Samson: Apoteza Maisha lakini Aokoa Roho (Waamuzi 16:28)
Mimi ni Samson.
Kabla sijakusimulia kisa cha maisha yangu niruhusu kwanza nijitambulishe.
Mimi naitwa Samson. Habari zangu mmezisoma katika kitabu cha Waamuzi sura ya 13
mpaka 16. Baba na mama yangu waliniita Samson, (kwa lugha yangu ya mama, kiebrania,
walitamka jina langu, shemesh, kwa kiswahili
chake, jua)
wakimaanisha “mtu mwenye nguvu.” Jina
langu lilikuwa la pekee. Hata kuzaliwa kwangu hakukuwa kwa kawaida. Ukimwondoa
Yohana na Yesu mnaowakumbuka, hakuna aliyezaliwa namna yangu kama mimi. Malaika
aliwaambia wazazi wangu: “mnaenda kupata mtoto—mtoto mwenye kazi maalumu
maishani. Kusudi la maisha yake ni kukomboa Israel toka mikono ya Wafilisti”.
Utume wangu ulikuwa wazi, njia yangu ya maisha ilikuwa imetandikwa wazi mbele
yangu. Kisha malaika wa Bwana akaendelea kusema, “Jambo pekee mnalopaswa kujua
mnapaswa kumlea kama mnadhiri wa Mungu,
jambo la pekee analopaswa kukumbuka, anapaswa kuishi kwa kuzingatia
vigezo na masharti ya mtu aliyetengwa na Mungu kwa kazi maalumu.”
![]() |
Nani kama Samsoni?! |
Nilipokwenda Timna
Mapema nilipokua ningali kijana mbichi nilijaribu kupiga
mbizi katika bahari ya mahaba. Ikatokea nikavutwa na mwanamke mmoja wa ovyo. Mwanamke
huyo hakutoka katika jamii ya watu wangu. Na haikuwa shida, mbona wengi walioa
au kuolewa na wapagani. Enzi hizo ilikuwa “ruhsa” kujifanyia lolote roho yako
itapenda. Hapakuwepo mfalme katika Israeli (Wa 17:6; 21:25), Yoshua aliyeingiza
Israeli alikuwa amekufa siku nyingi na Sauli mfalme wa kwanza wa taifa letu
alikua hajaja. Na mimi, roho yangu ilimpenda mwanamke mfilisti aliyeishi Timna.
Hakuwa muumini. Macho yangu yalipogongana na yake, nilivutwa naye, au niseme mrembo
aliniwasha tamaa. Nilijua ninamtaka. Nikawaambia wazazi wangu, “Mnipatie huyo,
maana ananipendeza sana” (14:3,7). Kawaida, wazazi wangu hawakupendezwa na
uamuzi wangu wa kumuoa asiyeamini, lakini nilikuwa mtoto kichwa-ngumu na
mwishowe wazazi wangu wakakubaliana nami.
Ili kukamilisha maandalizi ya arusi ilibidi niende Timna.
Safari ilikuwa ya hatari; miamba na vichaka vimetanda njiani. Njia inanyoka-inapinda,
inainuka- inashuka kufuatisha vilima vya Kaanani. Kulikuwa na maficho ya
kutosha kwa majangiri. Lakini hilo halikusumbua mawazo yangu, zaidi nilikuwa
nikifikiria utakuwaje usiku wa kwanza wa arusi na honeymoon. Ghafla macho yangu
yakakutana na kitu kibaya kuliko jambazi—nikaona wingu la dhahabu likirukia
toka nyuma yangu kuja karibu na mabega yangu. Alikuwa simba. Akifoka na
kujirusha hewani kunifikia. Ungekuwa wewe ungefanya nini? Duaa? Lilia mama
yako? Unajua nilichofanya? Bila kusita, nilipoona simba ananirukia aniue,
nikamuwahi na kuanza kumpangua na kumpasua. Ungeweza kusikia mifupa ikivunjika,
nyama ikichanika, na punde, simba alikuwa pembeni mwa barabara....akiwa vipande
viwili. Mimi mwenyewe nilibaki mdomo wazi nikishangaa kazi ya mikono yangu. Na
ule mzoga ulipokoma kuhangaika na kuacha kutetemeka, sikukaa nifikiri kwa nini
simba anivamie, ametumwa na Mungu kunizuia nisiendelee mbele na safari yangu?
Nilipotazama mzoni nilijua mimi ni mwanamume mwenye nguvu kupita wote.
Mimi na Kahaba wa Gaza
Bado huna hakika kuwa mimi ni mwanamume mwenye nguvu
aliyewahi kuishi? Unahitaji ushahidi zaidi? Nitakupatia hadithi nyingine. Siku
moja niliamua kwenda Gaza, mji wa kifilisti pembezoni mwa bahari (Wa 16:1-3).
Nilikuwa natafuta kisura wa kujifurahisha naye. Nikajibadili kimwonekano
nisijulikane na kujichanganya na watu waliojaa mtaani. Nilipokuwa
nimejipumzisha kwenye kona fulani, nilimwona mwanamke wa usiku. Nilipendezwa
kumtazama, nikalipa fedha na kulala naye. Katikati ya usiku nilipomaliza,
nikajiandaa kuondoka. Lakini nikaona watu wa Gaza walikwisha nishtukia na
kunigundua. Na waliamini wamenipata.
Niko ndani ya mji wao. Gaza kama miji mingine ya kifilisti ulikuwa
umezungushiwa kuta ndefu, hata huwezi kurusha jiwe juu yake, pana kuruhusu gari
linalokokotwa na farasi lipite. Kuta zao za mawe zilikuwa imara vya kutosha
kumzuilia adui nje. Lango la mji lilitengenezwa na mti mgumu, unene wake futi
6, likining’nizwa na mawabu za shaba, kwenye fremu ya mlango wa futi 10 mpaka 15.
Kama hiyo haitoshi geti la mji wao liliongezewa boriti za shaba juu yake
kulifanya imara zaidi siku walipohisi hatari. Lango lilikuwa zito kweli kweli.
Hakuna ambaye angeweza kutoka mjini mlango unapofungwa. Na wafilisti walijua
nimepatikana.
Nilipoziona nyuso zao na kusikia wanavyonong’onezana nilihisi
wanasema, “Tumempata, hatimaye Samsoni ni wetu”. Nilipogeuka na kuona kango
zito limefungwa namna ile mpango wao ulikuwa wazi kwangu. Walitaka kuninasa
kama panya kwenye mtego. Sijui ungefanyaje ungekuwa katika hali hiyo. Kujaribu
kujificha labda? Toboa ukuta? Hiyo haikuwa staili yangu. Huyo sio Samson.
Sikutetemeka katika hofu. Nilitembea wima, kifua mbele katikati ya mji mpaka
nikafika langoni mwa mji. Nikatazama huku na huko kuona kama kuna yoyote yupo
jirani ashuhudie mimi ni nani. Nilitema mate mikononi, nikainama chini,
nikakamata boriti lililokuwa likikazia mrango ufunge. Nashukuru bori hilo
liliwekwa pale chini. Nikapata pa kushikia. Kisha nikaanza kuvuta.....zaidi na
zaidi. Nilipovuta nikaanza kusikia joto joto la Roho wa Mungu limeanza kusambaa
mwili mzima. Nilipozidi kuvuta zaidi na zaidi joto la kiungu likazidi kukolea.
Nikaanza kuona nyufa, kusikia mbao zikilalamika (kakak..kaka..) na mwishoni
lango lilinyofoka na nikalimwaga chini. Mtu wa kawaida baada ya shughuli
iliyofanyika angeuacha mlango hapo na kuondoka zake. Lakini niliona sitakuwa
nimewapatia wafilisti wasiotahiliwa somo la kutosha. Kwa hiyo nikalinyanyua
geti mabegani mwangu na mpaka umbali wa maili 28 juu ya kilele cha kilima na kuliacha
hapo. Wangehitaji timu ya majeshi kuurudisha mlango getini. Isingefaa nikimbie
mji wao salama. Nilitaka wasumbuke. Mimi ni mwanamume mwenye nguvu aliyewahi
kuishi. Hakuna swali. Hakuna upinzani.
Niliporudi tena Timna
Aha! Mnakumbuka niliwaambia kuhusu safari yangu ya Timna kwa
ajili ya maandalizi ya arusi yangu? Kweli taratibu za uchumba zilikwisha,
uchumba wetu ulikubarika na wazazi wa pande mbili. Lakini mambo yalikuwa bado
hayako sawa. Arusi inakaribia. Ikanibidi nisafiri tena. Nyumbani mpaka Timna si
karibu. Nilipokuwa safarini, tumbo langu likinikata kwa njaa. Hatimaye,
nikafika sehemu ya barabara nilipomrarua mfalme wa pori. Nikaamua kutazama
uharibifu nilioufanya, nikachungulia mzoga. Haa kuna asali! Nilichokiona mimi
ni chakula kutuliza njaa yangu. Bila kujali kama kuna nyuki au kwamba Mungu
alinikataza nisiguse maiti, nikatuma mkono ndani ya mzoga na kujizolea asali.
Nikasubiri nione kama Mungu atatuma malaika mwenye upanga anikate shingo kwa
kuwa nimevunja kiapo kwa kugusa mzoga, sikuona. Nisubiri nione ardhi ikifunguka
kwa tetemeko na kunimeza, kimya. Labda wazazi wangu hawakuwa sahii
waliponiambia Mungu hataki mimi nishike kitu najisi kama: mbona sijadhurika? Nikawagawia
wazazi wangu bila kuwaambia nimeitoa wapi, nami nikaanza kuila asali huku
ikitapakaa mdomoni na kinitiririka mikononi. Nakwambia, hakuna siku asali
ilikuwa tamu kama siku ile!
Niliendelea mbele mpaka nikafika Timna, maandalizi ya arusi
yakaisha na arusi ya kufana ikafanyika. Arusini wafilisti walikuwa
wananishangaa-shangaa wakinichungulia bila kuamini macho yao. Wakijiuliza, hivi
Samson ni mwanamume wa kawaida au wa kimiujiza. Unajua nilivyokua nikijisikia.
Nikataka kuwaonesha kuwa mimi ni mwanamume.Nikaagiza bia ya Kifilisti. Kwani
bia moja inashida gani? Mwanaume, nikainywa na chupa kuiweka chini. Na hapo
nikajua nimevunja kiapo cha pili kama mnadhiri wa Mungu. Nikasubiri nione
hasira ya Mungu ikiniwakia na radi toka mbinguni ikiniangukia. Dhambi yangu ina
matokeo gani? Sikuwahi kufikiria swali hili kwa mda mrefu namna hii. Sikua
naogopa, lakini nilitamani kujua Mungu atanifanya nini? Na unajua alinifanyaje?
Hakuna! Hakuna lolote! Nikaanza kufikiri hii habari ya dhambi inaua ni maongezi
tu. Mbona nimevunja viapo vyangu viwili na hakuna kilichonitokea.
Maisha yakaendelea. Lakini si na mwanamke niliyemuoa. Ndoa
ile haikuendelea. Hiyo nayo ni hadithi ndefu. Lakini niliwatia adabu wafilisti
kwa kunivunjia ndoa yangu. Niliwaua
wafilisti wengi tu. Nani mwanamume kama mimi?
Nilipompata Delila
Na maisha yakaendele, nikiwa sina mwanamke wa kudumu. Ndipo
siku moja nikadhani nimepata jibu la maombi yangu. Nilikutana na mwanamke wa
moyo ndoto zangu. Alikuwa na nywele ndefu, ngozi nyeupe, na macho yake
yangekumaliza. Kila nguo inamkaa! Huyu ndiye mwanamke! Jina lake
aliitwa.....Delila. Alikua ameumbika; alikuwa na kila kitu cha kumfurahisha
mwanamume. Huwezi kuhitaji mwingine. Isipokuwa kwa kitu kimoja.....alikuwa
mzuri lakini....alikuwa akitaka kitu chake lazima akipate. Anaweza kukiomba kwa
kurudia rudia mpaka akipate. Na sasa alitaka kujua siri za nguvu zangu. Alikuwa
anaweza kusema, “Samson kama unanipenda niambie asili ya nguvu zako.” Alisema
huku akilegeza macho yake, na akizilaza nywele zake mara huku mara huku. Na
akanimaliza.
![]() |
Samsoni akiwa amesalitiwa |
Mara kadhaa alinibembeleza nimwambie, na mara zote nilimwambia
kidogo tu na sikumwambia ukweli wote. Lakini Delilah hakukata tamaa. Hata
hivyo, unajua, alikuwa ameahidiwa na maafisa wa usalama wa taifa furushi la
hela kama ataipata siri. Pesa nyingi kama jumla ya mishahara ya mfanyakazi kwa
maisha yake yote. Akijua hilo ndivyo alivyozidi kunisihi akisema, “Wasemaje
nakupenda; na moyo wako hauko pamoja nami? “ (16:13). Mwishowe nikamwambia
Delila nadhiri moja ambayo sikuwa nimeivunja. Nilimwambia kuwa sijawahi kukata
nywele zangu. Nilivyomwangalia machoni, nilijua ninaweza kumuamini. Usiku ule,
niliishia usingizini na kichwa changu mapajani mwake. Nilimtumainia maisha
yangu, lakini alinisaliti. Nilipokua nimelala, kumbe akamleta mtu kunikata
nywele zangu. Mimi sina habari. Kisha akaniita, “Samsoni, Wafilisti wanakujia!”
(16:20). Nikaamka mwanamume kama nilivyozoea kuamka. Nikasema mbona hawa
Wafilisti hawaelewi somo, hebu niwaoneshe mara nyingine tena kuwa mimi ni
mwanamume mwenye nguvu aliyewahi kuwepo. Nikajaribu kujinyoosha, lakini sipati
nguvu. Uchovu niliolala nao upo pale pale. Wafilisti wakaja, wakanikamata, na
kuninyang’anya nguvu zangu na uanaume wangu.
Majuto Kitanzini
![]() |
Samsoni Kitanzini |
Ndugu zangu hebu
niwaambie: mimi sikuwa hivi. Wameninyoa nywele zangu zote, siwezi kutamba tena.
Wamening’oa macho yangu, siwezi kuona tena. Wamenifunga, siko huru tena .
Nimeingiaje kwenye shimo hili?
Laiti kama ningewasikiliza wazazi wangu nisingekuwa hapa. Nakumbuka wazazi wangu walivyokua
wakiniambia na nilivyokua nikiwajibu:
- “Samsoni, usisahau, ukashika chochote kilicho kichafu. Samsoni usikaribie huko. Hutakiwi kugusa mizoga.” “Najua mama, najua." Niliwajibu, "Umekwisha niambia mara mia kidogo.”
- “Samson, usiende huko. Huko ndiko vinyaji vyote vinapatikana. Vinywaji vyote vilivyochachushwa. Kileo chochote kisipite mdomoni mwako. Wewe ni Mndadhiri. Usikariebie huko.”
- Baba yangu aliniambia, “Samson, kumbuka, usikate nywele zako.” “Ninajua, baba. Hiyo ni ishara kwamba mimi ni mnadhiri na kila mmoja anitambue kuwa mimi si wa kawaida.”
Ninakiri tatizo langu halikuwa
kwamba sikuambiwa. Laiti kama ningewasikiliza wazazi wangu nisingekuwa hapa.
Nimeingiaje kwenye shimo hili?
Sasa ninajua tamaa ya mwili inaweza kuwa imetulia, lakini haifi kamwe.
Makaa ya moto yanaweza kuwa yamebakia chini ya majivu ukadhani yamezima, lakini
yakipulizwa na upepo, yanaweza kuwasha msitu mzima. Na matokeo yake mtu anaweza
kuunguzwa. Na ndiyo yaliyonipata.
Nilipokua na kahaba, nilijifikiria, “Nikijiridhisha naye mara
hii ya mwisho, itakua basi.” Lakini unajua dhambi moja inaita nyingine. Nilikua
ninapanda pengu ambayo ilikua izae matunda yake baadaye. Nilianza kumkubalie Delila kunishika-shika. Sikuyakimbia
majaribu; nilibakia ndani ya mipaka yake. Unaweza kudhani nimezidisha, lakini
nadhani ingekua bora kama Wafilisti wangenifanya kipofu nikiwa bado mdogo.
Ingenisaidia nisijiingize kwenye mapenzi haramu. Delila inamaanisha “mtu aliye dhaifu” au “mtu aliye na
shauku.” Nilikua mwanamume mwenye nguvu kupita wote, na sikudhohofishwa na
maaskari au majeshi, lakini na mwanamke. Mimi, Samsoni mwenye nguvu sikuweza
kujiponya toka mikononi mwa Delila, “mtu aliye dhaifu.”
Siulizi tena nimeingiaje kwenye shimo hili.
![]() |
Samsoni awaua Wafilisti |
Ninajua ni makosa yangu. Sio kosa la Delila, japo kwa muda
mrefu nilimlaumu sana. Sio kosa la Delila, wala vaa yake, wala macho yake au
mabembelezi yake. Kosa ni langu: ningewasikiliza wazazi wangu nisingekua hapa. Kweli, hapa nilipo, sina nywele na sina macho. Lakini
namshukuru Mungu. Siwezi kunywa sumu. Baada ya kutolewa macho, sasa naweza
kuona. Na sasa kwa mara ya kwanza nimeweza kutubu na kuabudu na kuhutubu. Japo
wafilisti bado wamenifunga mwili wangu kwa minyororo, lakini Mungu ashukuriwe,
roho yangu iko huru. Wafilisti wamenifunga kama mbwa kibandani na kumtukana
Mungu wangu. Lakini, ninaomba Mungu adhihirishe nguvu zake kupitia udhaifu
wangu, aoneshe wema wake kupitia ubaya wangu. Ninamshukuru niko hapa ili
nikuambie uhitaji kua hapa, na kama upo hapa tayari usife moyo Mungu hutoa
nafasi ya pili tutazame makosa yetu ili tuyajutia na kuyaacha.
(Hubiri lililotolewa na Pr Enos Mwakalindile 13 April, 2013 Donge SDA church, Tanga)