Mchungaji, Vijana, na Sex?
I
|
weje mimi kama mchungaji nikutane na
vijana kwa mazungumzo kama haya—nimefilisika yakuongelea hata niongelee sex? Hata
mimi mwanzoni sikudhani ningefanya hivyo. Lakini nilipofikiri namna gani
ninaweza kutimiza kiapo nilichochukua kuchunga washirika wa familia ya Mungu na
hasa vijana, ilikuwa wazi mawazoni mwangu nilazima niwafikie hapo walipo. Nilijiuliza, ni
changamoto gani ambazo vijana wanakabiliana nazo katika kizazi chao? Na
nikatambua kuwa ngono kabla ya ndoa ni mojawapo wa mambo yanayowapatia changamoto vijana wetu
wanaponuia kuishi sawa sawa na imani yao. Ninaamini ngono haramu si pilipili iliyoko shambani,
isipokuwa muwasho ulioko miilini mwao. Hivyo, nawajibika kuwajali vya
kutosha kuzungumza nao kuhusu maswala yanayowakwamisha wanapojaribu kufuata
nyayo za Yesu maishani.
Ndipo nilipowaalika mezani wasichana na wavulana kwa mazungumzo ya uso kwa uso kuhusu ujana na imani. Na vijana sabini hivi waliitikia wito wangu wa kukutana nao mezani. Kikao chetu cha awali kilitawaliwa na mazungumzo ya jinsi jamii inavyoshabikia sex na mtazamo wetu kuhusu sex—mazungumzo yalituchangamsha kama pilipili kinywani. Nipatie muda wako mfupi nikusimulie jinsi mazungumzo yetu yalivyokwenda na kuishia kutufaa sote, mimi na wao. Karibu ujiunge nasi ninapokusimulia yaliyojiri.
Jamii na Ushabiki wa Sex
Tulipokusanyika mezani, nilianza
kuwakumbusha vijana jinsi sex au ngono ilivyotapakaa katika jamii kama hewa inavyofunika
uso wa dunia. Nikagusia namna macho yetu yanavyokutana na sex kwenye TV na
Video na simu na kompyuta. Iwe ni kwenye matangazo ya biashara au kwenye
vipindi vya fashion show, ujumbe unatumwa (message sent) ni: “sex ni raha,””
usijinyime,” “jimwage”. Iwe ni mtaani au kwenye ukumbi wa burudani sex
inatangazwa kwa tabasamu za kuvutia, macho ya kushawishi, mavazi ya kuita, au
vinginevyo. Huku nikisema hayo, nyuso za vijana ziliniambia, “endelea
tunakuelewa”
Basi nikaendelea kuwakumbusha jinsi
Sex inavyotuita masikioni mwetu mchana na usiku. Ukifungulia redio, ukisikiliza
nyimbo utakutana na sex ikiimbwa au kutajwa, moja kwa moja au chini kwa chini. Maudhui
na midungo mingi ya musiki wa kizazi
kipya unaamsha hisia za mahaba kwa wasikilizaji, huku vipindi vingine
vikiendeleza simulizi za utamu na uchungu wa kujamiana. Nikasema, hata midomoni
mwa majirani, jamaa na marafiki sex hutajwa kama hadithi ya kusimuliwa, utani
wa kuchekesha au matusi ya kutukanisha. Nilipoongeza kusema hayo, baadhi ya
vijana wakawa wanacheka kimya-kimya huku wengine wakinikazia macho.
Kama vile haitoshi, nikawaambia sex imejaa vichwani mwa watu kama maji yanavyojaa kwenye chupa ya Kilimanjaro. Wasichana hawawezi kusanyika pamoja wasiwazungumzie wavulana na mapenzi, na kadhalika na wavulana hawaachi kuzungumzia wasichana. Na hatari zaidi ni kwamba wasichana na wavulana wengi wanaamini ni sharti ucheze sex ili kuthibitisha uwezo wako wa kuwa mama au baba wa baadaye. (Hapo vijana wakaangaliana na kurudisha macho kwangu).
Kabla ya kumeza mate na kwenda kwenye mapumziko mafupi, sikusita kuwaonesha vijana mshangao wangu kwa ushabiki wa ngono katika jamii yetu leo. Kwani kwa wengi mapenzi yamekuwa si lugha ya kimwili ya upendo kwa watu walioshibana na kuaminina kwa maisha yote, bali imekuwa mchezo tu wa
kujifurahisha na na mtazamo unaoongoza maisha maisha. Na kwa lugha nyingine, leo sex imegeuka hewa; usipoivuta,
huna raha, huna maisha.
Sex Hailizi Mashabiki Wake?
Kabla ya kuwapatia vijana kipaza sauti changu na kuwaomba
watoe maoni yao juu ya gumzo hili la mapenzi, nilitamani kushiriki mashaka
yangu kuhusiana na ahadi za sex kwa
wapiga kura wake. Je, ni kweli zinaa huwapatia wapiga kura wake ua pasipo mwimba na
raha pasipo uchungu? Sikutaka kuwaonesha haraka vijana wangu machungu yote
yanayosindikizana na sex, au miiba inavyoshonana na waridi-sex.
Sikutaka kuwathibitishia haraka vijana kuwa ahadi za sex kwa mashabiki wake ni hewa tupu, na kwamba wapenzi wanaofurahia ua la mahaba ni kwa kitambo tu kabla ya hawaishia kuchomwa na miiba ya mimba zisizotarajiwa na magonjwa ya zinaa. Nilisita kutaja
miiba hiyo mapema nikijua mashabiki wengi wa sex wanaifahamu kiasi cha
kudhani wanaweza kufurahia uzuri wa ua pasipo kuikaribia miiba yake.
Ndipo nikawasimulia mfano wa kijana ambaye hakupatikana na matokeo yanayoogopeka kama ya ngono haramu kama mimba nje ya ndoa au magonjwa ya zinaa lakini hakupona. Kijana huyo alikuwa mkazi wa mjini—kijana anayekubalika na kila nguo anayovaa, mzuri wa sura, mdogo wa umri, na kipenzi cha wasichana. Akiamini maisha ni mapenzi na mapenzi ni maisha, kijana akawa ni wa kuruka-ruka kama kipepeo toka ua moja mpaka ua jingine, toka kitanda kimoja mpaka kingine. Lakini haikuchukua muda mrefu kabla marafiki zake aliowaacha kuanza kumwandama kwa matusi na lawama kwa sababu ya tabia yake ya onja-acha, onja-acha. Kijana akawa ni mtu mwenye ugomvi usiokwisha na mwenye msongo wa mawazo yasiyokoma. Kipato chake cha kifedha kilibaki pale pale huku gharama ya mahaba ikipanda juu na juu zaidi. Nayo ajira ya kijana ikaanza kuyumba-yumba. Kijana alitumia muda na nguvu na akili nyingi zaidi kwa anasa badala ya kazi iliyomweka mjini. Hata heshima yake katika jamii ikaanguka na jina lake likabaki likikanyagwa miguuni mwa wapitanjia na kutafunwa midomoni mwa wambeya. Mwishoni, kijana akasema “sex hailipi.” Kuanzia hapo kijana aliiona sex kama tapeli aliyemuahidia mengi na kuishia kumtimizia machache na kumkimbia. Japo jamii haikuemueleza uchungu wa sex ilipokuwa ikisifia uzuri wake, sasa kijana akawa amefunguka.
Lakini Wewe Kijana, Sex Unaitazamaje?
Basi ndipo nilipotaka kujua vijana wangu wamefunguka
kiasi gani, na wanafikiria nini juu ya mada inayopendwa na jamii yetu. Nilitamani
kufahamu mawazo yao yanafanana au kutofautiana vipi na yale ya jamii
inayowazunguka? Kwa kuanza nikawatupia vijana hamsini ( waliokuwa wamefika
mezani wakati huu) msemo huu: “Sex ipo tu
kwa ajili ya kutupatia raha.” Nikawaomba maoni yao. Kati yao 7 wakakubaliana
kuwa usemi huo una ukweli, 39 hawakuafiki, na 4 wakajizuia kutoa maoni yao.
Swali kama hilo hilo nilipolirudia kwa maneno mengine nikakutana na matokeo
yaliovuta zaidi masikio yangu ya udadisi. Nikawauliza mnakubalianaje na
sentensi hii: “sex ni dhambi”? Wanne
(4) kati yao wakajibu “ndiyo”, 22 wakasema “hapana”, huku 24 wakijizuia kujibu.
Japo hayo maswali yangu yaliuliza maoni ya wanameza kwa ujumla, jambo moja
lilikuwa wazi kwangu zaidi ya mengine: wengi wa vijana walionizunguka
hawaafikiani na maoni ya jamii inayotukuza sex. Vijana wangu wanaamini kwamba
sex haipo hapo ili tu kutufurahisha; lakini vile vile si kitu cha kukimbiwa na
wakristo kama dhambi.
Kwa kuwa sio vijana wote waliopigia
kura kujibu maswali yangu, nikatamani kuwachokoza zaidi hususani undani wa
mtazamo wao kuhusu ngono na namna wanavyokabiliana na vivutio vya biashara ya
mahaba.
Ndipo nikawauliza, “kwa nini sex inashabikiwa kiasi kikubwa na
jamii yetu?”
Majibu yalikuja yaliyofanana na kutofautiana kama walivyojibu maswali yangu ya hapo nyuma. Kundi moja la vijana walioona uzuri wa sex ndio kivutio cha kuifanya ipendeke kiasi kikubwa. Mapenzi ni matamu na vitamu vinapendwa. Na kwa kuwa Mapenzi matamu yana walaji wengi, ulaji huo umezalisha biashara inayotafuta kukidhi shauku ya walaji. Ndio maana hakuna sababu ya kushangaa kwa nini ukahaba kama kitega-uchumi hakikosi wateja au wawekezaji. Maongezi mezani yakahamia kwa watangazaji wa biashara wanaotumia fedha nyingi kumshawishi mtazamaji wa TV au msikilizaji wa redio kuwa endapo atanunua bidhaa zao kiu yake ya mapenzi itatimizwa. Sabuni itauzika, mafuta ya kupaka yatapata wateja, na magodoro yatafuatwa dukani kama mteja atona bidhaa husika itamsaidia avutie kimapenzi au atimize hamu ya mapenzi. Kwa maneno mengine, vijana waliniambia sex inapendwa kwa kuwa inapendeka.
Majibu yalikuja yaliyofanana na kutofautiana kama walivyojibu maswali yangu ya hapo nyuma. Kundi moja la vijana walioona uzuri wa sex ndio kivutio cha kuifanya ipendeke kiasi kikubwa. Mapenzi ni matamu na vitamu vinapendwa. Na kwa kuwa Mapenzi matamu yana walaji wengi, ulaji huo umezalisha biashara inayotafuta kukidhi shauku ya walaji. Ndio maana hakuna sababu ya kushangaa kwa nini ukahaba kama kitega-uchumi hakikosi wateja au wawekezaji. Maongezi mezani yakahamia kwa watangazaji wa biashara wanaotumia fedha nyingi kumshawishi mtazamaji wa TV au msikilizaji wa redio kuwa endapo atanunua bidhaa zao kiu yake ya mapenzi itatimizwa. Sabuni itauzika, mafuta ya kupaka yatapata wateja, na magodoro yatafuatwa dukani kama mteja atona bidhaa husika itamsaidia avutie kimapenzi au atimize hamu ya mapenzi. Kwa maneno mengine, vijana waliniambia sex inapendwa kwa kuwa inapendeka.
Lakini kundi lingine la vijana halikuona umaarufu wa Sex kama sababu pekee ya kufanywa ishabikiwe na wanajamii wengi. Wao waliona sababu ushabiki uliopindukia ipo kwa mashabiki wenyewe. Walilaumu ulegevu wa kimaadili miongoni mwa jamii yetu kama sababu inayowafanya watu wampigie magoti mungu zinaa. Wakaongeza kusema, shetani ameweza kupagaa watu na pepo la mahaba kwa sababu watu wenyewe hawajatulia katika msimamo wao wa imani. Na hapo nikaona wananiambia, “mchungaji sisi kama vijana tuna uchaguzi wa kufanya. Twaweza kuamua kukubali kupeperushwa na ushabiki wa ngono au kubakia imara katika maadili ya imani.” Niliwajulisha vijana wangu kwamba nimetiwa moyo na mtazamo huo, lakini nikaongeza kusema inawezekana kuna baadhi yenu bado hawajafikia kuitazama sex sawa sawa na ukristo wetu na tofauti na jamii yetu inayotuzunguka.
Mwisho: Lakini Sio Mwisho wa Mazungumzo
Kila mmoja wetu mezani alitamani
mazungumzo yetu yangeendelea. Lakini muda ukasimama mbele yetu kama ukuta na kipindi
chetu kikaishia hapo. Mpaka hapo mazungumzo yetu yalipoishia, nilifurahi kuona woga
ukitoweka mezani tulipoendelea kuzungumzia sex—swala la karibu kama miili yetu
na muhimu kama maisha yetu. Tulizidi kushawishika kuwa mada muhimu kama hizi zapaswa
kuzungumziwa kwenye majukwaa muhimu kama mezani pa mchungaji, na sio gizani au
vichochoroni mahali ambapo busara ya wale waliotangulia maishani haiwezi kuangazia.
Hivyo, kabla hatujaachana, tulitiana moyo kwa maneno ya Warumi 12:2 tukimwomba
Mungu atusaidie “kutofuatisha namna ya dunia hii, bali [tu]geuzwe kwa kufanywa
upya nia ze[tu], [tu]pate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya
kumpendeza, na ukamilifu.”
Na kulingana na ombi hilo tukahadiana
kukutana wakati mwingine tena. Wakati huo tutatafuta kujua
mapenzi ya Mungu yaliyo mema ni yapi kuhusiana na sex. Basi tukutane wakati mwingine tukutane hapa hapa kwa kujiunga nasi katika Meza ya Mchungaji na Vijana.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni