tumbo mbele ya  utaifa wake, na uzalendo wake, na jina lake?

Si haki, lakini kijana aliyeishiwa anaona ni bora aaibike na kudharauliwa na wenzake kuliko ateseke na kuumizwa na njaa. Njaa inatesa na haitamuachia mpaka imemyonya damu yake na utu wake. Ndio maana kijana anaamua kufanya kazi haramu—kulisha nguruwe. Na kwa jinsi tumbo linavyomungurumia, anatamani kula maganda wanayokula hawa nguruwe, ila hata nayo ameyakosa, hakuna anayempa kitu, asubirie mshahara wake. 

Kijana Mdogo Anarudi Nyumbani (fungu 17-21)

Afikiri Kurudi 

Ndipo alipoanza kupata akili akafikiri: `Mbona kuna wafanyakazi wengi wa baba yangu wanaokula na kubakiza chakula mezani, nami ninakufa hapa kwa njaa? Nitarudi kwa baba yangu na kumwambia: Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia.  Sistahili hata kuitwa mwanao. Nifanye kama mmoja wa wafanyakazi wako.` 


Haleluya kijana amefunguka. Sauti ya mabembelezi haikuweza kupenya pamba aliyoishindilia kwenye masikio. Lakini sasa ngurumo ya njaa imezibua masikio. Na sasa anasikia upendo wa Baba ukimwita. Njaa inapotishia kuchukua uhai wake nchi ya mbali anasikia ukarimu wa Baba unamwita arudi nyumbani. Hana sababu ya kufa kama mtoto asiye na baba, na anasema, “nitarudi kwa baba yangu”. 

Na hata sasa namsikia anasema:
ü Maisha ya kulisha wengine huku mimi nikilia njaa yamenichosha, narudi kwa baba yangu.
ü Maisha ya kuhangaikia tumbo huku nikidharauliwa yamenichosha, narudi kwa baba yangu.
ü Maisha ya nchi ya mbali yamenichosha, naarudi kwa baba yangu.
Na anaporudi kijana anaimba akisema:
Nilipotoka kabisa sasa narudi, nikakawia dhambini sasa narudi.
Nimechoka maovuni, sasa narudi, pendo lako lanitosha Bwana narudi.
Ndilo tumaini langu, sasa narudi, Yesu alinifia sasa narudi.
Damu yake yanitosha, sasa narudi, unioshe safi-safi Bwana narudi.
Narudi nyumbani daima kwako, kwa upendo nipokee naja nyumbani.

Arudi 

Mtazame kijana mdogo anasafiri akirudi kwa baba yake. Akiwa bado yu mbali, baba yake anamwona, na kwa moyo wa huruma anamkimbilia, wanakijiji washangaa kulikoni mzee atimue akimbie kama mtoto! Kumetokea nini? Muda si muda kila mmoja anapata jibu. Mzee kamkumbatia mwanae na kumbusu. 

Kwa muda mwanawe anatekewa na mapokezi. Anajua mapokezi aliyoyapata ni ya mwana aliyerudi nyumbani, na moyoni anahisi kwa kuondoka nyumbani amepoteza jina na haki ya kuwa mwana. Msikie anavyomwambia babaye: `Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia. Sistahili hata kuitwa mwanao.`

Kijana Mdogo apokewa Nyumbani (fungu 22-32)

Baba ampokea kijana mpotevu (fungu 22-24)

Baba anamwelewa kijana anaposema amemkosea Mungu na yeye. Ni kweli usipomtii mzazi umemwasi Mungu, unapomyima mpenzi wako upendo umemnyima Mungu, unapomtusi mumeo umemtukana Mungu, unapompiga mkeo umemzaba Mungu, unapomchukia jirani yako umemchukia Mungu, maana Mungu na watu walioumbwa kwa sura yake ni wamoja. Baba anamwelewa kijana anapotambua hilo anapomwambia `Baba, nimemkosea Mungu, na nimekukosea wewe pia.'

Lakini Baba hamwelewi kijana kabisa anaposema, sistahili hata kuitwa mwanao.
Ni mzazi yupi kati yetu anayeweza kumkana mwanaye anapomnyea. Ikiwa sisi tulio waovu tunajua mtoto kwa mama hakui na kamwe hatuutupi mjongoo na kijiti chake, iweje Baba mwema asimhesabu kijana mpotevu kama mwanaye? Baba hawezi kumpoteza kijana mara ya pili. Mara ya kwanza aliondoka na alimkosa, ampoteze tena kwa kumfanya mtumishi? Hapana.


Baba akawaambia watumishi wake: `Haraka! Leteni nguo nzuri mkamvike kama mwanangu! Watumishi hawavai pete wala viatu, lakini yeye mvisheni! Mchinjeni ndama mnono, babukyu; tule kusherehekea! Kwa sababu huyu mwanangu alikuwa amekufa, kumbe yu mzima alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana.` Wakaanza kufanya sherehe. Wakapiga kelele na kucheka na kucheza. Baba na mwanaye na watumishi na majirani ndani ya ukumbi, si mdundo huo. 

Kijana Mkubwa akataa kumpokea kijana mpotevu (fungu 25-28b)

Sherehe zimepamba moto, lakini kaka mkubwa yupo bado shambani. Kaka anabidii ya kazi muda wote huu yuko shambani. Aanarudi sasa na kukaribia nyumbani na anasikia vifijo na ngoma.  Anamwita mmoja wa watumishi hapo barabarani, anamwuliza: `Kuna nini?`  Huyo mtumishi anamwambia: `Ndugu yako amerudi nyumbani, na baba yako amemchinjia ndama mnono kwa kuwa amempata akiwa salama salimini.`  Kaka mkubwa anawaka hasira hata anakataa kuingia nyumbani.

Baba amsihi Kijana Mkubwa kumkubali Kijana Mdogo (28a-32)

Baba yake anatoka nje na kumsihi aingie. Lakini yeye anamjibu: `Kumbuka! Miaka yote nimekutumikia, sijavunja amri yako hata mara moja. Umenipa nini? Hujanipa hata mwana mbuzi mmoja nikafanye sherehe pamoja na rafiki zangu!  Lakini mtoto wako huyu aliyekula mali yako pamoja na makahaba, mara tu alipokuja umemchinjia yule ndama mnono.` 

Masikini kaka mkubwa anatia huruma. Kumbe amekuwa akishika amri kwa sababu anataka babaye ampatie kitu fulani. Kumbe anaonekana mwaminifu, hata anachelewa shambani, ili aonekane. Hafanyi kama mwana wa nyumbani bali kama mtumishi wa kuajiliwa. Kumbe anatamani alipwea hata wa mwana mbuzi kama futa-jasho ya uaminifu wake. Maskini kaka mkubwa anasikitika uaminifu wake ni wa bure kwani hajaonekana.

Kaka mkubwa anatia huruma kama mafarisayo na viongozi wa dini wa siku za Yesu. Wanaonesha uaminifu kwa Mungu kwa lengo la kuonekana na watu. Kama kaka mkubwa mafarisayo wanasali sala ndefu hadharani ili waonekane ni watu wa maombi. Wanafunga na kujitangaza kwa midomo mikavu ili waonekane ni watu wa kujinyima. Wanakaa viti vya mbele ili waoneka ni watu wa heshima. Wanakataa kuhudhuria sherehe ambapo wenye dhambi wanapatikana ili waonekane ni watu wa uadilifu. Kaka mkubwa na mafarisayo wanashida yao moja: wana njaa ya kuangaliwa na watu.

Lakini wote kaka mkubwa na mafarisayo wanashida kubwa zaidi. Wanamlaumu mtu yeyote anayewaangalia wengine tofauti na wao. Wanajiona wao na wengine kuwa ni tofauti kabisa. Wao tu wanastahili upendeleo na si wengine. Wao tu ndio watoto wa baba na si wengine. Umemsikia kaka anavyomwambia babaye? Anasema, “Huyu mwana wako”. Hasemi “Huyu ndugu yangu”. Kwa kaka mkubwa, kijana aliyepoteza mali ya baba na makahaba si ndugu yake. Na baba akimchukulia bwana mdogo kama mwanae afanya makosa. Kula na mwenye dhambi ni kosa. Na kwa kosa hilo kaka mkubwa hataki kumsamehe baba na anakataa kwenye sherehe alipo mdhambi mfujaji.

Baba yake anamjibu: `Mwanangu, wewe uko pamoja nami siku zote, na kila nilicho nacho ni chako.  Ilitubidi kufanya sherehe na kufurahi, kwa sababu huyu ndugu yako alikuwa amekufa, kumbe yu mzima; alikuwa amepotea, lakini sasa amepatikana."`
Sijui kama kijana mkubwa alielewa au la; sijui kama alibadili mtazamo na kukubali kuingia ndani kusherehekea.

Mwisho

Kisa kimeishia hapo. Lakini ujumbe ambao Yesu alitaka mafarisayo, na wanafunzi, na watoza ushuru, waupate toka simulizi hii ndio huu:

Haijalishi umekosa mara ngapi na kwa kiasi gani yupo baba anayesamehe yote.
Haijalishi unajisikia vibaya kiasi gani, au wengine wanakufanya ujisikie vibaya kiasi gani, yupo baba anayesamehe kwa furaha.
Haijalishi wangapi wanakudharau hadharani au faraghani, yupo baba anayekutetea.
Kama unahisi umepotelea katika ulimwengu wako, na hakuna aliye tayari kukusikiliza, yupo baba anayekujali.
Nyumbani yupo baba anayesikia. Sauti ya kilio chako anaisikia. Hakuna chozi hata moja linalodondoka asilione.
Nyumbani yupo baba anayempokea mtoto aliyetengwa, mtoto aliyekuwa amekufa.
Nyumbani yupo baba anayekusubiri urudi.

Rafiki rudi sasa na umpatie baba sababu ya kufurahi. Unaporudi tambua nyumbani kutakuwa na pati na uso wa Mungu utang'aa kwa tabasamu.


Hakuna maoni: