17/09/2013

Mpya! Mahojiano Maalumu Kati ya Yesu na Nikodemu: Ripoti na Uchambuzi (Yohana 3:1-13)


Yesu: Mkuu wa Nuru


Habari Rafiki! Karibu kwenye mahojiano maalumu kati ya Yesu na Nikodemu. Awali ya yote, hebu nikuombe ufunge macho. Sijasema tuombe. Umefunga? Unaona nini?... Giza?

Kadhalika ukifungua tu injili ya Yohana utaona giza! Nalo giza ni nene na pana kiasi cha kuikosesha dunia uhai. Katika msimu huu “haki[ja]fanyika chochote kilichofanyika”. Dunia haina sura  wala maumbile isipokuwa utupu mweusi. Lakini Mungu hapendi giza litawale dunia.



Ndiyo maana nuru ikivamia giza, na “wala giza halikuiweza.” (1:5). Na bado vita yao kali inaendelea huku nuru  ikipambana kumtia “nuru kila mtu, akija katika ulimwengu” (1:9). Na si siri: matokeo ya nuru kuangaza ulimwenguni yanawekwa wazi na Yohana mwenyewe anaposema, “wote walio[i]pokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu” (1:12).

Ni bahati iliyoje kupokea nuru na kufanyika mtoto wa Mungu! Tofauti na mtoto wa mtaani, mtoto wa nyumbani mwa Baba ana uhakika wa maisha, ana Yesu aliye nuru na uzima. Na Yesu mwenyewe anaahidi wote wanaomwamini hawatatembea gizani kamwe (8:12). 

Nikodemu: Mtu wa Giza?

Baadaye kidogo, katika sura ya tatu, Yohana anaripoti juu ya mtu aliyetembea gizani, wakati wa usiku (2:2) kuja kukutana na Yesu aliye nuru ya ulimwengu. Japo anatembea gizani Yohana anatufahamisha mtu huyu ni nani.

Yohana anamtaja kwa jina la Nikodemu. Japo hatumfahamu kabisa, jina lake linaweza kutufunulia tabia yake. Kwanza, japo ni myahudi lakini ana jina la kigiriki. Tunajua kuwa katika karne hii ya kwanza kigiriki ni lugha ya kimataifa inayotawala shughuli za kibiashara na kielimu. (Unajua tena hapa Palestina wasomi na watu wanaoenda na wakati hujipa majina ya kigiriki). Huenda Nikodemu ni myahudi “aliyefunguka”. Swali ni kama Nikodemu atakuwa tayari kufunguka anapokutana na Yesu usiku huu.

Lakini jina la Nikodemu linatuashiria kitu kingine kuhusiana na tabia ya mtembezi huyu wa usiku. Jina lake katika ulimi wa kigiriki, Nikodemos, humaanisha, mshindi. Kama Nikodemu ni  mshindi nataka kujua kama ni jasiri au mwoga. Huku kumwendea Yesu gizani ni dalili ya ujasiri au uwoga?

Lakini Nikodemu-Mshindi anamwendea Yesu akitokea wapi? Sio siri anatokea Yerusalemu. Sasa wengi katika Yerusalemu, Nikodemu akiwemo, walivutiwa sana na ishara na maajabu yaliyofanywa na nabii tokea mkoa wa Galilaya, wanamwita Yesu (2:23-25; 3:2). Japokuwa wenyeji wengi wa Yerusalemu walizikubali kazi za Yesu, lakini wengi wao pia hawakumwamini kama masihi—mkombozi aliyetumwa na Mungu. Kwani kwa mujibu wa msaafu wao Masihi hatokei Galilaya! Masihi ni mtoto wa Daudi, mzaliwa wa mji wa Daudi-Bethlehemu. Na akili zao zinawaambia Yesu katokea Galilaya na si Bethlehemu. Kwa hiyo Yesu si masihi (7:41,52). Nikodemu, anamwendea Yesu usiku akitokea mji uliozama katika giza la kutooamini.

Sasa kama wazee  wa Yerusalemu hawamwoni mwalimu wa Galilaya kama masihi, iweje Nikodemu aende kinyume na maoni ya wenzake? Hata kama ishara za Yesu hapa majuzi  ziliwafurahisha watu wengi wa mitaani hapa Yerusalemu, lakini maajabu hayo yalikuwa  bugdha na udhia kwa viongozi wa jamii na serikali. Nikodemu atamwendeaje mtu aliyejichukulia madaraka mkononi ya kufukuza wafanya biashara hekaluni hata kuwakoseshea makuhani mapato (2:13-21)? Akimwendea Yesu makuhani-watawala watamwonaje? Kufanya hivyo inahitajika kuwa na moyo wa simba.

Ingawa Nikodemu hana ujasiri wa kumpongeza  mchana mvunjifu wa mfumo uliopo; moyoni anaona Yesu anastahili pongezi na tena kusikilizwa kwa ukaribu. Ndipo Nikodemos, anashinda hofu ya kutengwa na wenzake na kuchagua kumwendea Yesu. Potelea pote. Lakini anajaribu kuwa mwangalifu—angalia muda gani anamwendea.

Ni muda sasa umepita tangu jua lianguke magharibi.  Nikodemu anaangalia huku na huku, anajifunika weusi wa giza, na anashika njia, anapita mitaa miembamba ya Yerusalemu, anakwenda, anakwenda. Anapita lango la mji, anakwenda, anakwenda aliko Yesu-Taa . Hebu tumfuate nyuma yake ili tukamsikie Nikodemu, mgeni wa usiku, ana nini na Yesu?

Giza na Nuru uso kwa uso

Sasa Yesu amejipumzisha katika bustani moja, iliyoko pembezoni mwa kuta za Yerusalemu na Nikodemu anaingia. Faragha ya Yesu na wanafunzi wake imeingiliwa. Lakini, kwa upendo mgeni anapishwa kiti  akae, tena haraka. Ni sawa mgeni apishwe  haraka, kulingana na tamaduni zao. Si hata mwonekano wake unafanana na  hadhi aliyonayo—kilemba kichwani, kazu ndefu, ndevu  mpaka kifuani! Wanafunzi wanamwachia nafasi akae.

Waangalie wanafunzi wanavyoangaliana wanapompisha mgeni akae,  wasikie wakiulizana: “iweje kiongozi wa Yerusalemu amtafute mwalimu wetu usiku huu— wakati ambapo Yerusalemu haiko tayari kumuamini masihi tokea Galilaya? Amekuja kwa lipi?” Hebu tubaki pamoja na wanafunzi pembeni, tusikie Nikodemu anataka nini.

Nikodemu amgeukia Yesu: Sehemu ya I; Hongera mwalimu (fungu 2)


Akiwa ameketi chini anatamtazama mwenyeji wake Yesu, mgeni Nikodemu anajaribu kumfungulia zawadi mwenyeji wake. Anafungua kinywa chake na kumwagia Yesu salamu za hongera. Msikie anavyoanza, "Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye." (Yoh 3:2).

Kwa macho ya paka, Yesu anamtazama Nikodemu machoni akimmwagia pongezi. Upesi, Yesu anang’amua hitaji la mgeni wake. Analijua bila kuambiwa na wambeya au wanahabari. Na ni siri iliyo wazi kwamba Yesu “aliwajua wote; ... [kwani] alijua yaliyomo ndani ya mwanadamu” (2: 24-25). Hata moyo wa Nikodemu uko wazi mbele za Yesu kama kitabu kilichofunguliwa.

Lakini kwa kutokujua kuwa amesimama mbele ya Mjua Yote, Nikodemu amefanya kosa la ujuaji. Umemsikia amesemaje? Amesema “tunajua.”  “Mimi pamoja na wenzangu wa Yerusalemu tumeona mambo yako, na tunajua wewe ni mwalimu wa viwango, rabi mwenye mhuri wa Mungu”. Nikodemu alidhania amekuja kuitazama taa ya Galilaya, asijue kumbe ni Jua linalotazama watu.

Yesu amgeukia Nikodemu: Sehemu ya I; “Zaliwa Upya” (fungu 3)


Yesu anamtazama Nikodemu na yuko tayari kumjibu. Kwa sifa zilizomwagwa, ningekuwa mimi kwa lugha ya mama ningesema, ndaga fijo. Lakini Yesu hadakii pongezi na uchombezi wa Nikodemu kwa ahsante. Kwa Yesu sifa alizopewa ni kama mauwa yaliyonyauka na mapambo ya kukanyagwa.

Mwambie Nikodemu ameanza vibaya na asirudie tena. Asijaribu tena kumpandisha mwalimu wa Galilaya daraja mpaka usawa wa kimo chake kwa maneno yake matamu. Akifanya hivyo asidhani anamtendea Yesu fadhila.  Japo Yesu atokea Galilaya ya wamataifa na yeye atokea Yerusalemu, ajue kwamba Yesu ni wa viwango vya juu tayari, zaidi ya  Yerusalemu zaidi ya hekalu.

Yesu hawezi kumshukuru Nikodemu kwa kumtambua kama mwalimu mwenye kazi zinazoonekana. Kwani Yesu ni zaidi ya mwalimu mwenye muhuri wa Mungu au mtenda miujiza ya kushangaza. Mwambie Nikodemu kuwa, Yesu ni Mungu-Mwalimu aliyeshuka toka juu kumfunua Mungu kwa wanadamu (Angalia Yoh 1:18; 3:13). Yesu ni mng’ao wa utukufu wa Mungu na chapa ya nafsi yake (Ebr 1:3). Yesu ni “Nuru ya ulimwengu”! (8:12). Hivyo ndivyo Yesu alivyo; na anapendeza akisalia hivyo. Haitaji make-up au sifa-bandia ili apendeze!

Kama vile hajasikia hongera alizopewa, Yesu anamjibu  Nikodemu akisema, “Amini, amini, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa mbinguni.” (3:3)

Nikodemu elewa anayeongea nawe sasa ni mfalme na sasa anaonge habari za ufalme wake. Nakwambia, “hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu” (3:13)[1]. Mwana wa Adamu ameupokea tayari ufalme toka kwa Mzee wa siku (kumbuka alichokiona Danieli katika njozi za usiku. Daniel 7:13-14) na sasa ameshuka nao mpaka hapa chini. Yeyote amwaminiye mwana ana uzima ana ufalme (Yoh 3:36; Kol 3:4). Tazama ishara anazotenda Yesu, humwoni hapa mtu mwenye mfano wa mwanadamu, mfalme kweli kweli, tena aliye juu ya hekalu lote, na mamlaka zote, na maumbile yote. Lakini pasipo kuzaliwa mara ya pili, huwezi kuuona ufalme huu wa mbinguni.”

Maneno ya Yesu yanamwangukia Nikodemu  kama radi machoni na kumwacha kichwa-chini asijue aendeleze vipi mazungumzo. Anabaki akitikisa kichwa na kujiuliza, “nimesikia sawa? Mimi Nikodemu nizaliwe anothen  ndio niuone ufalme wa mbinguni?”

Nikodemu amgeukia Yesu: Sehemu ya II; Inawezekanaje? (fungu 4)


Yesu amemwambia Nikodemu “zaliwa anothen, ( ἄνωθεν ) ndipo utauona ufalmeAmetumia neno la kigiriki anothen—neno lenye maana ya tena au toka juu. Inaelekea Yesu ana maana zote mbili anapomwambia anapaswa azaliwe anothen, yaani tena na tokea juu.

Lakini Nikodemu akitikisa kichwa na kubabaika akili kwa mwangaza wa ukweli, akaona aiache maana ya anothen kama “kuzaliwa toka juu” na kudakia maana ya anothen kama “kuzaliwa mara ya pili” kama kinga yake ya usoni nuru isimchome. Msikie anavyohoji, “Awezaje mtu kuzaliwa akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa?” (3:4).

Pole Nikodemu, lakini huna sababu ya kutapa-tapa. Kwa nini ubabaike unapoambiwa uzaliwe anothen? Ninaposema zaliwa anothen yaani mara ya pili kwa vyovyote si maanishi urudi tumboni mwa mama yako. Kama ningemaanisha hivyo mbona ingekuwa kazi bure. Maana siku zote zao na mbegu hufanana na mtoto-nyoka na mama nyoka hufanana? Nikodemu hatakama ungeingia na kutoka tumboni mwa mamayo mara saba ungebakia na asili hiyo hiyo kama ya mamayo. Ninaposema zaliwa anothen sisemi rudi tumboni mwa mama yako urudi upya.

“Mwalimu katika Israeli” kumbuka kuwa walimu hutumia lugha za ishara kuelezea uhalisia wa kitu, na hapa ndicho ninachokifanya. Mbona wewe na wayahudi wenzako hutumia lugha ya kuzaliwa anothen kuashiria kuwa wasio wayahudi  wamebadilishwa kuwa wayahudi? Ni lipi gumu hapa lisiloeleweka? (Angalia 3:12)

Hapana hakuna gumu lolote isipokuwa mchezo wa mende. Hapa Nikodemu unakimbilia uvungu wa zuria kuepa nuru inayokumumlika; unatafuta kujificha kwenye malumbano ya hoja kuogopa kutazamana na ukweli unaomtazama. Hapa unahoji uhalali wangu kukutaka wewe mzee wa kiyahudi ubadilike upya kama mwongofu mpya wa uyahudi. Unadhani wasio wayahudi wana haja kuzaliwa anothen, lakini si wewe. Hauko tayari ukweli huu ukutazame.

Yesu amgeukia Nikodemu: Sehemu ya II; Zaliwa kwa Roho (fungu 5-6)


Na ukweli hauko tayari kumwachia Nikodemu ajifiche kwenye malumbano ya hoja, leo amepatikana. Umebaki pale pale ukimmulika. Yesu, aliye kweli na uzima (1 Yoh 5:20),  anamkazia macho Nikodemu na kumwambia, “Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuingia ufalme wa Mungu.” (f.5).

Nikodemu unahitaji kupokea macho mapya na moyo mpya kabla hujaweza kuuona ufalme ulioshushwa na Mungu-Binadamu. Unahitaji  mwanzo mpya, macho mapya, kabla hujaweza kuuona utawala wa Mungu unaofunuliwa na Yesu Mgalilaya. Bila mabadiliko hayo utaishia kuziona kazi zangu kama tu za nabii aliyejaliwa na Mungu (Yoh 3:2) na si za Mungu aliyefanyika mwili (Yoh 1:14). Utakuwa na utakapopokea moyo safi na tofauti maana utamwona Mungu ndani yangu (Math 5:8).

Nikodemu hebu nikuambie,“Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia” (Yoh 3:11). Na ninakushuhudia, “Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili” (f. 6a). Tunashuhudia katika mambo ya kidunia mtoto wa nyoka ni nyoka na mtoto wa mwili ni mwili. Mtu wa mwilini amezaliwa gizani na hupenda mama yake giza. “Nuru imekuja ulimwenguni na watu wakapenda giza kuliko kuipenda nuru kwa sababu matendo yao yalikuwa maovu” (Yoh 3:19). Mtu wa gizani hupenda kubakia gizani na hukaa mbali na nuru, akiogopa asije akakemewa na nuru akabadilika (Yoh 3:19-21). Nashuhudia: Kilichozaliwa kwa mwili hupenda kusalia katika mwili.

Hata wewe mwenyewe Nikodemu unaelewa jinsi watu wanavyopenda giza na kukataa nuru. Juzi-juzi nilifukuza wafanyabiasha hekaluni, nikawatoa nje kondoo na ng’ombe wao, nikapindua meza na kumwaga chini fedha zao. Na unakumbuka jinsi tendo hilo lilivyowakasirisha wakuu wa hekalu. Nikodemu nakushuhudia: mtu wa mwilini hapendi mabadiliko ya kiroho;  hapendi kuona ufalme wa roho unatimua ufalme wa mwili. Nimekwambia, “kilichozaliwa kwa mwili ni mwili”.

Wewe Nikodemu na wenzako kaeni mkijua tatizo lenu la kutokukubaliana na ufalme wangu ni tatizo la mfumo mzima wa mwili. Tatizo limeanzia moyoni na kuenea mwili mzima. Ni uovu toka utosini mpaka mguuni. Isaya alitabiri vema juu yenu. Ninyi [m]mekuwa kama mtu aliye mchafu na matendo ye[nu] ta haki tamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi” (Isaya 64:6a). Kama nikuanguka katika matope ya dhambi, mmeanguka, mkatenguka, mkapinda, nakubakia mkiwa mmeinamia uovu. Lakini tumaini lingalipo. Ikiwa kama wewe na wenzako uliowataja uliposema tunajua—wote walioangukia Yerusalemu na Alekzandria na Washington na Tanga na Arusha watakuwa safi tena basi wakaoge upya Yordani (haifai kunawa!) ikiwa watanyooshwa tena basi wazaliwe upya (mazoezi na nidhamu pekee haifai!) ikiwa mtazaliwa upya mtakuwa na asili tofauti kabisa; maana, “kilichozaliwa kwa mwili ni mwili”.

Na kuzaliwa upya ninakokuzungumzia kunawezekana, kunawezekana. Maana,   “kilichozaliwa kwa Roho ni roho” (f. 6b). Nikodemu, kaa ukijua kwamba ufalme wa Mungu ni wa kiroho (Mungu ni roho) na wanaouingia ni wa kiroho. Watu wa rohoni hawazaliwi na mama zao wa mwilini isipokuwa na Mama yao Roho Mtakatifu. Na kama mama yao alivyo ndivyo na wanae walivyo. Ni kwa uweza wa Roho tu, mtu aweza kuzaliwa katika ufalme wa Mungu.

Nikodemu funguka: mbele yako ni yeye aliyetajwa na Yohana mbatizaji kuwa angebatiza watu kwa Roho Mtakatifu(1:33). Nikodemu funguka: mruhusu Yesu akuzae kwa Roho. Funguka na ugeuke na ulale sawa na njia na utoke upya. Funguka na uzaliwe upya kama mtu wa rohoni! Na hapo ndipo utakapojua, kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

Unadhani kuzaliwa kwa roho haiwezekani? Lipi gumu kwa Roho ambaye hapo mwanzo alitulia juu ya uso wa maji akashiriki kujadili na kutekeleza ajenda ya uumbaji hapo  Mungu aliposema “natufanye mtu kwa mfano wetu”? (mw 1:26)? Iweje Roho Muumbaji ashindwe kuumba upya watu wa mwilini kuwa watu wa rohoni? Nikodemu, inawezekana kufanyika upya na kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

Mpaka hapo, Nikodemu amebaki kimya, mdomo wazi! Aseme nini. Akiri ameelewa, ameamini? Sidhani kama yupo tayari kwa sasa. Na anamwongezea dozi kumwelezea mchakato wa uzalishwaji wa Roho.

Nikodemu Roho (kigiriki, Pneuma) anafanya kazi kama Upepo (ambao pia huitwa Pneuma).  Pneuma (Upepo) ukivuma utauhisi machoni unapokugusa, lakini hutauona. Pneuma ukipitia miti utaona matawi yakicheza, lakini hutaona nyayo zake. Na vivyo hivyo Pneuma (Roho) akimzaa mtu huona Roho anafanya-fanyaje, lakini utaona matokeo ya kazi zake. Utaona mtu amebadilika na kuwa na  nuru mpya ya Roho, mtazamo mpya wa kiroho na mwelekeo mpya wa kiroho. (2:7-8). Na ndipo utaona nilichokuambia, kilichozaliwa kwa Roho ni roho.

Neno hilo linaweza kutimia kwako Nikodemu. Roho akikuzaa upya: wewe mtu wa mwilini utakuwa mtu wa rohoni; wewe mwoga wa macho ya watu utakuwa mwoga wa macho ya Mungu; wewe shabiki wa dini utakuwa mwongofu wa imani; wewe mpenda ushabiki utakuwa mpenda Neno; wewe mpenda ishara utakuwa mpenda Kristo. Ukimulikwa hutajitetea ili ubakie gizani isipokuwa utajisalimisha ili uachane na giza. Amini amini nakuambia Roho akikushukia Nikodemu utaona kwamba  kilichozaliwa kwa Roho ni roho na kilichozaliwa na mwili ni mwili.

Nikodemu amgeukia Yesu: Sehemu ya III; Inawezekanaje (fungu 9)


Hata baada ya nuru hiyo badala ya kuukubali ukweli, cha ajabu, Nikodemu anatafuta tena kujikinga kwa hoja nyingine ili nuru inayochoma isimuumize moyo. Msikie anavyouliza, “Yawezaje kuwa mambo haya?” (f. 9).

Yesu amgeukia Nikodemu: Sehemu ya III; Hufahamu kuwa hiyo ni kazi ya Roho? (fungu 10)


Hapo hapo bila kumchelewesha Yesu anamuuliza, “Je!, Wewe u mwalimu katika Israeli, na mambo haya huyafahamu!” (f. 10).

Safi! Ni vizuri Yesu ampashe mvivu wa kufikiri kwa swali-motomoto. Kwa vyovyote Nikodemu anafahamu kuzaliwa kwa Roho kunawezekanaje, ameambiwa tayari; iweje aulize “Yawezaje kuwa mambo haya”. Hilo ni swali la mchovu anayesinzia. Ni sawa aamshwe, apashwa, na afunguliwe macho kwa ukweli unaowasha.

Yesu anamtupia swali Nikodemu: Iweje mwalimu katika Israeli kama wewe  usifahamu somo la msingi kwa mwanafunzi wa awali wa imani (darasa la ubatizo)—somo la kuzaliwa upya? Kwa vyovyote unafahamu mambo haya:

ü Ninajua Nikodemu umesoma manabii kama Isaya (32:15-20) na Ezekieli (36:25-27) na Yoeli (2:28) waliotabiri juu ya kipindi cha ukombozi. Umesoma habari za kipindi  ambapo Roho wa Mungu anayebadilisha atamwagwa kwa Israeli kama gharika juu ya ardhi kavu. Nikodemu unafahamu mambo haya.

ü Nijuavyo Nikodemu unajua kuwa Roho ambaye atakayemwagwa atafanya upya mioyo ya Waisraeli. Umekwisha soma aya ya nabii Ezekieli isemayo, ”Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi  mtakuwa safi;...nami nitawapa ninyi moyo  mpya, nami nitatia roho mpya ndani  yenu" Ezekieli (36:25-27). Nikodemu unafahamu mambo haya.

ü Nikodemu unajua kuwa ninapozungumzia kuzaliwa kwa maji na kwa roho ninaashiria kipindi hicho cha mvua ya Roho kwa taifa kavu, kipindi cha ukombozi na mabadiliko na uamusho—kipindi kilichoanza kutimia tangu  siku za Yohana Mbatizaji. Kipindi cha ubatizo wa maji kama ishara ya kumgeukia Mungu na kufanywa upya. Kipindi kinachokamilishwa na ujio wa masihi anayebatiza kwa Roho na moto. Nikodemu unafahamu mambo haya.

ü Nikodemu unajua kuwa ninapokwambia unapaswa uzaliwe upya unaambiwa kipindi cha masihi ajaye kimefika; kwamba ubatizo wa Roho na moto unapatikana; na kwamba mbele yako anasimama Mkombozi aliyekuja kutekeleza hayo (Yoh 1:33). Nikodemu unafahamu mambo haya.

Nikodemu umefumbia macho ukweli na huhitaji ufafanuzi wa mambo haya. Funguka Nikodemu. Shida yako Nikodemu ni shida ya wenzako wa Yerusalemu: hamwukubali ushuhuda wetu. Sisi tuna hakika na tunachokishuhudia lakini ninyi mnatilia mashaka ushuhuda wetu (3:11,12). Shida yenu ni kuona mashaka na kutoamini.

Sizungumzi hivi kwa kuwa nimekuchoka na nataka uondoke. Hapana. Hata hivyo nimefurahi umekuja kuniona mahali patulivu kwa maongezi tulivu. Lakini labda nikupe pole. Ulikuja kwa nia ya kuichunguza Nuru itokayo Galilaya lakini kumbe nuru imekuchunguza wewe na kukuweka pagumu. Nuru imekutaka uniamini. “Aniaminiye [mimi] haukumiwi; asiyeamini amekwisha hukumiwa.” (3:18). Mpaka sasa hukumu haijatangazwa kwako. Una nafasi bado kuchagua. Unaporudi nyumbani una uamuzi wa kufanya; aidha urudi gizani au utembee nuruni. Mazungumzo yetu yanaweza kuishia hapa. Kwa heri,  unaweza kusuka au kunyoa (wigi halifai).

Giza au nuru: Chagua


Nikodemu anaaga akiwa na moyo mzito. Anaondoka kimwili lakini akili yake iko kwenye mahojiano yaliyoisha. Anajua  hakuna mtu anayenena kama Yesu. Aidha Yesu ni Mwalimu aliyeshuka au ni mwalimu anayejinyanyua. Swali analobaki ni hili: afanyeje na madai ya Yesu Mgalilaya.

Amefika nyumbani na mzigo huo. Sijui amweleze mkewe au afe nao kiume. Vyovyote, lakini Nikodemu anapaswa atue mzigo, na kufanya maamuzi magumu. Ni juu yake kubakia amejifunika usiku unaomsitiri mpaka sasa; au atupilie mbali blankenti leusi, anyanyuke na atembee akiifuata nuru inayomwangazia?  Nikodemu amenasa katikati ya giza linalomhifadhi na nuru inayomchungulia. Nikodemu amebanwa. Mwombee Nikodemos-Mshindi ashinde kiburi na woga, afanye uamuzi sahii.

Nikodemu na changamoto ya uamuzi kati ya nuru na giza


Rafiki, tunapo muombea Nikodemu ni vizuri tutambue uzito wa utata ulioko mbele yake. Injili ya Yesu inatofautiana kabisa na dini aliyoipokea toka kwa wazee wake. Kumbuka amefundishwa dini ni kushika amri za Mungu. Anaelewa ushikaji amri ni mlango wa kumuingiza mtu katika ufalme wa Mungu. Kama farisayo ameamini hilo kwa moyo wote, ametafuta kulitekeleza kwa nguvu zote,  na kufundisha wengine kwa akili zote. Na kwa mafanikio hayo ya kidini Nikodemu anajijua yeye ni myahudi kweli kweli, na ana tiketi ya kuingia katika ufalme wa Mungu. Iweje Yesu amwambie ukitaka uingie katika ufalme uzaliwa upya, uniamini mimi kama mkombozi aliyeshuka na utakuwa umeingia katika ufalme? Vipi mafanikio yake kushika amri hayana mchango wowote kumuingiza katika ufalme? Kazi yake yote ni bure? Aanze upya? Nikodemu ana uchaguzi mgumu wa kufanya: abakie na dini yake au amchague Yesu. Si uamuzi rahisi..Muombee afanye uamuzi sahii.

ü Si rahisi kwa mtu aliyeirithi imani toka kwa wazazi wake, akiamini dini yake inamfanya kuwa mtoto wa Mungu; halafu aambiwe wewe si mwana wa ufalme na akubali kirahisi! Muombee.

ü Si rahisi mtu anayejiamini na kuridhishwa na rekodi ya uaminifu wake kwa Mungu aambiwe rekodi yake ndefu inamakosa tangia mwanzo, na akubali bila ubishi. Muombee.

ü Si rahisi mtu aliyezoea kutoa zaka, kwenda kanisani, kukata nywele fupi, kuvaa nguo ndefu, kula mboga na matunda, kuimba kwaya, kutoa matangazo, kuendesha ibaada, akijua kwa kufanya hivyo anapata siti kwenye ufalme wa Mungu, halafu aambiwe hata hajakaribia langoni mwa ufalme na akubali bila mashaka. Muombee.

Na ukweli ambao Nikodemu anapaswa aukubali ndio huu: Hakuna dini kama dini inayoweza kumpaisha mtu mpaka mbingu ya tatu mpaka kwenye ufalme wa Mungu isipokuwa Kristo pekee. Amini-usiamini, anayetafuta kupaa na kumfikia Mungu kwa kushika dini au sheria kama farisayo Nikodemu wenzake walivyoamini (Gal 2:16; 3:10), anajichosha bure. Akipaa sana ataishia kwenye usawa wa kimo chake-hapo uwezo wake unapokomea. Hawezi kufika mbali. Kama mbingu zilivyo mbali na dunia ndivyo atakavyoendelea kubakia chini mbali na ufalme.

Ni Kristo pekee aliyeshuka ndiye anayeweza kumpandisha mtu mbingu. Yeye ndiye ngazi ya Yakobo, hakuna nyingine. Ni Yesu-Mkombozi tu hakuna zidio au punguzo. Ni kristo pekee na chochote kile kisitajwe. Kristo ndiye njia na uzima na ufalme. Kristo atosha. Nikodemu amini Yesu atosha; na aseme Yesu atosha; na kila mmoja aseme sasa: Yesu atosha!

Muumini na furaha ya Uchaguzi wa Nuru


kwa habari ya Nikodemu hatujui (na bado tunaendelea kumuombea), lakini sisi wanafunzi wake twasema Yesu atosha. Bwana asifiwe, tumemwona Yesu, tumeiona nuru!

ü Tumeona wazi kuwa dini ya kweli sio mwanadamu aliye chini kutaka kumfikia Mungu aliye juu; isipokuwa, Mungu aliye juu kumfikia mwanadamu aliye chini kupitia Kristo pekee. Bwana ashukuriwe, tumeiona nuru!

ü Halafu tumeona kumbe mwalimu wa Galilaya ni mwana pekee atokaye kwa Baba Mungu amejaa neema na kweli, Yeye ndiye ya mfalme na ufalme wenyewe (Yoh 1:14). Aliye na Mwana ana uzima na ufalme! Haleluya, tumeona nuru!

ü Kisha tumeona ufalme wa Mungu unaonekana popote mwana wake anapodhihirisha misuri yake ya kifalme kwa kuwahubiria maskini habari njema, kufungua macho ya vipofu, kuwaachia huru wanaoonewa, na kutangaza mwaka wa Bwana wa kufunguliwa-Jubilii (Luk 4:18; 7:22 linganisha na Yoh 2:23). Bwana ainuliwe, tumeiona nuru!

ü Tena tumeona hakuna dini au elimu au uzoefu unamuingiza mtu katika ufalme wa Mungu isipokuwa uweza wa Mungu mwenyewe. Tumeona mtu anapopokea uweza huo kwa imani ndipo anapokuwa mtoto wa Roho na mwana wa ufalme. Hivyo mfalme wangu anenapo namsikia, akwendako nakwenda, apendacho nakipenda, achukicho nakichukia. Kwani ninakuwa nimepokea  roho mpya na mtizamo mpya na maisha mapya Bwana ahimidiwe, tumeiona nuru, tumezaliwa upya!

Nasema tena, kwa habari ya Nikodemu hatujui anamwonaje Yesu Mgalilaya, na hatuwezi kumsemea; lakini sisi waumini wake tunasema Yesu ni habari njema ya ufalme!

Mwisho


Na tunapomaliza tafakari ya mahojiano ya Yesu na Nikodemu, hebu tusifu pamoja na mtunga zaburi (34:1-5):

“Nitamhimidi Bwana kila wakati/ sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itasifu,/ Wanyenyekevu  wasikie wakafurahi.
Mtukuzeni Bwana pamoja nami/ Na tuliadhimishe jina lake pamoja...
[Tu]kamwelekea macho [tu]katiwa nuru, wala nyuso [zetu] hazitaona haya.”

Haleluya! Hebu walioina nuru na waitikie, amina.

Ombi


Hebu tuombe: Bwana Yesu, unyanyuliwe juu kwa kuwa wewe u mfalme wetu, na umeruhusu nuru ya ufalme wako ituangazie. Miguuni pako, tunatupa taji zetu toka vichwani mwetu. Kwa furaha pokea taji zetu. Ni wewe  tu wastahili taji zote. Uzidi kung’aa na kujulikana.

Lakini Ikiwa Bwana kuna watu wa taifa lolote au taasisi yoyote au kamati yoyote, au kwaya yoyote au chama chochote wananasita kukupigia goti wewe kama mfalme wa wafalme, wahurumie maana wapo gizani. Bwana tunakuomba uwatamkie “iwe nuru” nao watafunguka.

Na ikiwa, Bwana, kama yupo hapa mtu anayelingia dini yake, tabia yake, wasifa wake, elimu yake, mafanikio yake, kazi yake, au talanta yake, amuru sasa iwe nuru na magamba macho pake yatadondoka, ili asijione bali akuone wewe tu.

Sasa Bwana nakuomba umwage roho. Zalisha leo kwa Roho wako mwanamke huyu na mwanaume yule katika ufalme wako. Kwa uweza wako fanikisha sasa kila goti kukunjwa kwa Yesu, na kila ulimi kukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA,  kwa utukufu wa Mungu Baba. (Filipo 2:10). Amina.





[1] linganisha na 6:38; 6:42

Hakuna maoni: