16/04/2013

Samson: Apoteza Maisha lakini Aokoa Roho (Waamuzi 16:28)

Samson: Apoteza Maisha lakini Aokoa Roho  (Waamuzi 16:28)

 

Mimi ni Samson.

Kabla sijakusimulia kisa cha maisha yangu niruhusu kwanza nijitambulishe. Mimi naitwa Samson. Habari zangu mmezisoma katika kitabu cha Waamuzi sura ya 13 mpaka 16. Baba na mama yangu waliniita Samson, (kwa lugha yangu ya mama, kiebrania, walitamka jina langu, shemesh, kwa kiswahili chake, jua) wakimaanisha “mtu mwenye nguvu.”  Jina langu lilikuwa la pekee. Hata kuzaliwa kwangu hakukuwa kwa kawaida. Ukimwondoa Yohana na Yesu mnaowakumbuka, hakuna aliyezaliwa namna yangu kama mimi. Malaika aliwaambia wazazi wangu: “mnaenda kupata mtoto—mtoto mwenye kazi maalumu maishani. Kusudi la maisha yake ni kukomboa Israel toka mikono ya Wafilisti”. Utume wangu ulikuwa wazi, njia yangu ya maisha ilikuwa imetandikwa wazi mbele yangu. Kisha malaika wa Bwana akaendelea kusema, “Jambo pekee mnalopaswa kujua mnapaswa kumlea kama mnadhiri wa Mungu,  jambo la pekee analopaswa kukumbuka, anapaswa kuishi kwa kuzingatia vigezo na masharti ya mtu aliyetengwa na Mungu kwa kazi maalumu.”  
Nani kama Samsoni?!
Nikaanza kukua. Miaka ilipokua ikiipita na misimu ikizunguka ndivyo na umri na nguvu zangu zilivyozidi kuongezeka. Na nikaja kuwa na nguvu kweli, kweli. Hakuna ambaye hakunifahamu. Kila mmoja alilijua jina la Samson. Kila mmoja alilitamka jina langu kwa heshima. Na wasingeweza kunidharau. Nilikuwa na nguvu. Hakuna mwanamume chini ya jua aliyewahi kuwa na nguvu kunizidi. Nini? Mnadhani ninazidisha maneno kunogesha radha ya hadithi? Hebu  niwapatie ushahidi na muamue wenyewe kama madai yangu ni ya kweli au uongo.

Nilipokwenda Timna

Mapema nilipokua ningali kijana mbichi nilijaribu kupiga mbizi katika bahari ya mahaba. Ikatokea nikavutwa na mwanamke mmoja wa ovyo. Mwanamke huyo hakutoka katika jamii ya watu wangu. Na haikuwa shida, mbona wengi walioa au kuolewa na wapagani. Enzi hizo ilikuwa “ruhsa” kujifanyia lolote roho yako itapenda. Hapakuwepo mfalme katika Israeli (Wa 17:6; 21:25), Yoshua aliyeingiza Israeli alikuwa amekufa siku nyingi na Sauli mfalme wa kwanza wa taifa letu alikua hajaja. Na mimi, roho yangu ilimpenda mwanamke mfilisti aliyeishi Timna. Hakuwa muumini. Macho yangu yalipogongana na yake, nilivutwa naye, au niseme mrembo aliniwasha tamaa. Nilijua ninamtaka. Nikawaambia wazazi wangu, “Mnipatie huyo, maana ananipendeza sana” (14:3,7). Kawaida, wazazi wangu hawakupendezwa na uamuzi wangu wa kumuoa asiyeamini, lakini nilikuwa mtoto kichwa-ngumu na mwishowe wazazi wangu wakakubaliana nami.

Ili kukamilisha maandalizi ya arusi ilibidi niende Timna. Safari ilikuwa ya hatari; miamba na vichaka vimetanda njiani. Njia inanyoka-inapinda, inainuka- inashuka kufuatisha vilima vya Kaanani. Kulikuwa na maficho ya kutosha kwa majangiri. Lakini hilo halikusumbua mawazo yangu, zaidi nilikuwa nikifikiria utakuwaje usiku wa kwanza wa arusi na honeymoon. Ghafla macho yangu yakakutana na kitu kibaya kuliko jambazi—nikaona wingu la dhahabu likirukia toka nyuma yangu kuja karibu na mabega yangu. Alikuwa simba. Akifoka na kujirusha hewani kunifikia. Ungekuwa wewe ungefanya nini? Duaa? Lilia mama yako? Unajua nilichofanya? Bila kusita, nilipoona simba ananirukia aniue, nikamuwahi na kuanza kumpangua na kumpasua. Ungeweza kusikia mifupa ikivunjika, nyama ikichanika, na punde, simba alikuwa pembeni mwa barabara....akiwa vipande viwili. Mimi mwenyewe nilibaki mdomo wazi nikishangaa kazi ya mikono yangu. Na ule mzoga ulipokoma kuhangaika na kuacha kutetemeka, sikukaa nifikiri kwa nini simba anivamie, ametumwa na Mungu kunizuia nisiendelee mbele na safari yangu? Nilipotazama mzoni nilijua mimi ni mwanamume mwenye nguvu kupita wote.

Mimi na Kahaba wa Gaza

Bado huna hakika kuwa mimi ni mwanamume mwenye nguvu aliyewahi kuishi? Unahitaji ushahidi zaidi? Nitakupatia hadithi nyingine. Siku moja niliamua kwenda Gaza, mji wa kifilisti pembezoni mwa bahari (Wa 16:1-3). Nilikuwa natafuta kisura wa kujifurahisha naye. Nikajibadili kimwonekano nisijulikane na kujichanganya na watu waliojaa mtaani. Nilipokuwa nimejipumzisha kwenye kona fulani, nilimwona mwanamke wa usiku. Nilipendezwa kumtazama, nikalipa fedha na kulala naye. Katikati ya usiku nilipomaliza, nikajiandaa kuondoka. Lakini nikaona watu wa Gaza walikwisha nishtukia na kunigundua.  Na waliamini wamenipata. Niko ndani ya mji wao. Gaza kama miji mingine ya kifilisti ulikuwa umezungushiwa kuta ndefu, hata huwezi kurusha jiwe juu yake, pana kuruhusu gari linalokokotwa na farasi lipite. Kuta zao za mawe zilikuwa imara vya kutosha kumzuilia adui nje. Lango la mji lilitengenezwa na mti mgumu, unene wake futi 6, likining’nizwa na mawabu za shaba, kwenye fremu ya mlango wa futi 10 mpaka 15. Kama hiyo haitoshi geti la mji wao liliongezewa boriti za shaba juu yake kulifanya imara zaidi siku walipohisi hatari. Lango lilikuwa zito kweli kweli. Hakuna ambaye angeweza kutoka mjini mlango unapofungwa. Na wafilisti walijua nimepatikana.
Nilipoziona nyuso zao na kusikia wanavyonong’onezana nilihisi wanasema, “Tumempata, hatimaye Samsoni ni wetu”. Nilipogeuka na kuona kango zito limefungwa namna ile mpango wao ulikuwa wazi kwangu. Walitaka kuninasa kama panya kwenye mtego. Sijui ungefanyaje ungekuwa katika hali hiyo. Kujaribu kujificha labda? Toboa ukuta? Hiyo haikuwa staili yangu. Huyo sio Samson. Sikutetemeka katika hofu. Nilitembea wima, kifua mbele katikati ya mji mpaka nikafika langoni mwa mji. Nikatazama huku na huko kuona kama kuna yoyote yupo jirani ashuhudie mimi ni nani. Nilitema mate mikononi, nikainama chini, nikakamata boriti lililokuwa likikazia mrango ufunge. Nashukuru bori hilo liliwekwa pale chini. Nikapata pa kushikia. Kisha nikaanza kuvuta.....zaidi na zaidi. Nilipovuta nikaanza kusikia joto joto la Roho wa Mungu limeanza kusambaa mwili mzima. Nilipozidi kuvuta zaidi na zaidi joto la kiungu likazidi kukolea. Nikaanza kuona nyufa, kusikia mbao zikilalamika (kakak..kaka..) na mwishoni lango lilinyofoka na nikalimwaga chini. Mtu wa kawaida baada ya shughuli iliyofanyika angeuacha mlango hapo na kuondoka zake. Lakini niliona sitakuwa nimewapatia wafilisti wasiotahiliwa somo la kutosha. Kwa hiyo nikalinyanyua geti mabegani mwangu na mpaka umbali wa maili 28 juu ya kilele cha kilima na kuliacha hapo. Wangehitaji timu ya majeshi kuurudisha mlango getini. Isingefaa nikimbie mji wao salama. Nilitaka wasumbuke. Mimi ni mwanamume mwenye nguvu aliyewahi kuishi. Hakuna swali. Hakuna upinzani.

Niliporudi tena Timna

Aha! Mnakumbuka niliwaambia kuhusu safari yangu ya Timna kwa ajili ya maandalizi ya arusi yangu? Kweli taratibu za uchumba zilikwisha, uchumba wetu ulikubarika na wazazi wa pande mbili. Lakini mambo yalikuwa bado hayako sawa. Arusi inakaribia. Ikanibidi nisafiri tena. Nyumbani mpaka Timna si karibu. Nilipokuwa safarini, tumbo langu likinikata kwa njaa. Hatimaye, nikafika sehemu ya barabara nilipomrarua mfalme wa pori. Nikaamua kutazama uharibifu nilioufanya, nikachungulia mzoga. Haa kuna asali! Nilichokiona mimi ni chakula kutuliza njaa yangu. Bila kujali kama kuna nyuki au kwamba Mungu alinikataza nisiguse maiti, nikatuma mkono ndani ya mzoga na kujizolea asali. Nikasubiri nione kama Mungu atatuma malaika mwenye upanga anikate shingo kwa kuwa nimevunja kiapo kwa kugusa mzoga, sikuona. Nisubiri nione ardhi ikifunguka kwa tetemeko na kunimeza, kimya. Labda wazazi wangu hawakuwa sahii waliponiambia Mungu hataki mimi nishike kitu najisi kama: mbona sijadhurika? Nikawagawia wazazi wangu bila kuwaambia nimeitoa wapi, nami nikaanza kuila asali huku ikitapakaa mdomoni na kinitiririka mikononi. Nakwambia, hakuna siku asali ilikuwa tamu kama siku ile!
Niliendelea mbele mpaka nikafika Timna, maandalizi ya arusi yakaisha na arusi ya kufana ikafanyika. Arusini wafilisti walikuwa wananishangaa-shangaa wakinichungulia bila kuamini macho yao. Wakijiuliza, hivi Samson ni mwanamume wa kawaida au wa kimiujiza. Unajua nilivyokua nikijisikia. Nikataka kuwaonesha kuwa mimi ni mwanamume.Nikaagiza bia ya Kifilisti. Kwani bia moja inashida gani? Mwanaume, nikainywa na chupa kuiweka chini. Na hapo nikajua nimevunja kiapo cha pili kama mnadhiri wa Mungu. Nikasubiri nione hasira ya Mungu ikiniwakia na radi toka mbinguni ikiniangukia. Dhambi yangu ina matokeo gani? Sikuwahi kufikiria swali hili kwa mda mrefu namna hii. Sikua naogopa, lakini nilitamani kujua Mungu atanifanya nini? Na unajua alinifanyaje? Hakuna! Hakuna lolote! Nikaanza kufikiri hii habari ya dhambi inaua ni maongezi tu. Mbona nimevunja viapo vyangu viwili na hakuna kilichonitokea. 
Maisha yakaendelea. Lakini si na mwanamke niliyemuoa. Ndoa ile haikuendelea. Hiyo nayo ni hadithi ndefu. Lakini niliwatia adabu wafilisti kwa kunivunjia ndoa yangu.  Niliwaua wafilisti wengi tu. Nani mwanamume kama mimi?

 

Nilipompata Delila

Na maisha yakaendele, nikiwa sina mwanamke wa kudumu. Ndipo siku moja nikadhani nimepata jibu la maombi yangu. Nilikutana na mwanamke wa moyo ndoto zangu. Alikuwa na nywele ndefu, ngozi nyeupe, na macho yake yangekumaliza. Kila nguo inamkaa! Huyu ndiye mwanamke! Jina lake aliitwa.....Delila. Alikua ameumbika; alikuwa na kila kitu cha kumfurahisha mwanamume. Huwezi kuhitaji mwingine. Isipokuwa kwa kitu kimoja.....alikuwa mzuri lakini....alikuwa akitaka kitu chake lazima akipate. Anaweza kukiomba kwa kurudia rudia mpaka akipate. Na sasa alitaka kujua siri za nguvu zangu. Alikuwa anaweza kusema, “Samson kama unanipenda niambie asili ya nguvu zako.” Alisema huku akilegeza macho yake, na akizilaza nywele zake mara huku mara huku. Na akanimaliza.
Samsoni akiwa amesalitiwa
Mara kadhaa alinibembeleza nimwambie, na mara zote nilimwambia kidogo tu na sikumwambia ukweli wote. Lakini Delilah hakukata tamaa. Hata hivyo, unajua, alikuwa ameahidiwa na maafisa wa usalama wa taifa furushi la hela kama ataipata siri. Pesa nyingi kama jumla ya mishahara ya mfanyakazi kwa maisha yake yote. Akijua hilo ndivyo alivyozidi kunisihi akisema, “Wasemaje nakupenda; na moyo wako hauko pamoja nami? “ (16:13). Mwishowe nikamwambia Delila nadhiri moja ambayo sikuwa nimeivunja. Nilimwambia kuwa sijawahi kukata nywele zangu. Nilivyomwangalia machoni, nilijua ninaweza kumuamini. Usiku ule, niliishia usingizini na kichwa changu mapajani mwake. Nilimtumainia maisha yangu, lakini alinisaliti. Nilipokua nimelala, kumbe akamleta mtu kunikata nywele zangu. Mimi sina habari. Kisha akaniita, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!” (16:20). Nikaamka mwanamume kama nilivyozoea kuamka. Nikasema mbona hawa Wafilisti hawaelewi somo, hebu niwaoneshe mara nyingine tena kuwa mimi ni mwanamume mwenye nguvu aliyewahi kuwepo. Nikajaribu kujinyoosha, lakini sipati nguvu. Uchovu niliolala nao upo pale pale. Wafilisti wakaja, wakanikamata, na kuninyang’anya nguvu zangu na uanaume wangu.

 

Majuto Kitanzini

Samsoni Kitanzini
Ndugu zangu hebu niwaambie: mimi sikuwa hivi. Wameninyoa nywele zangu zote, siwezi kutamba tena. Wamening’oa macho yangu, siwezi kuona tena. Wamenifunga, siko huru tena .

 

Nimeingiaje kwenye shimo hili?

Laiti kama ningewasikiliza wazazi wangu nisingekuwa hapa. Nakumbuka wazazi wangu walivyokua wakiniambia na nilivyokua nikiwajibu:
  •  “Samsoni, usisahau, ukashika chochote kilicho kichafu. Samsoni usikaribie huko. Hutakiwi kugusa mizoga.”  “Najua mama, najua." Niliwajibu, "Umekwisha niambia mara mia kidogo.”
  •  “Samson, usiende huko. Huko ndiko vinyaji vyote vinapatikana. Vinywaji vyote vilivyochachushwa. Kileo chochote kisipite mdomoni mwako. Wewe ni Mndadhiri. Usikariebie huko.”
  • Baba yangu aliniambia, “Samson, kumbuka, usikate nywele zako.” “Ninajua, baba. Hiyo ni ishara kwamba mimi ni mnadhiri na kila mmoja anitambue kuwa mimi si wa kawaida.”
Ninakiri tatizo langu halikuwa kwamba sikuambiwa. Laiti kama ningewasikiliza wazazi wangu nisingekuwa hapa.

Nimeingiaje kwenye shimo hili?

Sasa ninajua tamaa ya mwili inaweza kuwa imetulia, lakini haifi kamwe. Makaa ya moto yanaweza kuwa yamebakia chini ya majivu ukadhani yamezima, lakini yakipulizwa na upepo, yanaweza kuwasha msitu mzima. Na matokeo yake mtu anaweza kuunguzwa. Na ndiyo yaliyonipata.
Nilipokua na kahaba, nilijifikiria, “Nikijiridhisha naye mara hii ya mwisho, itakua basi.” Lakini unajua dhambi moja inaita nyingine. Nilikua ninapanda pengu ambayo ilikua izae matunda yake baadaye. Nilianza kumkubalie Delila kunishika-shika. Sikuyakimbia majaribu; nilibakia ndani ya mipaka yake. Unaweza kudhani nimezidisha, lakini nadhani ingekua bora kama Wafilisti wangenifanya kipofu nikiwa bado mdogo. Ingenisaidia nisijiingize kwenye mapenzi haramu. Delila inamaanisha “mtu aliye dhaifu” au “mtu aliye na shauku.” Nilikua mwanamume mwenye nguvu kupita wote, na sikudhohofishwa na maaskari au majeshi, lakini na mwanamke. Mimi, Samsoni mwenye nguvu sikuweza kujiponya toka mikononi mwa Delila, “mtu aliye dhaifu.”

Siulizi tena nimeingiaje kwenye shimo hili.

Samsoni awaua Wafilisti
Ninajua ni makosa yangu. Sio kosa la Delila, japo kwa muda mrefu nilimlaumu sana. Sio kosa la Delila, wala vaa yake, wala macho yake au mabembelezi yake. Kosa ni langu: ningewasikiliza wazazi wangu nisingekua hapa. Kweli, hapa nilipo, sina nywele na sina macho. Lakini namshukuru Mungu. Siwezi kunywa sumu. Baada ya kutolewa macho, sasa naweza kuona. Na sasa kwa mara ya kwanza nimeweza kutubu na kuabudu na kuhutubu. Japo wafilisti bado wamenifunga mwili wangu kwa minyororo, lakini Mungu ashukuriwe, roho yangu iko huru. Wafilisti wamenifunga kama mbwa kibandani na kumtukana Mungu wangu. Lakini, ninaomba Mungu adhihirishe nguvu zake kupitia udhaifu wangu, aoneshe wema wake kupitia ubaya wangu. Ninamshukuru niko hapa ili nikuambie uhitaji kua hapa, na kama upo hapa tayari usife moyo Mungu hutoa nafasi ya pili tutazame makosa yetu ili tuyajutia na kuyaacha.
(Hubiri lililotolewa na Pr Enos Mwakalindile 13 April, 2013 Donge SDA church, Tanga) 

Maoni 1 :

Pacoster Tech alisema ...

asante Pr. Nimebarikiwa sana na somo lako.