11/04/2013

NAMNA YA KUMSAIDIA MTOTO KUJENGA HAMU YA KUJISOMEA



uTANGULIZI

Kumsaidia mtoto kupenda kusoma ni zawadi kubwa unaweza kumpatia mwanao maishani. Watoto waliozoweshwa kusoma nyumbani (sio kufanya homework ya shule tuu) wameonekana kuwa na mafanikio makubwa kimasomo shuleni kuliko wale ambao hawasomi. Mtoto anaweza kunufaika kwa yafuatayo anapopenda kujisomea vitabu mbalimbali, magazeti, n.k.:

  • ·        anajiongezea maarifa,  
  • ·        anakuza fikra au mawazo yake
  • ·        anapanua upeo wake wa kuona na kuyanyambulisha mambo.
  • ·        zaidi anajiongezea kujiamini.


ZIFUATAZO NI mbinu CHACHE UNAWEZA KUTUMIA:  


1.     Waruhusu watoto waone mfano kwako. Hebu wakuone ukisoma biblia, kitabu, gazeti, novels, n.k..

2.     Ongea nao kuhusu vitabu ambavyo umekuwa ukisoma. Wasimulie jinsi ulivyonufaika navyo.

3.     Soma na watoto wako kila siku na muda maalum ambapo televishen imezimwa na mambo mengine yamesitishwa.  Kabla hawajalala wasomee kitabu. nenda nao chumbani na ingia kitandani nao au kaa kwenye kiti uwasomee somo fulani au hadithi.
     Waruhusu pia kuuliza maswali na wewe pia upate nafasi ya kuuliza maswali. Kwa kuongelea yale tusomayo pamoja inasisitizia kwenye bongo zetu yale tusomayo. Na zaidi inafanya mda ule kuwa wenye mvuto. Mwanao akiuliza swali la udadisi unaweza lingine ukampa nafasi ya kulifuatilia zaidi na atakapopata fumbuzi la swali lake atazidi kutambua umuhimu wa kujisomea.                                                                     Ibada za kila siku ni za msingi sana kwa watoto lakini pia kusoma nao aina nyingine za vitabu kutawanufaisha zaidi watoto wetu.

4.     Tayarisha notes fupifupi uwapatie wazisome, mfano hadithi za biblia, jinsi na umuhimu wa kutunza afya zetu, habari za watu maarufu, waliofanikiwa maishani, siasa, historia, n.k..

5.     Tafuta kufahamu nini mtoto anapenda, kama ni kupika mtafutie vitabu vya mapishi, kama ni wanyama basi vitabu vinavyohusu wanyama, kama michezo basi gazeti au vitabu kuhusu michezo mbalimbali n.k. mweleze jinsi hivyo vitabu vitakavyo mpatia ufahamu au ujuzi zaidi wa hicho kitu anachokipenda.

6.     Mfundishe tofauti za usomaji. Kusoma kutafuta kujua jambo fulani, kusoma kuelewa zaidi jambo fulani, na kusoma kwa kujiburudisha. Kuna habari nyingi na za kila aina, upatikanaji wake ni rahisi zaidi na popote mfano tovuti (internet) kwa computer au hata kwa simu n.k..  Hivyo basi ni muhimu kumfundisha mwanao namna ya kuchuja habari zenye manufaa kwake na habari zisizo na manufaa kwake, zenye kujenga na zenye kuharibu. 

7.     Mpongeze mwanao kwa kusoma. Kama kunajambo zuri amefanya na unatamani kumpatia zawadi, kwenda kwenye duka la vitabu na kumpatia nafasi ya kutafuta kitabu anachopenda, hii inaweza kuwa zawadi nzuri.


MWISHO

Kumbuka kwamba muda huu ni wa pekee kwako na wanao kujenga mahusiano. Baada ya siku ya maangaiko na shughuli nyingi hatimaye watoto wanapata nafasi ya utulivu na wewe.  Kwa hiyo fanya muda huu uwe wa kufurahisha na kuburudisha.

Imeandaliwa na:  Aika Mwakalindile


Hakuna maoni: