29/03/2013

Ndoa ni Taasisi Yenye Heshima Kuu (Mwanzo 2:18-24)




H
akuna heshima ya juu ambayo Mungu anaweza kukupatia kama wakati unapofunga ndoa na mpenzi wako. Na hiyo ndiyo heshima ambayo Mungu aliwapatia wazazi wetu wa kwanza.  Adamu na Hawa walipokea heshima ya ndoa walipokuwa bado wanaheshimika kama watoto wapya wa Mungu, waliotoka tu mikononi mwa Muumbaji wao. Tunajifunza kutoka katika sura ya kwanza na ya pili ya kitabu cha Mwanzo kwamba Mungu alimweka Adamu bustanini Edeni. Mungu alimpatia Adamu hadhi ya mtawala/mfalme chini yake. Na kama mfalme wa sayari dunia Mungu akampitishia wanyama wa aina zote ili awapatie majina. Pamoja na kazi ya heshima aliyopewa, Adamu alipomaliza kuifanya alijihisi kama mtawala mpweke (umewahi kujikuta umezingirwa na vitu na watu lakini bado mpweke?). Kwa Adamu, ilikuwa dhahiri kwamba hakukuwa na kiumbe yeyote ambaye angemfaa kama “msaidizi wa kufanana naye”(Mw 2:18,20). Mpaka hapo, mbele ya wengine Adamu alikuwa mfalme aliyetukuka kwa kupewa milki kubwa isiyopungukiwa na aina za viumbe; lakini mbele ya macho yake, Adamu anajiona mwenyewe akiwa amepungukiwa.  Na ni ndoa pekee ndio ingeweza kuziba pengo lililojitokeza pembezoni mwa Adamu mfalme.

Lakini inakuwaje kazi ya Mungu ya kwanza ipatikane na mapengo? Adamu alipunguaje wakati ndio tu ametoka kuumbwa? Mwandishi wa kitabu cha Mwanzo anapotoa angalizo kuwa Adamu hakuona ambaye angemfaa kama msaidizi wa kulandana nayei, je huku sio kutoa makosa kazi ya Mungu kwamba alipomuumba Adamu aliachia kazi njiani? Kwa kusema Adamu alimuhitaji msaidizi, lugha hiyo inamuumbua mfalme kama muhitaji na mwenye mapungufu. Lakini ni mapungufu gani, mbona ni kimtazama Adamu ninamuona ana miguu na tumbo na moyo na ubongo? Utasemaje hajakamilika? Adamu alilijuaje hilo? Na Mungu alimkamilishaje?

Adamu Mhitaji

Kweli inasumbua kuelewa mfalme aliyepewa kutawala viumbe vyote apatikane na utupu wa  kujazwa. Pamoja na kwamba Adamu alikuwa ndio ametoka mikononi mwa Muumba asiye na kasoro wala doa (akiwa bado kwenye karatasi za kiwandani), kusema ukweli, bado alikuwa hajakamilika. Adamu mwenyewe alitambua hajakamilika alipoendelea na kazi ya kuwapa majina wanyama walipokuwa wanaopita mbele yake. Ninapenda kutazama mawazoni mwangu Adamu akiendelea na kibarua kazi yake ya kwanza ofisini:
ü  Mnyama wa kwanza anapita mbele zake, Adamu anaona mnyama huyo anaweza kumsaidia kulima anamwita Ng’ombe ( na namsikia Adamu akisema, “aha kumbe ninaweza kusaidiwa kulima”).
ü  Adamu anamwona mnyama mwingine wa miguu minne akipita mbele zake, naye anamchunguza anaona anaweza kubeba mizigo na anamwita punda (msikie tena Adamu akisema, “kumbe ninaweza kusaidiwa kubeba mizigo”).
ü  Na tena mnyama mwingine anapita mbele Adamu akikimbia, Adamu anaona huyu anaweza kuchukua haraka atakako kwenda na akamwita farasi (Adamu anasema, “aa kumbe ninaweza kusaidiwa kwenda haraka nitakako kwenda”).
Na kwa utaratibu huo huo wanyama wote wanapita mbele ya macho ya Adamu naye anawapatia majina kulingana na tabia zao na namana wanavyoweza kumfaa. Lakini haraka sana Adamu ameweza kuona wanyama na ndege hao wangemfaa kama wasaidizi chini yake na si wasaidizi sawa naye. Biblia inasema, “hakukuonekana wa kumsaidia Adamu aliteyefanana naye” (mw 2:20b).

Adamu alitamani msaidizi ambaye atafanana naye. Bila shaka hapa Adamu alihitaji mshirika mwenye hadhi sawa naye, mwenye akili sawa naye, mwenye utashi sawa naye: kwa kifupi Adamu alihitaji msaidizi anayelandana naye. Kwa kupewa msaidizi-mshirika wa aina hiyo Adamu hakuwa na haja ya heshima nyingine zaidi ya hiyo. Kama mshirika katika uhusiano wa karibu sana naye kama wa mapenzi msaidizi msaidizi pembeni yake angefanana zaidi na yeye kuliko na ng’ombe na punda na farasi na kasuku. Na ni mwenzi wa aina hiyo tu ndiye angeweza kumpatia heshima ya kiwango sawa naye.

Huwezi kuheshimika mbele ya macho yako kama anayesimama pembeni yako anakiwango cha chini au hauendani naye. Unahitaji msaidizi mnayeweza kuabudu pamoja, mwenye maadili ya juu kama yako, mwenye elimu ya kupelekana, na uzoefu wa maisha ya kufanana. Haikupasi kutofautiana sana na mwenzio kama utapenda kutunza hadhi na furaha uliyopewa na Mungu.

Mungu na Hitaji la Adamu

Kama Mungu angeendelea kumwacha Adamu hivyo hivyo pasipo kumpatia mwenzi wa ndoa tungeona kuwa hitaji la Adamu la ndoa ni la kufikirika tu na si la halisia. Na hapo tungeona Mungu anamchukulia Adamu kama wanyama wengine waliomzunguka. Lakini bahati nzuri haikuwa hivyo. Mungu akatafuta kuumba kiumbe kinachoweza kusimama kandokando mwa Adamu kama mwenzie. Kiumbe hicho ni sharti kisiwe na hadhi ya chini kama ya wanyama hata Adamu ahisi yeye naye ni wa hadhi ya chini kama mwenziye pembeni yake. Na hapo hapo kiumbe hicho kisiwe cha hadhi ya juu kama malaika hata Adamu ahisi ni mtu “bwana mdogo’ kando ya Goliati. Kiumbe huyo atapatikanaje? Mungu akampulizia Adamu dawa ya usingizi. Adamu akalala. Operesheni ikaanza. Na Mungu akachukua ubavu wake mmoja, na kumuumba mwanamke wa kwanza, Hawa. Na Adamu akasema, “sasa huyu ni mfupakatika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu...kwa kuwa ametwaliwa katika mwanamume” (Mw 2:23). Kwa kumpatia mwenziye toka mbavuni mwake, Mungu anahakikisha Adamu anampata mwenziye wa kutembea ubavuni mwake na si miguuni mwake wala kichwani mwake. Sasa Adamu anaweza kutembea kifua mbele kama mwanamume kamili.

Adama aliyeheshimika kwa kupata mke hakuwa na haja ya kuhofia kuumbuka kwa sababu ya mapungufu yake:
ü  Kwa kuwa wanalandana na msaidizi wake, Adamu hawezi kuona haya kupanga mipango pamoja na msaidizi wake (na sio kupasua kichwa mwenyewe),
ü  Adamu anaweza kufanya kazi pamoja na msaidizi wake bega kwa bega (na sio kupindisha mgongo mwenyewe),
ü  Adamu anaweza kutembea pamoja na msaidizi wake mkono kwa mkono (na sio kubaki mwenyewe), Adamu na mkewe wanaweza kuzaa na kulea watoto pamoja, wanaweza kufutana machozi pamoja, wanaweza lala pamoja, amka pamoja, abudu pamoja, ishi pamoja. Adamu alihitaji hakuhitaji mwingine yeyote isipokuwa mwenzi.
Huwezi kufuata nyanyo za Adamu na hawa katika kushirikiana na mwenzio, ukijazia upungufu wa mwenzako, na bado ujisikie mpweke na duni pachoni pako na mbele ya watu.

Mungu na Hitaji la Ndoa kwa Wote

Mwishoni, mwandishi wa kitabu cha Mwanzo akatangaza nia ya Mungu ya mwanamume na mwanamke kuishi kama wamoja katika uhusiano wa ndopo aliposema, “Kwa hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake naye ataambatana na mkewe, nao watakuwa mwili mmoja: (fungu, 24). Kwa kuwa ndoa ni kusudi la Mungu kwa wanadamu lililowekwa wazi kiasi hiki, basi imepaswa kuheshimiwa na watu wote. Usitegemee ndugu zako, wazazi wako, serikali yako wakuheshimu kama wewe mwenyewe huhiheshimu ndoa yako. Wewe ni mwenye kuheshimiwe kama mwanandoa; iheshimu ndoa yako uheshimike.