12/06/2013

Yesu, Petro, na Upendo: Shule ya Upendo katika bichi ya Galilaya (Yohana 21:15-17)

(Hubiri hili lilitolewa Kana SDA church Machi 2013, Tanga; na Sahare SDA Church, Tanga Mei 2013)

Utangulizi

Mwanamke asiye na Upendo wa Kweli

Nimewahi soma hadithi ya mwanamke mmoja ambaye hakufurahia tena kumpenda mwenziye. Mumewe mama huyu alikuwa mgonjwa; ikabidi ampeleke kwa daktari.  Walipofika, daktari alibaki na mgonjwa ofisini kwa uchunguzi huku mwanamke akibaki katika ukumbi wa mapokezi akimsubiria. Daktari alipomaliza uchunguzi, akaja kukutana na mke wa mgonjwa   akiwa na uso wa huzuni. Mwanamke kumwona daktari hivyo, hakuweza kutulia. Haraka akauliza, “Daktari, mme wangu atapona?” Daktari akakusanya ujasiri na kumjibu: “ninaona mme wako ni mgonjwa sana; na asipohudumiwa vya kutosha, hakika atakufa.”

Mwanamke akachoshwa kusikia hivyo! Baada ya kuvuta pumzi kidogo, akuuliza, “una maana kuna matibabu yanayoweza kuokoa maisha ya mpenzi wangu”? “Ndio” Daktari alijibu na kumwambia, “mmewe akipata matibabu stahiki na huduma bora anaweza kuishi miaka mingi zaidi. Zaidi ya dawa atakazopatiwa itabidi umpatie mwenzako huduma zifuatazo:
  • Mrudishe nyumbani mgonjwa na umfanye kama mfalme,
  • Mtayarishie chakula ulichopika mwenyewe,
  • Mletee chai ya asubuhi kitandani,
  • Nawisha mikono yake kabla na baada ya kula,
  • Usimruhusu afanye chochote unachoweza kumfanyia,
  • Kama anahitaji kitu mpelekee,
  • Mminye-minye mgongoni asubuhi na jioni; mkande-mkande mwili mzima na mikono yako uliyoilainisha kwa mafuta,
  • Aha..kuna lingine pia: kwa kuwa uwezo wa mgonjwa kukabiliana na magonjwa ni mdogo, hakikisha nyumba yako ni safi muda wote.
Baada ya maelezo hayo, mganga akamuuliza mwanamke kama ana swali lolote. Mwanamke akatulia, pasipo swali la kuuliza wala neno la kuongeza. Ndipo daktari akavunja ukimya na kamuuliza, “je, unataka nimwambie mumewe kinachomsumbua na huduma stahiki anayostahili kuipata au utamwambia mwenyewe”? Mke akazinduka na kujibu, “usijali, nitakwenda kumwambia mwenyewe.”

Basi daktari akamwacha na mwanamke akaenda kukutana na mumewe. Lakini alifika chumba  alipokuwapo mgonjwa mwanamke alikuwa angali na uso ulioshuka na mashavu yaliyosinyaa. Mumewe alipomwona hivyo akahisi mambo yameharibika na kuharakisha kumuuliza, “vipi mpenzi, hali yangu ni mbaya sana? Kwani ninaumwa nini?” Mkewe hakujibu haraka. Akingali anaangalia chini na mikono kifuani akajibu na kumwambia, “Daktari amesema…. utakufa tu?”

Mwanamke hajajifunza kupenda kwa kweli na anashangaza! Hivi, mgonjwa wake ni wa kufa tu? Lakini  isishangaze sana. Kwani wanaume na wanawake wangapi wanaofanana na mama huyu, wangapi  wanaopenda wakati wa raha na wakati wa dhiki huishia? Wangapi wanaopenda kwa mahesabu na gharama ikizidi hukimbia? Wangapi wanaopenda kwa moyo wote?

Petro asiye na upendo wa kweli

Ninapofungua Biblia ninamkuta mwanamume mwingine aliyempenda Bwana wake lakini si kwa moyo wote. Mwanamume huyo ni Petro, mmoja wa wafuasi wa Yesu. Petro alimpenda Yesu lakini si mara zote. Kwa mfano, Petro alimpenda Bwana wake alipomwita amfuate, hata akaacha shughuli yake ya kumuingizia kipato ili kumfuata Yesu. Aliweza kufuatana na Yesu kutokea Galilaya mpaka Yudea na mpaka Yerusalemu lakini si mpaka Golgotha. Golgotha ya adha na fedheha na mateso na kifo ilikuwa mbali mno na moyo wake; msalaba ulikuwa na gharama kubwa kwa Petro kuuchukua. Kwa nini ataabike kwa ajili ya Yesu? Hata hivyo Bwana wake atakufa tu.

Hatumsemi Petro namna hii kwa kuwa hayupo hapa kukanusha au kujitetea. Rekodi takatifu na ya kuaminika inamuonesha mwanamume huyu mara kadhaa akikataa kutaabika kwa ajili ya Bwana wake. Kwanza kitabu cha Mungu kinatuonesha Petro akimuonya Yesu asizungumzie habari za kukamatwa na kuteswa kwake (). Kitabu kinatuonesha pia kwamba  muda mfupi tu wale askari walipokuja Gethsemani wamchukue Yesu akiwa katika pingu kama jangili korofi achukuliwavyo na polisi, Petro alipinga mpango huo kwa upanga (). Tena tunasoma kwamba mara Yesu alipokamatwa, Petro alitimua mbio na kuwashawishi wenzake kukimbia (). Hata alipokimbia, Petro alidai hamjui Mgalilaya  aliyefungwa pingu. Petro aliona ni bora amkane Bwana wake kuliko kutaabika pamoja naye—hata hivyo atakufa tu.

Lakini Yesu ni tofauti na mama yule na Petro huyu katika kupenda. Bwana Yesu ni wa pekee. Yesu hupenda bila kuacha: akiachwa—haachi, akichokwa—hachoki. Kumbuka, hata baada ya Petro kumuacha Yesu na kukimbilia ziwani Yesu alimfukuzia mpaka huko (Yoh 21:3). Ziwani palikuwa ni mahali mwafaka ambapo Petro alidhani angejituliza. Kwa kujishughulisha na uvuvi alidhani anaweza akajisahaulisha majuto ya kumkana Bwana wake. Alfajiri hii Yesu anapokutana na Petro, anamkuta Petro amehangaika usiku mzima bila mafanikio, amechoka; hana wazo la Yesu kichwani wala samaki nyavuni. Yesu aliyeondolewa duniani alikuwa ametoweka kichwani mwake. Lakini Yesu aliyefichika machoni pa Petro mkimbizi akaamuru nyavu zilizoshindwa kupata nyavu usiku zishushwe chini asubuhi hii. Ni samaki gani mjinga atauona mtego wa kumnasa na akaribie nyavu?  Petro alitilia shaka mbinu hiyo ya uvuvi,akidai weledi na uzoefu wake wa uvuvi haumtumi kufanya hivyo. Pamoja na mashaka hayo Petro akaona ajaribu kutii agizo, hata hivyo hajui aliyemwamuru ana nia gani. Alipotii tu, Bwana akambarikia Petro samaki wengi ajabu! Samaki walipojaa nyavuni, ndipo Yesu akarudi kichwani! Petro akang’amua kuwa kumbe ni Yesu!

Hakuna mahali Yesu hayuko
Weusi wa usiku, nuru yake iko
Sitaenda mahali Pendo lake haliko
Yupo hapo tayari kokote niendako

Kabla sijamuona, macho yake yako kwangu
Kama pumzi niivutayo, yuko karibu yangu
Zaidi ya baba, zaidi ya mama, yu rafiki yangu
Mwanzo mpaka mwisho yu uzima yangu
Niendapo popote yuko mbele yangu

Na alfajiri hiyo Yesu alitangulia mbele waliomkimbia. Alijali hata akasimamia moto kuwashwa, ili miili ya 
wavuvi iliyolowa na kutetema itiwe joto! Akasimamia uchomaji samaki-nyama choma- ili miili ya wavuvi hawa itiwe nguvu. Asubuhi hii Upendo umefanyika mwili na wavuvi  wameuona utukufu wake. Upendo unaonekana ukitangaza na kusema, Petro hutakufa tu!

Petro katika Shule ya Upendo

Petro anapopigwa butwaa na utukufu wa upendo huu, Yesu akaanzisha mazungumzo. Mazungumzo baina ya Yesu na Petro yameanza, huku wengine wakiwa wasikilizaji. Natamani nisogee pembezoni mwa mahojiano yao. Masikio yangu yanawasha kusikia Yesu anamwambia nini Petro baada ya Petro kumkimbia Yesu na Yesu kumpata Petro. Sogea pamoja nami tufuatilie mazungumzo yao kama yanavyopatikana katika Injili  kama ilivyoandikwa na Yohana, sura ya ishirini na moja. Fuatilia nami fungu la kumi na tano mpaka kumi na saba (Yoh 21:15-17). (Unapofuatilia mazungumzo haya kwenye biblia yako, linganisha na tafsiri yangu yangu ya moja kwa moja toka katika lugha aliyotumia Yohana kusimulia kisa hiki, kigiriki. Kwa makusudi nitaacha bila kubadilisha baadhi ya maneno aliyoyatumia mwandishi). Nami nasoma kama ifuatavyo:

15. walipokwishapata kifungua  kinywa, Yesu alimuuliza Simoni Petro, “Simoni mwana wa Yohana unanipenda kwa kweli [agapas me]? Naye akamjibu, “kweli Bwana wewe unajua kuwa ninakupenda kama ndugu[filoo se].” Yesu akamwambia, “Tunza wanakondoo wangu.”
16. Akamuuliza tena mara ya pili, “Simoni mwana wa Yohana! Unanipenda kwa kweli [agapas me]?” Petro akamjibu, “Kweli, Bwana; Wewe wajua kwamba ninakupenda kama ndugu [filoo se].” Yesu akamwambia, “chunga kondoo wangu.”
17. Akamuuliza mara ya tatu, “Simoni mwana wa Yohana! Je, unanipenda kama ndugu [filoo see]?” Hapo Petro akasikitika kwa sababu amemuuliza mara ya tatu, “unanipenda kama ndugu [filoo se]?” Naye akamwambia, “Bwana wewe [na si mwingine] wajua yote, wewe wajua kwamba ninakupenda kama ndugu [filoo se].”

Natumaini umeyasikia mahojiano haya. Ninapoyatafakari najiuliza,  kwa nini Yesu amsemeshe Petro namna hii? Je! inawezekana Yesu anatafuta kumsaidia Petro ajifunze kupenda wengine kwa vitendo kama Yeye Bwana anavyompenda? Kama ndiyo, kwa namna gani mazungumzo haya yanamsaidia Petro ajifunze kupenda kwa kweli? Niliporudi kwenye mahojiano hayo na maswali haya kichwani, nikaona kwamba hapa Yesu anamfundisha Petro ajifunze upya kupenda kwa kweli. Na anafanya hivyo kwa kumpatia masomo yafuatayo.

Somo la Kwanza: Jua kuwa hujui Kupenda kwa kweli

Somo la kwanza ambalo Yesu alitaka Petro ajifunze kabla hajajua kupenda kwa kweli ni kwamba hajui kupenda kwa kweli. Somo hilo Yesu alilitoa alipomwita Petro mara tatu kwa jina, “Simoni mwana wa Yohana”. Kumbuka, Simoni ni jina alilopewa na wazazi wake alipozaliwa; na Petro ni jina alilopewa na Yesu alipokubali kumfuata. Kwa nini Yesu amuite Petro kwa jina la zamani, jina alilokua akitumia kama mvuvi wa samaki na si jina la Petro alilopewa na Yesu mwenyewe alipokubali kuwa mfuasi wake? Hapa, Yesu anamwita Petro kwa jina la Simoni kumkumbusha Petro kwamba sasa amerudia jina lake la kale, kazi yake ya kale, na maisha yake ya kale. Simoni sasa amefuata samaki ziwani badala ya kufuatana na Yesu msalabani. Ni sawa Yesu amwite Petro kwa jina hilo maana sasa anapenda kuvua zaidi kuliko kumfuata Yesu. Na kama si kuitwa hivi, Petro atajuaje hajui kupenda bila kujulishwa kuwa hajui kupenda?

Lakini Yesu alipomwita Petro Simoni mwana wa Yohana –kumwita hivyo kulimsaidia Petro apate ujumbe huo?  Au Yesu aliongea fumbo ambalo ni wewe na mimi tu, wasomaji wa leo, tunaoweza kulifumbua? Hapana, ujumbe ulifika, maana Petro haoneshi tena ujuaji wa Simoni. Simoni katika injili ni mjuaji na mbishi. Muda wote alikuwa akitamba anampenda Bwana wake lakini si sasa. Kwa mfano, Petro alibisha alipoambiwa, Simoni, Simoni Shetani anataka kukuingia ili unikane na  na unikimbie (Luk 22:31-33). Petro alikataa akidai labda wengine wangefanya hivyo lakini si yeye. Tofauti na wakati huo sasa Petro anapoitwa simoni habishi wala hapingi. Nyavu zake alizonazo pembeni yake ni ushahidi tosha wa kumuaminisha kuwa hajui kupenda—na hilo ni somo la muhimu ambalo Yesu alitaka Petro ajifunze.

Yesu yupo tayari kuwasaidia wakina-Petro, wale wanaokiri kuwa wafuasi wa Bwana, kutambua kuwa
hawajui kupenda kwa kweli-wamemkimbia na kurudia maisha yao ya kale. Kama alivyomwita Petro-Simoni vile vile Yesu anawaita wanaume na wanawake wanaokiri kuwa wafuasi wake lakini wanaishi sawa sawa na majina yao ya zamani. Yesu anawaita kwa majina yao akitaja: Ewe Simoni mwana wa kujiamini, Ewe Simoni mwana wa Kujiokoa, Simoni mwana wa kujihurumia, Simoni mwana wa kujipenda. Ewe Simoni…Simoni nakuita! Swala linalobakia ni kama akina Petro wakiitwa Simoni watajitambua? Watatambua kuwa wameyaacha majina yao ya ukristo na kurudia maisha yao ya kale? Watatambua kuwa hawajui kupenda kwa kweli?

Somo la Pili: Kubali kuwa hujui kupenda kwa kweli

Naamini Petro alijifunza somo hilo la awali, kwamba amemuangusha Bwana wake, hajampenda vya kutosha. Lakini, zaidi ya kujua huku, Petro anapaswa akubali (zaidi ya kujua akubali)  kuwa hajui kupenda kabla hajajifunza kumpenda Bwana wake zaidi. Hakuna mwanafunzi anayeweza kuelimikia isipokuwa ameonesha haja ya kuelimishwa. Ndio maana Yesu anamtaka Petro akubali anahitaji kujifunza kumpenda zaidi kwa kumuuliza, “unanipenda…unanipenda…unanipenda”

Yesu hana mchezo anapomuuliza Petro “unanipenda.” Swali limechongwa na lina makali ya kutosha kuchoma moyo wa Petro na kumliza. Umesikia Yesu akiuliza na Petro akijibu? Katika kiyunani Yesu anauliza kama Petro  anampenda kwa kutumia neno tofauti na ambalo Petro analotumia kujibu. Mara mbili Yesu anamuuliza Petro, “unaniagape au unanipenda kwa kweli [agapes me]? na mara zote Petro alikwepa kujibu anamuagape, ila akajibu,  ninakufiloo, au “nakupenda kama ndugu’ [filoo see]. Yohana na watumiaji wa kiyunani cha Agano Jipya walielewa tofauti ya upendo wa Agape na Fileo, japo mara nyingine waliyatumia maneno hayo bila kuyatofautisha. Agape ni upendo wa kimbingu hasa baina ya Mungu na mtu; na fileo ni upendo wa kibinadamu baina ya ndugu na ndugu. Mungu aliu-agape ulimwengu hata akamtoa mwanae wa pekee (Yoh 3:16). Hata Yesu alipomuuliza mara ya tatu unanipenda kama ndugu! Petro alisikitika kwa kuwa swali hili la mwisho linaonesha kushindwa kwa Petro kummpenda Yesu kwa kweli, kwa moyo wote, na bila kujali gharama, kama Mungu ampendavyo mwanadamu. Mara hii ya mwisho ni kama Yesu anauliza, Petro! “Unanipenda kama umpendavyo nduguyo badala ya kama nikupendavyo? Na Petro kwa uchungu wa toba akajibu, “unajua Bwana, sijafikia kukupenda kwa kweli kama unipendavyo; ila nakupenda kama ndugu kama nilivyozoea”. Kwa kusema hivi Petro amekubali ameshindwa kumpenda Yesu kwa upendo wa kweli (agape).

Umeona? Hapa swali la Yesu kwa Petro unanipenda limefanya kazi iliyokusudiwa moyoni kwa Petro; kwani limemuongoza kukiri amepungua kupenda. Kwa kinywa chake amekiri kuwa amempenda Bwana wake kimazoea, kibinadamu, kindugu tu tofauti na matazamio ya Bwana juu yake.
Kwa kuitwa Simoni, Petro alitambua hajaendelea kumpenda Bwana wake lakini kwa kuulizwa unaniagape amekubali hajui kumpenda kwa moyo wote. Ni vizuri kukubali makosa; usipokubali utawezaje kujifunza? Na Petro alipokubali tu, Yesu hakusita kumfundisha mwanafunzi huyu apendeje.

Somo la Tatu: Hudumia wengine ufaidi upendo wa kweli


Katika mazungumzo haya hapo bichi ya Galilaya, Yesu akaendelea kumfundisha Petro kwamba atapenda kwa kweli anapohudumia wengine kwa moyo wote. Yesu akampatia somo hilo kwa kutumia kielelezo cha mchungaji na kondoo wake. Kama mchungaji anavyowapenda kondoo zake kwa kuwatunza, Petro hana budi kufanya vivyo hivyo. Kwani ulisikia katika mazungumzo yao, Petro alipokuwa akimjibu Yesu kuwa anampenda kama ndugu, Yesu alimjibu nipende kwa kutunza kondoo zangu; akimaanisha, nipende kama mchungaji apendavyo kondoo kondoo zake.

Petro atajifunza kupenda kwa kweli kwa kuiga kile mchungaji anachowafanyia kondoo zake: kutunza. Petro angalia mchungaji anavyojali kondoo zake. Kondoo wakipatwa na janga gongo la mchungaji na fimbo yake huwalinda; kondoo wakiwa na njaa mchungaji huwapeleka “katika malisho ya majani mabichi”; wakiona njaa huwapitisha “kando ya maji matulivu”; wakipotea huwarejesha zizini. Kondoo wakivamiwa mchungaji hakimbii akisema hata hivyo watakufa tu; isipokuwa anatetea maisha yao hata kwa gharama ya kupoteza maisha yake mwenyewe (Yoh 10:11). Petro unanipenda? Iga mchungaji anavyowatunza kondoo wake.

Namna ya kuhudumia wengine kwa upendo

Kwa vipi Petro anaweza kupenda kama mchungaji mwema anavyojali  kondoo zake? Unawezaje pia?

Waone wahudumiwa kama sehemu ya nafsi yako


Ili Petro afikie kujali wengine kama mchungaji wa kondoo, anapaswa kwanza kuwaona  wengine kama sehemu ya nafsi yake mwenyewe. Utakumbuka Yesu alisema mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake (10:11). Na hiyo ina maana kwamba mchungaji anawatazama kondoo wake kama sehemu ya nafsi yake, anawathamini kama anavyothamini nafsi yake, hata kuweza kubadilishana nafsi yake kwa uhai wao. Kwa macho ya mchungaji mwema: wao ni yeye na yeye ni wao. Lakini mchungaji asiyejali huwaona kondoo kwa macho tofauti kabisa. Anawaona wao kama wao. Anawatofautisha kondoo na nafsi yake. Hata kondoo wakipatwa na hatari, yeye ni wa kwanza kuwakimbia. Maslahi yake ni ya muhimu kuliko mahitaji ya kondoo (Yoh .) Kwa macho ya mchungaji wa mshahara mimi ni mimi na wao ni wao. Wao wakifa bado mimi ni salama!

Hapana, hapana haipaswi iwe hivyo! Petro hataweza kupenda kondoo kama atajiona yeye ni yeye na wao ni wao. Hata sisi hatuwezi kupendana kama tuwaona wao ni wao na sisi ni sisi; sisi ni wanadamu wao ni wanyama tu, sisi tunahaki ya kuishi wao hawana. Hata Paulo katika Matendo 17 Paulo myahudi akiongea na wagiriki wa mji wa Atheni alisema, hakutofautisha wayahudi na wayunani, Yerusalemu na Atheni aliponukuu mshahiri wa kigiriki kusema, “Sisi wote ni uzao wake” (Mdo 17:28).

Na kama Paulo yuko sahii basi hakuna ukuta wa kututenga sisi na wao. Nyumbani mwa Baba yetu sisi ni sisi: hakuna weupe kwa weusi, wamakonde kwa wachaga, wakenya na watanzania, wakristo kwa waislamu, wanawake kwa wanaume, matajiri kwa maskini, vijana kwa vikongwe, walemavu wa ngozi na wasio walemavu wanashiriki damu moja. Wenzetu wakipoteza maisha ni damu yetu imepotea, wakitembea uchi ni jina letu limeaibika, wakikosa chakula, madawa, na elimu ni sisi tumekosa. Hatuwezi kutojali ndugu zetu wakibaguliwa, wakionewa, wakisingiziwa uongo, wakiingiliwa kwa nguvu. Sisi ni walinzi wa ndugu zetu kuwatetea, kuwalinda, na kuwaokoa. Maana wao ni sisi. Wao hawawezi kufa sisi tukiwaangalia! Na ndivyo mchungaji wa kondoo anavyowatazama kondoo zake— anawachukulia wao kama yeye.
Lakini kwa vipi tena Petro anaweza kupenda wengine kwa kweli kama mchungaji mwema apendavyo kondoo zake?

Waone wahudumiwa kama mwili wa Yesu


Zaidi ya kuwaona kondoo kama sehemu ya nafsi yake, Petro anapaswa kuwaona wengine kama mwili wa Bwana Yesu mwenyewe. Kumbuka, Yesu alipomuuliza Petro unanipenda Yesu alijibu tunza kondoo zangu. Kwa lugha nyingine Yesu anasema, Petro unapowatazama kondoo nione mimi mwenye mali. Mimi sitakuwepo pamoja nawe kimwili kupokea upendo wako, lakini nina kondoo wenye  chapa yangu pamoja nawe. Tambua sura yangu juu yao na unipende mimi kwa kuwapenda wao. Maana mimi mchungaji na kondoo zangu tu wale wale.

Rafiki, somo alilopewa Petro latufaa sisi pia. Huwezi kusema unampenda mzazi lakini si watoto wake, huwezi kumpenda Mungu usiyemuona huku ukiwachukia viumbe walioumbwa kwa sura yake. Hivyo, utajifunza kumpenda Mchungaji kwa kuwapenda kondoo wake:
  • utajifunza kumtumikia Mungu kwa kutumikia watu wake
  • utajifunza kumtetea Mungu kwa kutetea watu wake
  • utajifunza kumsikia Mungu kwa kusikiliza watu wake
  • utajifunza kumsifia Mungu kwa kupongeza watu wake
  • utajifunza kumfurahisha Mungu kwa kufurahisha watu wake
  • utajifunza kushirikiana na Mungu kwa kushirikiana na watu wake
Petro, kwa kuwa Mungu na watu ni kitu kimoja, penda Mungu kwa kupenda watu.

Umuhimu wa kujua kuhudumia wengine kwa Upendo


Na hilo ni somo la msingi na la muhimu kwa wanafunzi wote makini wanaotaka kufaulu kupenda kwa kweli. Maishani kila mmoja anapimwa upendo wake na siku ya mwisho ya hukumu, kila mmoja atatahiniwa ufaulu wa somo hilo.

Ukijua utaepuka kuwa siku ya mwisho kwenye kundi la walioshindwa


Hata kabla ya siku hiyo ya hukumu orodha ya watakaofeli imekwisha bandikwa katika ubao wa matangazo. Katika sura ya ishirini na tano ya injili ya Mathayo, orodha waliofaulu kumpenda Bwana Yesu kwa kweli inashangaza. Orodha inapungukiwa na majina yaliyoyatazamiwa na wengi. Wengi wa wahubiri walioweza kunena kama malaika hawakuwamo, waliokuwa wajuzi wa unabii na siri zote na maarifa yote hawakuwamo. Wengi wa waliokuwa na imani za kuamisha milima hawakuwamo, waliotoa mali kulisha maskini hawakuwamo, waliojilipua kama wafia dini hawakuwamo. Eti hao wote walifeli kwa kuwa walikuwa wakitumikia majina yao na matumbo yao badala ya kuwatumikia watu wa Mungu! Jifunze kupenda leo usije ukapatikana katika kundi hili.

Ukijua utaweza kuwepo siku ya mwisho kwenye kundi la walioshinda


Na ajabu majina ya waliofaulu kupenda watu kwa kweli yanajulikana. Mathayo anawataja washindi hao kama wale waliolisha wenye njaa, walionywesha wenye kiu, waliowatazama wagonjwa, waliotembelea wafungwa, waliokaribisha wageni. Eti hao ndio wapenda watu, hao ndiyo wenye dini safi, isiyo na hitilafu mbele za Mungu (ling. Yak 1:27).

Ukijua utaweza kuwepo leo kwenye kundi la wanaofurahia maisha


Basi nikawa na hamu kujua hawa waliofaulu walikuwa na siri gani ya ushindi? Mbona wengine kama wao walifanya kazi hizi wazifanyazo lakini wakafeli? Hivi wanajua watafaulu? Ile siku ya mwisho watajitapa wakisema, “ndio tulijua tutafaulu, hata rekodi na takwimu ya mema yetu tunayo yanatushuhudia kuwa sisi ni wa kufaulu tu?” Cha ajabu haikuwa hivyo; wale waliofaulu walishangaa wamefaulu! Kumbe hawa walikuwa wasahaulifu. Walisahau mema waliyotenda walipowafadhili wengine. Walipofadhili hawakutafuta mambo yao, hawakujivuna, hawakujitangaza. Walikuwa wasahaulifu kweli kweli! Hawa walisahau mabaya waliyotendewa walipowasamehe wengine, wakasahau uchungu wote, wakavumilia yote, wakastahimili yote. Hata hawakujua walikuwa wanapimwa walipokuwa wanaitikia mahitaji ya watu. Ndio maana watauliza, Bwana ni lini tulikufanyia haya? Yesu atawajibu, “kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo mlinitendea mimi” (Mathayo 25:40). Kadri mlivyojali kondoo zangu mlinijali mimi. Kumbe siri ya ushindi wao ilikuwa nikujisahau katika kuwakumbuka wengine.

Bila shaka Petro alilielewa somo hili. Ukisoma barua ya Petro ya kwanza utamuona Petro aliyejifunza kupenda kwa kutenda. Katika 1 Petro 5 Petro anawasihi wachungaji wenzie walichunge kundi la kondoo, si kwa kulazimishwa, si kwa kutaka fedha za aibu, bali kwa hiari na moyo wa kutaka kumfurahisha Mchungaji Mungu. Maana Petro mwenyewe anawaambia, “na mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyonyauka” (fungu 4). Ni wazi Petro ameelewa somo: upendo wa kweli hautoki moyoni kwa kusukumwa au kushinikizwa bila hiari na mahitaji ya watu; bali huwamwagikia  wengine kutoka katika hazina yake pasipo kuzuiwa na ubinafsi, hata huduma haiwi tena wajibu bali burudani.

Mwisho


Nimalizie kusema wewe na mimi tuna bahati. Tunabahati kujifunza kutoka kwa makosa ya mama yule na Petro huyu. Hatuna haja kurudia kumkana Bwana wala kuwaacha wahitaji wanaotunzunguka wafie mbali, na huku tukidai ni wafuasi wanaompenda Mungu. Tuna bahati kujifunza toka katika kinywa cha Yesu akimfundisha Petro namna ya kupenda kwa kweli. Nadharia imepatikana tayari, kilichobaki ni vitendo. Basi tunapoamua sasa kubadilisha elimu hii kuwa vitendo halisi, tuombe.

Ombi:

Bwana na Mchungaji wetu mwema, tunakushukuru kuvumiliana nasi katika kutufundisha kupenda. Ninajua sasa na ninakubali ujazo wa upendo moyoni mwangu umepungua sana. Nihurumie sasa na unijaze upya. Nipe kuwajali wengine kama unavyonijali mimi, nipe kujisahau katika kuwakumbuka wengine. Tena unipe kutumika kupenda na usikose kunipa furaha ya kupenda kutumika. Ahsante Bwana kwa kuwa umenipa nafasi nyingine ya kupenda watu. Utukuzwe kwa neema yako, na uweza wako, sasa na hata milele. Ameni.

Na Bwana akubariki sana sana unapopenda watu. Hata wakati mwingine, kwa heri.