13/02/2014

Kanisa Linavyosimama Mbele za Yesu: Ufafanuzi wa Mathayo 16:13-19

0. Utangulizi

Watu wana mitazamo mbalimbali. Hata kuhusu kanisa watu wanaliangalia  tofauti tofauti. Kanisa linaweza kuonekana vizuri kwa macho ya mmoja mwingine likaoneka vibaya. Tofauti ipo machoni, kwani uzuri wa kitu upo katika macho ya mwonaji: 
  • Kwa macho ya mwingine kanisa ni kama “kimbilio la wanyonge” huku kwa mwingine ni kama “nyumba iliyohamwa siku nyingi” (uzuri wa kitu upo katika macho ya mwonaji). 
  • Kwa mwingine kanisa ni mgodi wa hazina ya milele huku wengine  kanisa ni shimo lililojaa mapokeo ya zamani (uzuri wa kitu upo katika macho ya mwonaji). 
  • Kwa mwingine kanisa la Lutherani ndio kanisa na huku kwa mwingine Katoliki ndio kanisa (uzuri wa kitu upo katika macho ya mwonaji). 
  • Tena kwa mwingine kanisa ni Wapentekoste na kwa mwingine ni Wa Sabato (uzuri wa kitu upo katika macho ya mwonaji).

Lakini macho yetu sio kiongozi amini. Leo yananionesha mwanamke yule kuwa anapendeza. Kesho yananionesha mwingine na kunifanya nipoteze hamu na wa jana. Hata kanisa nililoliona jana limejaa ngano leo naliona limejaa magugu tupu. Macho yetu si kiongozi wa kuaminika, hayatulii.

Macho ya Kristo pekee hayachezi-chezi. Yanatulia yanapotazama. Zaidi ya tochi macho ya Yesu yanapenya ngozi nakufika mpaka moyoni. Yanaona uzuri na udhaifu uliofichika. Mtazamo wa Mungu ni sahii.

Na hapo nakusikia unauliza, hivi Mungu analitazamaje kanisa? Mungu anawachukuliaje watu wake? Swali zuri namna gani! Japo swali hili laulizwa leo, bahati nzuri jibu lake ni la zamani na uhakika kama injili ya Mathayo.

Kabla Yesu hajawaambia wanafunzi wake mtazamo wake juu ya kanisa alijaribu kuwauliza wao wanamtazamaje.  “Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa nani?” (Mathayo 16:13). 

Na Yesu akapewa majibu. Majibu tofauti-tofauti kutoka mitazamo yao tofauti-tofauti. Kulikuwa na hao waliosema Yesu ni Yohana Mbatizaji; wengine walisema Yesu ni Eliya; Yesu ni Yeremia; Yesu ni mmojawapo wa manabii. Bila shaka Yesu alihuzunishwa na majibu yao. Kwa sababu Yesu alikuwa zaidi ya Yohana Mbatizaji, Eliya, Yeremia, au nabii. 

Baadaye, Petro akamtuliza Yesu kwa jibu sahii: “Wewe ndiwe Kristo (Masihi-Mkombozi aliyetumwa na Mungu), Mwana wa Mungu aliye hai?” Haleluya! Hapo, hapo Yesu akampongeza akimwambia, una bahati, huo sio mtazamo wa kibinadamu, “mwili na damu havikufunulia hili, bali baba yangu aliye mbinguni”(fungu la 18). Kwa lugha nyingine, Petro kwa kuwa unanitazama kwa macho ya imani kama mwana wa Mungu na mkombozi, subiri nitakueleza watu wenye imani kama yako ninavyowatazama. Kaa chini basi nilitambulisha kanisa langu kwako kama ninavyolitazama. Umesikia Yesu anavyolitambulishaje kanisa lake?

1. Kanisa ni Kama Jengo lililosimama Mwambani


Kwanza kabisa ninamsikia Yesu akilitambulisha kanisa kama Jengo lililosimama Mwambani (angalia nami fungu la 18a) “Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu”.

Lakini unaweza kuuliza kuna uhusiano gani kati ya Petro, Mwamba, na kanisa, hata tuseme Yesu analiona kanisa likiwa limejengwa mwambani? Kabla hatujauona uhusiano huo inabidi kuvitazama vipande vya sentensi hii kimoja-kimoja na kwa ukaribu kabla hatujavitazama katika ujumla wake.



Tuanze na Petro. Yesu anapompongeza Petro kwa kumtambua hamwiti Petro, isipokuwa anamwita Simoni Baryona, hilo ndilo jina lake alilopewa na wazazi wake. Petro ni jina la kupewa-“jina la ubatizo” (Yoh 1:42). Petro  lina maana katika kiyunani kama mwamba. Na katika kiaramaki (lugha mama ya Yesu na Petro) mwamba huitwa kefa. Kwa kuwa Yesu alikuwa anaongea na Petro kwa kiaramaki bila shaka Yesu aliongea hivi: “Wewe ndiwe Kefa (mwamba) na juu ya kefa (mwamba) hili nitalijenga kanisa langu”

Simon Baryona anaitwa Kefa na juu yake Kanisa litajengwa? Kweli Yesu, Simon Baryona ni mwamba? Mbona baadaye Simon Baryona ulimwita shetani alipotaka kukuzuia usiongelee habari ya msalaba? Simon Baryona ni mwamba? Mbona baadaye ulimwambia “Shetani anataka kukupeta, lakini nimekuombea imani yako isitindike” Simoni Baryona ni mwamba? Mbona baadaye alikukimbia dhoruba ya mateso ilipoanguka? Ni mwamba gani unaoweza kusogea? Simon Baryona ni mwamba? Kanisa linawezaje kuwa imara kama litajengwa juu ya “kefa” hili? Bwana unamwona sawa sawa Petro? Hapana, hapana,  Petro kama Petro anaitwa Mwamba lakini tunamfahamu kama kijiwe, hawezi kuhimili uzito wa Jengo la kanisa na kanisa haliwezi kuwa salama likisimama juu ya Petro tunayemjua.

Tulia, tulia….Ni kweli Simoni mwana wa Yona ni sawa na wanadamu wengine. Lakini hapa Simon ameonesha ukefa, upetro, umbwamba. Na ninyi ni mashahidi, wengi wamechagua kuyumbishwa na upepo wa maoni ya watu kunihusu mimi. Wengi wameniona kama Yohana Mbatizaji, Eliya, Yeremia, na kama nabii tuu. Lakini hapa Simon amejibu kama Petro (jiwe); amekataa kusogezwa na maoni ya wengi, kama mwamba usivyosukumwa na upepo. Petro ni muumini wa kwanza kunikiri mimi kama Mwana wa Mungu. Imani ya Petro kwangu kama Masihi na Mwana wa Mungu ni mwamba imara na salama ambao juu yake nitalijenga kanisa langu. Kama unasita uliza historia. 

Na hapo labda unataka kujua, Je! Yesu alijenga kanisa lake juu ya imani ya Petro? Ni kweli kanisa leo linasimama juu ya imani ya mtume Petro:
  • Katika mathayo 16:16 Petro ni wa kwanza kumkiri Yesu kama Mwana wa Mungu.
  • Katika Matendo sura ya 2 Petro ndio wa kwanza kumtangaza Yesu kama Masihi na Mwana wa Mungu kwa Wayahudi
  • Na katika Matendo sura ya 10 tunamkuta Petro tena kama mhubri wa kwanza wa Yesu kama Masihi na Mwana wa Mungu kwa Wamataifa.


Kwa kifupi wayahudi kwa wamataifa wanaikiri imaini ile ile ya Petro kwa Yesu. Kama Petro wakristo leo: 
  • Tunaamini Yesu ni Masihi na Mwana wa Mungu hata kama wengine hawaamini hivyo.
  • Leo hii tunaamini Yesu ni Masihi aliyetumwa na Mungu kutukomboa hata kama wengine hawamuoni hivyo. 
  • Tunamwona Yesu kama Mungu mwenye nguvu hata kama wengine wanamwona ni mwana wa Mariam tu. 

Na ni imani hii ndio inayotufanya tusalie salama kama jengo lililosimama mwambani. Imani hii na mtazamo huu ndio mwamba. Msingi wa maoni ya wengi kuhusu Yesu kama nabii tu, mwalimu tu hautufai kusimamisha imani yetu juu yake. Misingi hiyo haitulii kama mchanga wa mwambao. Leo ipo kesho imechukuliwa na maji. Tunaposongwa na mitazamo tofauti tofauti juu ya Yesu ni muhimu kutoyumbishwa kama Petro. Na tukisimamia katika imani ya Petro tuko salama.

Hivyo, mbele ya macho ya Yesu kanisa la Mungu ni Jengo linalosimama juu ya mwamba wa imani. Ndivyo linavyosimama mbele ya macho ya Yesu.

2. Kanisa ni kama Jeshi lililoko uwanja wa vita

Tena, ninamsikia Yesu akitambulisha kanisa kama Jeshi lililo katika uwanja wa vita (angalia  Math 16:18b). Yesu anasema, “milango ya kuzimu haitalishinda [kanisa langu]” Kwa maneno hayo Yesu analiona kanisa kama Jeshi lililoko vitani linapambana. 

Lakini kanisa linashindana na nani? Linashindana na milango ya kuzimu. Na hapa kuzimu haiwakilishi kitu kingine isipokuwa mauti na kifo (uf 1:18). Kutoka kwa dhambi ya Adamu na wengine tunajua dhambi huzaa mauti (Yak 1:15). Na kama dhambi huzaa mauti, basi kanisa linapambana na dhambi na mauti--baba na mtoto. Adui wa kanisa sio wewe sio mimi na wala si wao; adui wa kanisa sio waislamu wala wapagani, adui wa kanisa sio viongozi wake wala washiriki wake; adui wa mtu sio baba yake, sio mme wake na wala sio watoto wake; labda tu kama wamegeuka kuwa mawakala wa kifo na mauti.

Kanisa halijatulia na haliwezi kutulia, mpaka limeondolewa uwanjani mwa vita, na dhambi na kifo vimetupwa Jehanamu. Wale wanaolilia utulivu na amani watusubiri malangoni mwa Yerusalemu. Huko ndiko hakuna maombolezo wala kilio wala maumivu (ufu 21:4). Wale wanalalamikia magugu yamezidi kutubanaa, uovu umetusonga zaidi, watusubirie siku ya hukumu ambapo wema na wabaya watatenganishwa milele. Kanisa ni Jeshi lililoko vitani, hivyo ndivyo Yesu anavyoliona.

Wewe na mimi tuko vitani. Inawezekana tumemkimbia Yesu, tumemkana hadharani,…. Hilo halitukatishi tamaa, tunajua tuko vitani. Tunaweza kutetereka na kujeruhiwa. Si neno, lakini hatutaitupilia mbali imani yetu. Mapambano yanaweza kuwa makari na majeraha yetu yakatupunguzia damu nyingi na kutuliza usiku kucha, lakini hatutatupilia mbali silaha yetu na imani yetu. Vidole vya wanao tushtumu na kutushtaki vinaweza kuelekezwa mioyoni mwetu na kutukumbusha tulivyomkana Yesu, hatutakata tamaa kutumaini wema wa Yesu. Kama tutabakia uwanja wa vita, hakika tutashinda. Maana Yesu anasema, “milango ya kuzimu”hayatamshinda muumini anayemtumainia Yesu kama Petro. Kama jiwe lililowekwa mlangoni mwa kaburi la Yesu halikuweza kumzuia Yesu siku ya Jumapili ile, kadhalika hata sisi “milango ya kuzimu haitatushinda” tunaposhikiria imani yetu. 

Kujua kuwa kanisa liko vitani kunanifanya nisilikatie tamaa ninapolitazama. Hata mimi kujua niko vitani kunanifanya nisijikatie tamaa katika mapambano ya maisha na imani. Kanisa ni la wapiganaji.

Mbele ya Yesu Kanisa ni zaidi ya jengo lilosimama mwambani, isipokuwa ni  Jeshi linaloshindana vitani. Hivyo ndivyo Yesu anataka kila mmoja alitambua kanisa lake hivyo. Na zaidi ya hapo Yesu analitambua kanisa kama mlinzi wa malango ya ufalme wa mbinguni


3. Kanisa kama mlinzi wa malango ya ufalme wa mbinguni

Katika aya hii ya Mathayo 16 Yesu anamalizia kulitambulisha kanisa kama Mlinzi wa malango ya ufalme (angalia nami fungu la 19): “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni”. Kwa maneno mengine Yesu anasema, "Kefa nitakupa  wewe funguo [wewe kefa ambaye hukuteteleka kunikiri mimi kama Masihi na Mwana wa Mungu]. Wewe ni mshika funguo, mlinzi katika malango ya ufalme.” Unaweza kufunga na kufungua, kuruhusu na kuzuia, wewe ni mlinzi.

Lakini Kefa au waumini wanaokiri imani ya Kefa ni walinzi wa namna gani mlangoni pa ufalme?  

Kabla hatujalielewa maana ya ufunguo: unakumbuka maneno ya Yesu kwa walimu wa dini katika Luka 11:52? Yesu alisema, “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia.” Mahali pengine Yesu anawalaumu Mafarisayo (washika dini) kwa kosa hilo hilo (Math 23:13). Mara zote hizo funguo zinasimama badala ya maarifa na ujuzi waliopewa. Wana-sheria na Mafarisayo walikuwa na ujuzi wa maandiko ambao ungeweza kuwanufaisha wao na wengine. Lakini hawakutumia maarifa hayo ipasavyo.

Na kwa Petro na waumini wote, ujuzi na maarifa ya ufalme umetolewa.
Petro na waumini tumefunuliwa na Baba wa mbinguni kumwona Yesu kama Masihi na Mwana wa Mungu. Ufunuo huo ni ufunguo langoni mwa ufalme. Injili ya Yesu yaweza kuwafungulia malango ya ufalme wote wanaoipokea na kuwafungia malango hayo hayo wanapoikataa. Petro na sisi wakristo tumepewa funguo nyeti. 

Lakini mwenzetu Petro alizitumiaje funguo zake? Historia takatifu imerekodi kwa ufasaha jinsi mtume Petro alivyotumia maarifa ya kumjua Yesu masihi, kwa mfano: 
  • Petro alizitumia funguo hizo siku ya Pentekoste alipowaonesha wayahudi  kuwa Yesu ni Masihi na Mwana wa Mungu aliye hai. Akawaambia, “Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi” (Mdo 2:38). Na siku ile wengi kwa kumsikia Petro na kukubali  ujumbe wake walifunguliwa malango ya ufalme—tunaambiwa maelfu.
  • Mara nyingine Petro alimfungulia malango ya ufalme Kornelio na nyumba yake na wote wakaingia (Mdo 10)
  • Mara nyingine Petro  akiwa na Yohana alimfungulia kiwete langoni mwa hekalu naye akapokea uponyaji
  • Mara nyingine Petro na Yohana wakawafungulia wasamaria nao wakapokea Roho Mtakatifu
  • Lakini mara nyingine Petro alimfungia Anania na Safira na hawakuingia katika ufalme

Funguo alizopewa Petro ndizo tulizopewa. Tumepewa kuwafungulia watu wamjue Yesu kama Mkombozi nao wafunguliwe. Na kama kila mmoja wetu aliyepewafunguo hizi atazitumia wangapi wangepokea msamaha wa dhambi, wangapi wangefunguliwa na utumwa wa dhambi, wangapi wangepokea uponyaji. Yesu analitambulisha Kanisa kama walinzi katika malango ya ufalme. Ni bahati kuu kiasi gani lakini ni wajibu mzito namna gani kumiliki funguo za lango kuu la uzima?

0. Mwisho


Ninapomaliza kutafakari mazungumzo ya Yesu na Petro kuhusiana na kanisa lake niseme: Usiamini macho yako. Amini macho ya Yesu. Na Yesu anawatazama watu wake wanaomwamini kama kama Jengo mwambani, askari vitani, na mlinzi mlangoni. Kama unamwamini yeye, Yesu anakwambia wewe: unabakia salama kama mwamba unaponiamini, utapata ushindi kama jemedari unaponiamini, na una wajibu wa kuwafungulia wengine waniamini kama askari langoni. Mwombe Yesu akupe macho yake na ubarikiwe.