Kabla ya Yote
Kati
ya watu wote walioingia na kutoka katika jukwaa la historia, nani aliyegawa
walimwengu kama mwanamume huyu? Alipotua tu juu ya uso wa sayari dunia, ripoti zinaonesha namna watu walitofautiana
namna kumpokea. Mwandishi mmoja anasema wageni walisafiri umbali mrefu ili kumsujudia mtoto huyu wa kiume, huku
wenyeji wakifanya mikutano mirefu ili kumuua. Mwingine anaandika kuwa alipokuwa angali mvulana mdogo,
walimu wa dini waliinamisha masikio yao kumsikiliza, huku wazazi wake wakimnyoshe vidole kumgombeza. Na tena mwingine akaongeza kuwa alipotoa hotuba yake ya kwanza katika hadhara ya watu waliomfahamu tangu utoto wake, wasikilizaji walimsikia kwa furaha lakini muda mfupi baadaye waliziba masikio yao na kutaka kumfungia kufuli mdomo wake. Lakini ripoti inaendelea kuonesha mwanamume huyu aliendelea kuhutubia mikusanyiko midogo na mikubwa. Siku moja katika hotuba yake mwanamume alidai kuwa Yeye ni mkate
ulioshuka toka mbinguni na wasikilizaji wake wanapaswa kumpokea nafsini kama
chanzo pekee cha uhai. Wachache waliweza kuyakubali madai hayo, lakini wafuasi wake wengi hawakuweza kumwelewa na walimwacha (Yoh 6:66). Viongozi wa dini na jamii waliposikia madai ya mwanaume huyu wakajaribu kutumia nyadhifa na nyenzo walizokuwa nazo kumdhibit mhubiri huyu asije akaligawa zaidi taifa. Viongozi wakatuma
vyombo vya usalama kumkamata, laikini askari waliotumwa wakarudi na pingu tupu
wakisema hatujawahi kusikia mwanamume anayenena kama mwanamume huyu (7:32). Katika
historia iliyoandikwa sijui mwanamume mwingine aliyewahi kuamsha hisia mchanganyiko kiasi hiki kama mwanamume huyu? Mtu huyo huyo akubaliwe na akataliwe, aheshimiwe na adharauliwe, apendwe
na achukiwe?
Mwanamume huyo si mwingine ila Yesu wa Nazareti. Natamani
kujua undani wa Yesu ili kubaini kwa nini watu watofautiane kumpokea kwa hisia zilizopishana kiasi hiki. Nitajaribu kurudi kwenye kurasa za historia na kufuatana naye anapopita katika barabara za vumbi za Palestina. Nitafuatana naye ili nisikie anasema nini na nimtazame anafanya nini huku nikifuatilia miitikio ya waliomshuhudia. Na ninaanza kukutana na Yesu kwenye injili ya Yohana sura ya tisa. Katika sura hii Yesu anafanya mambo ambayo hayajawahi kuonekana na anasema mambo ambayo hakuna mtu aliyewahi yasema.Mwanamume huyu nin nani?
Tukio A: “Nani
katenda dhambi?”
Yesu
anapita, anamwona kipofu. Wapo vipofu wengi hapa mjini Yerusalemu. Wengi wao ni upofu
wanaupata ukubwani kwa sababu za uchafu, maji yenyewe hayawekwi dawa. Hapa kuna kipofu aliyezaliwa hivyo. Yesu
anamwona kwa macho ya huruma. Lakini wanafunzi wanamwona kipofu huyu kwa macho ya udadisi. Wanafunzi
wakimtazama kipofu huyu wakaona huo ndio wakati mwafaka wa kukata rufaa kwa
Yesu kwa malumbano yaliyokuwa yakiendelea miongoni mwa wayahudi kuhusiana na uhusiano
wa dhambi na ugonjwa. Wapo walioamini mtu anaweza kuumwa kwa sababu ametenda
dhambi (wayahudi kwa ujumla wao waliamini afya ni baraka toka kwa Mungu na
ugonjwa ni laana). Lakini kulikuwa na nadharia nyingine. Walimu wengine wa
kiyahudi walifundisha hata kama mtu hajatenda dhambi maishani kabla ya kuumwa
inawezekana alitenda kabla hajazaliwa (japo ilikuwa ngumu kuthibitisha hilo).
Wapo wayahudi wengine walioamni mtu anaweza kuumwa kwa sababu wazazi wake
walitenda dhambi (wakielewa yale maneno ya Torati kwamba Mungu huwapatiliza
adhabu kwa maovu ya baba zao hata kizazi cha tatu na cha nne cha
wamchukiao). Sasa kichwani mwa wanafunzi
, swali halikuwa, je dhambi inaleta magonjwa, isipokuwa je, mdhambi yupi kaleta
upofu huu? Sikiliza swali lao kwa maneno yao, “Rabi ni yupi aliyetenda dhambi,
mtu huyu au wazazi wake, hata azaliwe kipofu”?(fungu, 2).
Yesu
anajibuje swali la wanafunzi? Kwanza, Yesu anakanusha nadharia zote
zilizotolewa kwamba mgojwa mwenyewe au wazazi wake walitenda dhambi ndio maana
akazaliwa kipofu. Magonjwa mengine hayasababishwi na dhambi tuliyotenda bali ni
maumbili dhaifu tuliyorithi. Kuna wagonjwa wa ukimwi waliozaliwa nao au
kuambukizwa na wenzi wao wa ndoa. Kuna magonjwa ya kurithi au kuletewa.
Usimtazame kipofu wa kuzaliwa au ukoo wake kama wadhambi. Hilo Yesu aliliweka
wazi kabisa.
Lakini
utata unajitokeza katika maelezo ya Yesu yanayofuata ufafanuzi huo. Ni kama
Yesu anasema, amekuwa kipofu ili Mungu ajidhihirishe! Sawa Yesu, kweli Mungu ni Mwenye enzi
yote na anastahili kujidhirisha kwa wote wenye mwili, wenye afya na wasio na
afya. Lakini Bwana wa dunia yote hapaswi kuwa Mungu wa haki? Je, Mwenyezi Mungu ana haki ya kumfanya mtu kipofu ili aoneshe uwezo wake wa kuponya? Bwana hivi hapa hautuchanganyi? Kama Mungu ana haki kuharibu ili atengeneze, mbona sauti ya haki ndani yangu inabisha na mimi nimeumbwa kwa mfano wake? Lakini hivi Yesu aliwaambia wanafunzi Mungu amemfanya mtu huyo kipofu iliajioneshe? Au kwa kusema hivyo tunamuwekea Yesu maneno mdomoni?
Inawezekana shida haipo kwa kauli ya
Yesu yenyewe ila kwa kauli ya Yesu kama ilivyotafsiriwa. Tukisoma kauli ya Yesu
kama Yohana alivyoandika katika kiyunani tunaona kauli ya Yesu inaweza
kufasiriwa tofauti na ilivyo sasa na kutusababishia tumfikirie Mungu vibaya.
Tuanze na mstari wa tatu wa sura hii ya tisa. Yesu asema, “Huyu hakutenda
dhambi, wala wazazi wake” (weka nukta[.] hapa badala ya semi koloni[;]). Sehemu ya
pili ya fungu la tatu inapaswa ianze na maneno, “Ili kwamba (neno la kigiriki hina ambalo linaweza kufasiriwa pia bali
kama ilivyo kwenye tafsiri ya Union Version) kazi za Mungu zidhihirishwe ndani
yake, imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku
waja asipoweza mtu kufanya kazi” (fungu 4). Hapa Yesu hakutoa tungo tata.
Kwa
hiyo ni kama namsikia Yesu anawaambia wanafunzi wake; swala hapa sio nani katenda dhambi. Mimi
ninapomtazama mgonjwa huyu ninaona fursa ya kazi. Nikitazama majeraha ya mtu simtazami
kama polisi kutaka kujua ni nani aliyemsababishia nimtie nguvu. Mimi nikitazama
udhaifu wako ninaona nimepata fursa ya kukuganga! Nimetumwa kama “Nuru ya
Ulimwengu” (9: 5) Na ninakwenda kumtia nuru kipofu huyu. Ninajua kazi yangu
itanitambulisha mimi ni nani japo utambulisho wangu unagawa watu. Ninajua sina muda, kama jua
nimepewa masaa 12 tu kuangazia vipofu wapate kuona tena. Imenipasa kufanya kazi
hii bila kujali matokeo. Ni lazima wajue mimi ni "Nuru ya Ulimwengu" (8:12).
Tukio B: Yesu akutana na kipofu mara ya kwanza
Alipokwisha
kusema hayo Yesu akaendelea mbele na kazi yake. Kwa ujasiri mwingi na huruma tele akatema mate chini
kutengeneza tope, akampaka kipofu mate usoni. Neno aliyekuwepo mwanzo wa uumbaji (Yoh 1:1-3) aliyetengeneza tope na kumuuba mtu wa kwanza (mwanzo 2:7), siye huyu amefanyika mwili na sasa anaumba tena? Wanafunzi wanaona hilo? Yesu kwa kutema mate na kutengeneza tope ni kama anamkumbusha kila mtu kisa cha uumbaji na kuwaashiria kuwa yeye ni muumbaji na anaumba upya macho haya. Nani atamuona Yesu hivyo? Yesu akaendelea mbele kumtuma kipofu aende kunawa katika bwawa la Siloamu (maana yake, Aliyetumwa). Kipofu akakubali kufanya alichotumwa kukifanya, japo haikuwa rahisi kufanya hivyo. Kwanza mpaka hapo kipofu hajaahiwa kusikia vipofu wakinawa Siloamu wanapona. Pili vipi aibu ya kutembea na tope usoni? Tatu, kwa nini aende umbali huo mpak kisimani wakati
angeyapata maji njiani kabla ya kufika huko? Mwanamume huyu anaagiza watu wafanye mambo ambayo hayaingii akilini. Lakini kipofu aliamini Yesu anaweza kuwa anania nzuri kwa kumpatia
maagizo aina hiyo. Aliyaamini, aliyatii kwa kuende kunawa Siloamu. Na
aliponawa, kipofu akarudi nyumbani anaona! Mara nyingi, maana ya maagizo ya Mwanamume huyu haionekani haraka akilini, lakini matokeo yake ni ya wazi machoni.
Tukio C: Majirani
na Kipofu anayeona
Kipofu
anayeona akarudi nyumbani na kuzua mshangao katika mitaa ya Yerusalemu—mitaa
iliyojaa nyumba zilizobanana na majirani wanaofahamiana. Kundi la watu mtaani
waliokuwa wakimfahamu kipofu kama omba-omba na kumsaidia njiani, walishtushwa kumuona na kushindwa kukubaliana na ukweli uliokutana
na macho yao. Wengine wakasema, “ndiye”; wengine, “siye ila anafananaye tu”!
Kipofu mwenyewe akiingilia kati na kuzima malumbano kwa kusema, “ni mimi, ni
mimi.” Watazamaji wakataka kujua alipataje kuona. Bila kumungunya maneno kipofu
akajibu jinsi alivyoponywa: aliniwekea tope la mate machoni, akaniamuru niende
kisimani kunawa, nikanawa na kurudi ninaona. Tangia hapo, hawakua na shaka kuwa
ni yeye na aliponaje, lakini kilichowatatiza ni nani aliyeweza kufanya kitu
hiki. Ni nani huyu aliyeweza kumponya kipofu tangu kuzaliwa? Ana mamlaka gani
ya kuponya mlemavu wa aina hii, na amepata kibali cha nani kuponya siku ya
Sabato, siku ya mapumziko, ambapo kazi yoyote ile hata ya uponyaji imepigwa
marufu na viongozi wa dini?
Maswali
hayo yalikuwa magumu mno kutatuliwa na wenyeji waliomfahamu kipofu huyu. Hivyo
wakakata rufaa kuomba msaada kwa viongozi wa dini. Ninatamani kufuatilia
viongozi wataamuaje kesi hii. Je, mtu aliyefanya uponyaji huu atakubalika kwa
kazi nzuri aliyoifanya au atapingwa bila kujali kazi nzuri aliyoifanya?
Tukio D: Mafarisayo na Kipofu anayeona
Viongozi
wa dini waliopelekewa kesi walijulikana kama mafarisayo, viongozi
walioheshimika mbele ya jamii kwa uadilifu wao kwa katiba na sheria ya Israeli.
Mafarisayo walimchukua aliyekuwa kipofu kwa mahujiano maalumu, kwanza wanataka
kuhakiki kama ni kweli alitendewa muujiza:
Mafarisayo:
Ulipataje kupona?
Aliyekuwa
kipofu: Alinitia tope juu ya macho, nami nikanawa, na sasa naona.
Mpaka
hapo mafarisayo wakaona shida katika maelezo ya kipofu aliyepokea uponyaji.
Hawakuguswa kwamba kipofu omba-omba sasa ni mzima, ila walitatizwa na mamlaka
ya mtu aliyefanya kitendo hiki. Wengine wakasema Yesu hakufanya uponyaji kwa
ridhaa ya Mungu, maana haishiki Sabato. Wakadai Yesu si chochote isipokuwa
mvunja-sheria. Lakini wengine wakakataa na kusema mtu hawezi kuwa mvunja-sheria
na hapo hapo Mungu amwezeshe kufanya muujiza huu. Basi baraza likagawanyika
pasipo maamuzi kuchukuliwa: Yesu ni nani? Ndipo mafarisayo wakamgeukia kipofu
kutaka kujua maoni yake.
Mafarisayo: Unamaoni gani juu ya mtu huyo. Wewe
unahusika zaidi kujibu swali hili, maana ni macho yako aliyoyafungua.
Kipofu: Ni nabii. Kichwani
Kipofu haoni tofauti ya Yesu na nabii Elisha eliyefanya miujiza mingi kwa idhini
ya Mungu?, Jibu lake: Yesu ni nabii
Mpaka
hapo mafarisayo hawakuridhika. Hawakudhani kuwa Yesu anaweza kuwa kama manabii
wa kale waliofanya miujiza ya kweli; maana kulikuwepo na wazushi enzi hizo,
watenda miujiza bandia.
Tukio E: Mafarisayo na Wazazi wa Kipofu anayeona
Basi
wakataka ushahidi wa kutoka kwa chanzo sahii cha habari—wazazi wa kipofu.
Wazazi watasemaje? Sikia mahojiano yao:
Mafarisayo: Mnamtambua mtu huyu, ni mtoto wenu?
Mnakubali alizaliwa kipofu? Kama ndio, alipataje kuona?
Wazazi wa Kipofu: Tunajua ni mwana wetu,
kweli alizaliwa kipofu, lakini kwa habari ya alipataje kupona hatujui.
Muulizeni mwenyewe, atajisemea mwenyewe maana ni mtu mzima.
Wazazi
walijua hatari ya kutoa ushahidi utakaothibitisha mamlaka ya Yesu juu ya
magonjwa na mapokeo yao ya utunzaji Sabato. Waliambiwa yeyote atakayemkiri Yesu
kama masihi atatupwa nje ya jamii ya Wayahudi. Nani anapenda kufutwa ushirika?
Tukio F: Mafarisayo
na Kipofu anayeona
Mafarisayo
wakamgeukia kipofu, na kutaka kumbana amkiri akili mamlaka ya Yesu ili wapate
kumuadhibu.
Mafarisayo:
mpe Mung utukufu. Tunajua huyo si nabii kama ulivyosema, ila mwenye dhambi
Kipofu:
ni mwenye dhambi mimi sijui. Najua neno moja tu, nalikuwa kipofu na sasa naona
Mafarisayo:
Alikutendea nini mpaka ukapata kuona?
Kipofu:
Niliwaambia hamkunisikia na sasa mnaniuliza tena? Mnataka kuwa wanafunzi wake?
(Kauli
hii toka kwa aliyekuwa kipofu, asiye msomi ilikuwa ni kama matusi kwa
mafarisayo wasomi. Wakakasirika)
Mafarisayo:
Labda wewe ndiwe mwanafunzi wake, sisi ni wanafunzi wa Musa mtoa Sheria. Huyu
jamaa yako hata hatujui alikotoka (wenzetu enzi hizo umashuhuru wa mtu
unauhusiano na alikotoka)
Kipofu:
Hii ni ajabu mtu mashuhuri aliyeweza kunifungua macho hamjui alikotoka? Tunajua
Mungu hutumia watu wema kufanya mema. Haijawahi kusika mtu amemfumbua macho
kipofu wa tangu kuzaliwa. Kama huyu mtu
asingelitoka kwa Mungu mwema, asingeweza kufanya wema huo?
Mafarisayo:
Ama wewe mtoto wa laana! Ulizaliwa katika dhambi tupu na unajaribu kutufundisha
sisi?
(Wakamtupa
nje)
Tukio G: Yesu na Kipofu aliyeponywa
Yesu
kusikia wamemtoa nje akamfuata na kuanza kuhojiana naye.
Yesu:
Unamwamini mwana wa mwanadamu, mjumbe wa Mungu?
Aliyekuwa Kipofu:Ni
nani nipate kumwamini?
Yesu:
Umekwisha muona, na ndiye anayesema nawe sasa
Aliyekuwa Kipofu:
Naamini Bwana. Akaanguka chini kumsujudia
Yesu:
Nimekuja ulimwenguni kuhukumu; na hukumu yangu ndio hii: wasioona waone,
wanaoona wasione.
Mafarsayo:
Unamaana umetuhukumu sisi kuwa wasioona?
Yesu:
Kama mngekuwa hamuoni nisingewahukumu mnaona, lakini sasa mnasema mnaona huku
hamuoni hamuna hudhuru na hukumu yenu ipo pale pale.
Mwanamume Huyu ni Nani? Majibu Mbalimbali
Katika injili ya Yohana miujiza ya Yesu inajulikana kama ishara. Na muujiza wa kuponywa kipofu ulikusudiwa kuamuashiria Yesu ni nani? Lakini makundi mbalimbali yaliyokutana na Yesu katika yaliitikia utambulisho wake tofauti tofaut kulingana na sababu zao mbalimbali.
Majirani wa Kipofu:
Hawana Hamu Kujua Yesu ni Nani
Kundi
la kwanza la watu walioshuhudia kazi ya Yesu ya kuwatia nuru watu ni majirani
na waliomfahamu kipofu hapo mtaani. Hawa walishuhudia mtu waliyekuwa wakimuona
mtaani kwao na kila mara wakimsaidia kama omba-omba eti sasa anaona!
Walishangaa sana wakiulizana ni kweli? Walipojua kuwa ni kweli, wakakimbia
kuwapasha habari viongozi wao. Hawa wapenda-umbeya hawana kazi nyingine
isiipokuwa kusimulia kipya walichokiona. Hawana muda wa kutafakari
walichokiona. Wanawashwa kusikia muujiza mpya, hotuba mpya, muziki mpya, lakini
hawana muda wa kutafakari walichosikia kinamfunuaje Yesu kwao. Watu wa namna
hii kwa kwa kukosa hamu kumjua Yesu, wanabakia katika upofu wao. Hapana
sisi si watu wa aina hiyo. Sisi huwa tunaimba huku tukiomba, “nataka nimjue
Yesu na nizidi kumfahamu, nijue Pendo lake kuu wokovu wake kamili. Zaidi, zaidi
zaidi...."
Mafarisayo na
Viongozi wa Dini: Hawataki Kujua Yesu ni Nani
Kundi
la pili la watu waliokutana na ushahidi wa Yesu kama Nuru ya ulimwengu ni
mafarisayo na viongozi wa dini. Hawa hawakutaka kujua Yesu ni nani. Na wanasababu zao.
Kwanza
kama viongozi, hawataki kujua wasije wakaonekana hawajui. Walijiona kama
viongozi wasomi, wakijiita wanafunzi wa Musa. Na kama wasomi walidhani wanajua
sana kiasi cha kutotegemea kufundishwa na mtu yeyote. Waliamini viongozi
waliosoma vitabu kama wao hawezi
kufundishwa na mtu ambaye hakwenda shule. Eti usomi ni kutojifunza tena! Na
hata kipofu alipowaambia mtu
aliyenifungua macho si mwingine isipokuwa nabii, mtu aliyetoka kwa
Mungu, walimtusi yeye na wazazi wake kwa kebei na dharau! Hivyo walimu wa hawa
wa dini wakakataa kufundishwa na mwanafunzi wao na wakabakia katika upumbavu
wao, bila ya wao kutambua Yesu ni nani hasa.
Wafuasi
wa Yesu sio kama mafarisayo na hawapaswi kuwa kama wao. Tofauti na mafarisayo
wakristo tunajua Yesu ni nuru ya ulimwengu. Ulimwengu wote unaangazwa na jua
hili moja. Tofauti na mafarisayo walioamini Musa ni wa Waisraeli, na hasa wao
walioisoma sheria yake, sisi wakristo tunafahamu Yesu wetu ni nuru inayomtia
nuru kila mtu, wanaoona na wasioona, viongozi kwa wafuasi, wasomi kwa wasio
wasomi. Tofauti na mafarisayo, sisi tunaamini kila mtu ameumbwa katika sura ya
Mungu na kila mtu anaangaziwa na utukufu wa Kristo.
Na
siku inakuja, nayo imefika ambapo wakristo hawatatafuta kuwa walimu zaidi
kuliko wanafunzi na waumini hawatakuwa wepesi kusema kuliko kusikia. Siku hiyo
wanaoona watafunguliwa macho na wasioona, wasomi wataelimishwa na wasio na
elimu, viongozi watawasikiliza wafuasi wao. Na siku hiyo wakristo kwa waislamu,
wakaloliki kwa waprotestanti, watunza jumapili kwa watunza jumamosi watafurahia
kuutazama utukufu wa Mungu unaoonekana katika kipaji cha uso cha mwenzake, kila
mtu atafaidika na uzoefu wa imani ya mtu mwingine. Na siku hiyo Kristo
atajulikana kweli kama nuru ya kila mtu.
Ninajua
siku hiyo inakuja maana sisi sio mafarisayo ambao walikataa kumtambua Yesu ni
nani wakidhani wanajua kila kitu na hakuna wa kuwaambia kitu.
Lakini
kuna sababu nyingine iliyowafanya mafarisayo kutotaka kumtambua Yesu. Madai ya
Yesu kama mkombozi aliyesubiriwa yalitofautiana kabisa na elimu yao. Walijua
mkombozi ajaye atakuwa mtu mashuhuri, na watu mashuhuri walijulikana kwa sehemu
mashuhuri walikotoka. Sasa Yesu hawezi kuwa mashuhuri kama mkombozi maana hata
hajulikani ametokea wapi. Wakahitimisha, Yesu hawezi kuwa masihi. Kadhalika
wayahudi walijua mkombozi ajaye atakuwa kama Musa wa pili, iweje huyu Yesu
aponye mtu katika siku ya mapumziko na hivyo kufanya kazi tofauti na Torati ya
Musa tunavyoifundisha? Yesu-mvunja sheria hawezi kuwa Musa wa pili wala
mkombozi wa Israeli. Mpaka hapo utaona Mafarisayo hawakuwa tayari habari yoyote
mpya inayotofautiana mtizamo wao wa kidini.
Wazazi wa Kipofu:
Hawana ujasiri kueleza Yesu ni Nani
Kundi
la tatu lililoshuhudia jinsi uponyaji wa kipofu ulivyomtangaza Yesu ni wazazi
wenyewe wa kipofu. Wao walijua lakini hawakuwa na ujasiri wa kueleza
walichojua. Walijua mtoto wao aliyezaliwa kipofu ndiye anayesimama mbele yao
anaona. Walijua aliyeweza kufanya hivyo ni mkombozi kutoka kwa Mungu. Miujiza
ya namna hii ndio walisikia manabii wa kale wakiifanya, na manabii walitabiri
masihi ajaye angefungua macho ya vipofu. Walijua Yesu aliyefanya hivi si
mwingine ila masihi. Lakini walipoulizwa kushuhudia kwa maneno imani yao kwa
aliyemponya mtoto wao, walikwepa kwa hofu ya kutengwa na kunyanyaswa na vyombo
vya dola.
Mpaka
injili ya Yohana inafungwa, hatujasikia wazazi wa kipofu wakiwa wanafunzi wa
Yesu. Huwezi kumtambua Yesu ni nani bila kumtangaza na bado ukawa
mfuasi wa Yesu. Imani isiyokugharimu haina thamani, ikikugharimu utaithamini. Kama unajua Yesu ni nani
usiogope kumtangaza kwa gharama yoyote na utaufurahia uhusiano wako naye.
Kipofu Anayeona:
Hana woga kukiri Yesu ni Nani
Kati
ya makundi yote yaliyoshuhudia uponyaji alioufanya Yesu ni kipofu pekee
aliyefunguliwa macho ndiye aliyepata kumtambua Yesu ni nani. Maneno ya Yesu
yalidhirika ukweli wake: “mimi nimekuja ulimwenguni humu kwa hukumu, ili wao
wasioona waone, na wanaoona wawe vipofu” (39). Nuru ya Yesu iliyomfungua kipofu
haikumuangukia kwa ghafla na kwa wingi usoni hata kumpofusha asiuone utukufu wa
Yesu. Yesu alijifunua kwake taratibu taratibu na kipofu hakusita kuifuata nuru
iliyokuwa ikimuangazia hatu kwa hatua. Mwanzoni alipoulizwa majirani zake nani
aliyekuponya, alijibu, “mtu yule aitwaye Yesu” (11), baada alipoulizwa na
mafarisayo anamwonaje Yesu, alijibu bila woga, “nabii” (17) na baadaye kidogo
akaongeza kusema Yesu ni mtenda miujiza aliyetoka kwa Mungu (30-33). Baadaye
Yesu alipojitambulisha kwake hekaluni, akaanguka chini kumsujudia akimuita,
“Bwana.”
Kipofu
anayeoona ni mfano wa kuigwa wa namna sahii ya kumuitikia Yesu kama Nuru ya
ulimwengu. Nuru inapokuangazia usiipuuze kuifuatilia kama majirani
walivyoipuuza wakabakia gizani, usiiogope kuikuikubali hadharani kama wazazi wa
kipofu walivyokwepa kuikiri wakabakia gizani, na wala usipingane nayo kwa nguvu
kama mafarisayo ukabakia gizani. Kubali hivi leo kutembea nuruni
Yesu ni Nuru ya Ulimwengu
Siulizi tena kwa nini mwanamume huyu agawe watu. Kwa kauli na matendo Yesu alijitambulisha kama Nuru ya Ulimwengu na hasa katika sura ya tisa ya Yohana. Hakumungunya maneno aliponena na hakuficha matendo alipoyatenda. Alikuwa wazi kama nuru. Lakini kama ilivyo asili ya nuru Yesu huangaza na kutia giza. Kwa wanaomkubali Yeye ni taa iongozayo wanaomkata ni giza la kujikwaa. Nuru ni ile ile, lakini humtia nuru macho huyu na humtia giza mwinginge. Wasioona wanaona na wanaoona wasione. Uamuzi ni wa mpokeaji. Amua leo pamoja nami kumkubali mwanamume huyu ili upokee nuru na uzima na furaha!